Ubora wa miundo-misingi kiini cha Misri kupokezwa uenyeji wa fainali za AFCON

Taifa Leo - - DIMBA - Abuso ni mtangazaji wa michezo katika Radio France International, Tanzania

MISRI itakuwa mwenyeji wa fainali za soka kwa mataifa bingwa ya Afrika zitakazofanyika kuanzia Juni 13 hadi

Julai mwaka huu.

Uamuzi huu ulifanywa baada ya

Kamati Kuu ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), kukutana jijini Dakar nchini Senegal wiki jana. Hatua hii ilikuja baada ya Cameroon mwishoni mwa mwaka 2018, kupokonywa nafasi ya kuwa mwenyeji wa taji hilo kwa sababu za kiusalama na maandalizi mabaya.

Cameroon ingefanikiwa kuandaa fainali hizo, ingekuwa mara yake ya kwanza tangu mwaka 1972. Hakika ingetoa matumaini makubwa ya kutetea tena taji hili kama wenyeji kwa sababu walishinda mwaka 2017.

Itakuwa mara ya kwanza kwa michuano hii kushirikisha timu 24 badala ya 16, kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa wakati wa michuano hii mikubwa ya bara la Afrika.

Kenya ambayo mara ya mwisho ilishiriki katika fainali hizi miaka 15 iliyopita, imerejea kwa mara nyingine kutafuta ubingwa wa taji hilo.

Lakini je, nini kilichoisaidia Misri kushinda nafasi hii ya kipekee ya kuandaa taji hili la AFCON? Kabla ya kufafanua hilo, ni vyema kufahamu historia ya nchi hii kuwahi kuandaa AFCON katika miaka iliyopita.

Hii itakuwa mara ya tano kwa Misri kuwa mwenyeji wa fainali hizi, iliyoziandaa kwa mara ya kwanza miaka karibu 60 iliyopita. Mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1959, iliyokutanisha matafa matatu ambayo yalianzisha taji hili ambapo pamoja na wenyeji Misri, kulikuwa na Sudan pamoja na Ethiopia.

Kuelekea michuano hii, mechi 51 za kutafuta ubingwa wa taji hilo, zitachezwa katika viwanja vinane katika miji mitano ya nchi hiyo ikiongozwa na Cairo, Alexandria, Ismailia, Suez na Port Said.

Baada ya kusema hayo, Misri kupewa nafasi hii katika dakika za lala-salama, ni wazi kuwa kitu kikubwa ambacho wajumbe wa CAF waliangalia ni miund-mbinu ya viwanja, ambavyo vitatumiwa wakati wa mechi hizo.

Cameroon ilikosa viwanja vya kutosha na hii ilikuwa sababu kubwa ya kupokonywa haki za kuandaa michuano hii. Natumai unakumbuka changamoto hii pia iliwahi kuikumba Kenya wakati ilipopewa nafasi ya kuandaa michuano ya CHAN mnamo 2018.

CAF ilichukua hatua hiyo kwa sababu ya miundo mbinu mibaya hasa viwanjani, hadi dakika za lala-salama, ni uwanja wa Kasarani tu ndio ulionekana tayari kuandaa michuano hiyo.

Mbali na viwanja, suala jingine muhimu la kuangalia katika kuamua ni nani anaanda fainali hizi, ni hoteli. Je, wachezaji, wageni mashuhuri na mashabiki wanaokwenda kushuhudia fainali hizi watalala wapi? Bila shaka, kwa uamuzi huu wa Misri, hili ni jambo ambalo lilifanywa kwa usahihi mkubwa kwa sababu miji iliyotajwa ina hoteli za kifahari mno kutokana na nchi hiyo kuwa nchi ya kitalii.

Jambo la mwisho ambalo huangaliwa ni usalama wa nchi husika. Kundi la waasi katika maeneo yanayozungumza Kiingereza na uwepo wa kundi la kigaidi katika mpaka wa Nigeria na Cameroon ilikuwa sababu nyinginezo zilizofanya nchi hiyo kukosa nafasi hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.