Ufufuo wa ‘The Menace’ akirejea KPL kwa matao

Taifa Leo - - DIMBA - NA CHRIS ADUNGO

MAPEMA wiki jana, mwanasoka nyota wa zamani wa Harambee Stars, Dennis Oliech aliwafungia waajiri wake Gor Mahia bao la ushindi dhidi ya Mathare United katika mchuano wa Ligi Kuu ya KPL uwanjani MISC Kasarani.

Bao hilo lilikuwa la kwanza la Oliech tangu ajiunge rasmi na miamba hao wa soka ya humu nchini ambao walimpokeza mkataba wa miaka miwili mwanzoni mwa mwaka huu.

Kulingana na kandarasi hiyo, Oliech atakuwa akipokezwa mshahara wa hadi Sh350,000 kwa mwezi, malipo ambayo yanamfanya kuwa mchezaji anayedumishwa kwa ujira wa juu zaidi katika kivumbi cha KPL.

Japo kurejea kwake katika soka ya humu nchini hasa baada ya kuwajibikia klabu mbalimbali za haiba kubwa ughaibuni kunazidi kukosolewa pakubwa, Oliech analeta utajiri mkubwa wa tajriba na uzoefu mpana wa kimataifa katika kampeni mbalimbali za vipute vya humu nchini.

Chini ya mkufunzi Jacob ‘Ghost’ Mulee, maarifa ya Oliech yalitegemewa sana na

Stars katika jitihada za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zilizoandaliwa nchini Tunisia mnamo 2004. Hiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa Kenya kushiriki mapambano hayo ya haiba kubwa.

Hadi alipostaafu katika soka ya kimataifa mnamo 2016, Oliech alikuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Stars baada ya kucheka na nyavu za wapinzani mara 34.

Ubora wa kiwango cha

Oliech hadi kufikia sasa katika ulingo wa soka ni jambo ambalo limemfanya kocha Sebastien Migne anayedhibiti mikoba ya

Stars, kudokeza uwezekano wa kumpanga sogora huyo kwenye kikosi chake cha kwanza katika siku za usoni.

Awali, kocha Hassan Oktay wa Gor Mahia aliungama kwamba Oliech angali na makali ambayo yana uwezo wa kukitambisha kikosi cha Stars katika fainali za AFCON zitakazoandaliwa nchini Misri kuanzia Juni mwaka huu. Akizianika sababu zilizochangia kurejea kwake uwanjani kusakata soka baada ya kustaafu miaka mitatu iliyopita, Oliech, 33, alishikilia kwamba bado angali na miaka mitatu au minne zaidi ya kutamba ugani, na lengo lake kwa sasa ni kuwanyanyulia Gor Mahia taji la 18 la KPL muhula huu.

Mbali na kuimarisha viwango vya ushindani ligini, kuwepo kwa Oliech katika soka ya KPL kutawahamasisha zaidi wachezaji chipukizi wanaopania kujikuza kitaaluma katika ulingo wa kabumbu kiasi cha kutua ughaibuni kusakata soka ya kulipwa katika siku za halafu.

Oliech ambaye pia amewahi kufanyiwa majaribio na Free State Stars ya Afrika Kusini, aliwachezea Mathare United kwa mara ya mwisho mnamo 2003 kabla ya kutua Al Arabi nchini Qatar kisha kujiunga na Nantes, Auxerre na Ajaccio (zote za Ufaransa) na hatimaye kuhamia Dubai Sports Club mnamo 2015.

“Kuna wachezaji ambao huendelea kutesa kwenye ulingo wa kabumbu hadi miaka 37. Mimi hapa nina miaka 33 pekee. Hali ya mwili wangu ni shwari kwa kuwa nimekuwa nikishiriki mazoezi kila Jumatatu uwanjani Woodley,” akatanguliza.

“Nilipoagana na Dubai Sports Club mnamo 2015, nilitaka kurudi Ulaya lakini haikuwa rahisi. Nilielekea Afrika Kusini kwa majaribio lakini mambo yakawa mazito zaidi Free State walipobadilisha kocha mnamo Mei 2018. Maamuzi ya kujiunga na Gor Mahia yalianzia hapo,” akasema.

Kwa mujibu wa Oliech, kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa mfungaji bora wa ligi kwa mabao zaidi ya 25 na kuwanyanyulia waajiri wake ufalme wa taji la KPL.

Mbona Gor Mahia

“Ndugu zangu wakubwa wamepitia Gor Mahia, nami nimeonelea niichezee klabu hii kabla sijastaafu kabisa. Sababu nyingine ni kwamba kuna wachezaji watano ndani ya Gor Mahia ambao nilikuwa nao kambini mwa Stars. Baadhi yao ni George ‘Blackberry’ Odhiambo na Francis Kahata. Hawa wanaelewa mchezo wangu vizuri sana na nitategemea wawe wakinipokeza mipira mizuri ya kufunga mabao muhimu,” anasema Oliech kwa kukiri kwamba amepokelewa vizuri na wachezaji wenzake, na wala hatajichukulia kuwa spesheli zaidi ya wengine.

“Sikurudi mpirani kwa sababu ya pesa, ila ni mapenzi yangu ya kusakata boli. Nikilinganisha mshahara wa sasa na pesa nilizokuwa nikipokezwa huko Ulaya, huu ni ujira mdogo sana,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba tayari amewekeza kwenye biashara za vyakula na amenunua ardhi na nyumba kadhaa.

Amtema mpenzi

Nasra Salim almaarufu Meg C au Kidoli amepania kulifufua penzi lake kwa Oliech ambaye kwa sasa ametemana na kichuna Paula Mumia aliyemdokolea tunda kwa yapata miaka sita.

“Nimewasikia baadhi wakisema eti sina mpenzi. Ninamchumbia ‘D’ na nimeolewa. Nadhani unajua jibu,” Meg C aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook. Akimjibu mmoja wa mashabiki wake aliyempongeza kwa kumpata mpenzi, Meg C alikiri kuteswa na penzi la zamani na raha yake itakuwa ni kurudiana na dume lake.

“Wajua moyo wangu ni wa nani. ‘D’ amenifanya wazimu wa mapenzi 2019,” akasema.

Japo haijabainika wazi ‘D’ ni nani, lakini kwa mtazamo wa jinsi Meg C alivyozamia suala hilo na matukio ya hivi majuzi, huenda mpenziwe wa zamani Oliech ndiye aliyekuwa mrejelewa kwenye jumbe zake. Wawili hao walikuwa wakitoka pamoja kimapenzi mnamo 2000 lakini wakatengana baada ya mwaka mmoja wa kuchumbiana. Meg C alimsuta Oliech kwa kutokuwa tayari kufunga ndoa naye.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.