Rais Ramaphosa atangaza vita vikali dhidi ya ubakaji

Taifa Leo - - HABARI ZA AFRIKA NA DUNIA - Na MASHIRIKA

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameomba wanaume waungane dhidi ya ubakaji na dhuluma za kingono nchini humo akitaja visa hivyo kuwa "hatari kubwa ya kitaifa".

Alisema inasikitisha jinsi wanawake wanazidi kubakwa na kuuawa kila kukicha na sasa wakati umefika kukomesha dhuluma za kijinsia.

Alitoa wito huo alipokuwa akizundua manifesto ya kusimamia Chama cha African National Congress (ANC).

Karibu visa 40,000 vya ubakaji huripotiwa nchini humo kila mwaka na inasemekana idadi hiyo ni ndogo kwani kuna visa vingine vingi ambavyo huwa havifikishwi kwa asasi husika.

Mbele ya makumi ya maelfu ya wafuasi wake, rais alitumia hotuba yake katika uwanja wa michezo wa Durban kuambia wanaume wasimame kidete kuonyesha kujitolea kwao dhidi ya ubakaji wa wanawake. "Tumepiga hatua kubwa kuboresha nafasi ya wanawake katika jamii...lakini dhuluma za kijinsia ni hatari ya kitaifa ambayo tumejitolea kukomesha ili wanawake na wasichana wa Afrika Kusini waishi kwa amani, usalama na hadhi ya utu," akasema.

"Ukombozi wa wanawake unahitaji marekebisho ya tabia na hali zinazochangia ukandamizaji na kutengwa kwa wanawake," akaongeza. Aliorodhesaha mikakati mbalimbali ambazo zinaweza kusaidia katika juhudi hizi, ikiwemo adhabu kali zaidi dhidi ya wabakaji na utaalamu bora zaidi wa polisi na viongozi wa mashtaka ili waboreshe uwezo wao wa kuchunguza na kushtaki aina zote za uhalifu.

Kwa jumla, manifesto ya ANC ilikuwa na ahadi za kurekebisha uchumi na kupambana na ufisadi huku chama hicho tawala kikitaka kuvutia wapigakura zaidi kabla uchaguzi wa wabunge ufanywe Mei. Chama hicho cha Nelson Mandela ambacho kimeongoza Afrika Kusini tangu utawala wa wabeberu uliposhindwa miaka 25, kinatarajiwa kushinda katika uchaguzi huo kwa mujibu wa kura za maoni licha ya kukumbwa na changamoto tele zilizofanya umaarufu wake upungue na kusababisha migawanyiko ndani ya chama.

Umaarufu wake ulipungua kutuatia sakata tele za ufisadi na ubadhirifu wa fedha zilizoibuka wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais Jacob Zuma, ambaye aliondolewa mamlakani Februari mwaka uliopita baada ya kuongoza kwa miaka tisa. Mapema wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya miaka 107 tangu chama kilipoundwa, Ramaphosa alikiri kuwa kwa miaka kadhaa sasa, "chama chetu kimeshindwa kuridhisha matarajio ya wananchi wetu".

Alisema ANC sasa ina mwongozo bora zaidi utakaosaidia kuimarisha uchumi, kutoa nafasi zaidi za ajira na kupunguza umaskini.

Picha/afp

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ahutubia vyombo vya habari katika mkutano wa chama cha ANC nchini humo majuzi. Ramaphosa amewaomba wanaume waungane dhidi ya ubakaji akiutaja kama hatari ya kitaifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.