Kisiwa cha Lamu sasa chatarajia viwanja vya kisasa vya kupigia gozi

Taifa Leo - - DIMBA - NA ABDULRAHMAN SHERIFF Dimba (kati) (kuhsoto) Picha/abdulrahman Sheri

KISIWA cha kihistoria cha Lamu kinatarajia kuwa na viwanja viwili vikubwa vya kisasa iwapo ahadi zinazotolewa zitatimizwa karibuni.

Wakati habari iliyotolewa na Serikali ya Kaunti ya Lamu ya kuujenga upya uwanja wa zamani zaidi wa Twaifu zilipokewa kwa furaha na wakazi wa kaunti hiyo, mfanyabiashara maarufu amejitokeza kueleza mipango ya kujenga uwanja mwingine wa kisasa Kisiwani humo.

Uwanja huo wa Twaifu ulioko Kisiwani Lamu ndio wa pekee ambao hautoshelezi kwa mahitaji ya klabu zilizoko katika kaunti hiyo ambayo ina timu nyingi zikiwemo za wanasoka wakubwa na vijana chipukizi.

Kwa ufumbuzi wa kuhakikisha kuna kiwanja zaidi ya kimoja cha kisasa kipo katika kaunti hiyo, Mwenyekiti wa Lamu Cultural Festival Group (LCFG), Alwy Ghalib Ahmed almaarufu ‘Bush’ amefahamisha kuwa anapanga mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa uwanja mwingine unajengwa Kisiwani hapo.

Bush anasema ana mipango kabambe anayoazimia kuitekeleza akishirikiana na Gavana wa kaunti hiyo, Fahim Twaha pamoja na wakuu wa Shule ya Upili ya Lamu Boys juu ya uwezekano wa kujenga uwanja wa kisasa katika uwanja ulioko wa shule hiyo.

Bush amesema wana nia ya kujenga uwanja huo mwingine miezi michache ijayo kwa ajili ya kusaidia vijana kuweza kucheza soka kwenye mazingira yatakayowafanya waendeleze vipaji vya uchezaji wao.

Kinara huyo wa LCFG anasema azma yake kubwa ni kutaka kuanzisha timu ya mseto ya kaunti hiyo ya Lamu ambayo itatoa wachezaji wazuri kutoka sehemu zote za kaunti na kuiweka pamoja na kuutumia uwanja huo kwa mazoezi pamoja na mechi zao.

“Tunaazimia kuanzisha timu ya North Coast Football Club ambayo itaendeshwa kitaalamu na ambayo wachezaji wake watakuwa pamoja na nina uhakika baada ya muda wa miaka michache, itaweza kuwa timu yenye uwezo wa kupambana na timu yoyote kubwa nchini,” akasema.

Alikuwa na matumaini makubwa kikosi cha timu hiyo kitaweza kufanya ziara ya kutembelea sehemu mbalimbali za nchi na nchi jirani kwa ajili ya wachezaji wake wapate kuonekana na kuvutia kusajiliwa na klabu kubwa.

Bush anasema timu hiyo itakuwa ya kikosi cha wachezaji 20 watakaokuwa kati ya umri wa miaka 18-25 na ana nia kubwa ya kuona kuwa baada ya kipindi cha miaka miwili, watafanya mipango ya kuwaita maskauti kutoka Uropa na sehemu nyingine kushuhudia wenye vipaji.

Anataka kuhakikisha kwamba talanta za sehemu hiyo hazipotei bure.

“Tuna chipukizi wengi wenye vipaji vya kucheza soka ya kawaida pamoja na soka ya ufukweni, lakini kunahitajika kuwe na mipangilio ambayo yatawezesha wachezaji wetu kuonekana wapate kusajiliwa na klabu nyingine za hapa nchini na ng’ambo,” akasema Bush.

Bush alisema anatarajia kuutekeleza mradi huo kwa njia za uwazi na hata ataomba kibali kutoka kwa Wizara ya Nchi za Kigeni kwa ajili ya kutafuta wadhamini kutoka mataifa ya ng’ambo.

“Nina imani kubwa tutaweza kufanikiwa kwa hilo,” akasema.

Anasema ana matumaini makubwa sio kwa wafadhili wa ng’ambo pekee, bali pia ana imani wafanyabiashara maarufu wa hapa nchini watajitolea kusaidia kwa mradi huo wa kuwafanya vijana wapendelee kucheza soka na kujiepusha na majanga yaliyoko ya utumizi wa dawa za kulevya na maovu mengine.

Aliahidi kufuata kanuni na mipangilio kwa kushirikiana na washikadau wakiwemo maofisa wa tawi la Pwani Kaskazini la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na uongozi wa kaunti hiyo chini ya Gavana Twaha kuhakikisha uwanja wa Lamu Boys unakuwa wa Multi Sports Stadium.

Bush ambaye ni mwanasiasa amesema, ameamua kushirikiana na washika dau wengine kwa sababu ya manufaa ya vijana wa sehemu hiyo ambao wana vipaji vya kusakata soka lakini hawapati mahitaji ya kuendeleza vipaji vyao vipate kuonekana.

Kinara huyo amewataka wanasiasa wa eneo hilo wazike tofauti zao za vyama na wafanye kazi kwa ushirikiano na hasa juu ya michezo ambayo anaamini yanaweza kuwa dawa tosha ya kuwafanya vijana wajiepushe kutekeleza mabaya yoyote.

Uwanja wa Twaifu ambao ndio unaochezewa mechi nyingi una tifu la mchanga na mara kwa mara viongozi wamekariri kujitolea kuujenga lakini unabakia hivo ulivyo. Lakini Mwenyekiti wa FKF tawi la Pwani Kaskazini, Fuad Ali Adi aliambia Dimba kuwa serikali ya Lamu iko mbioni kukamilisha mipango na huenda ukaanza kujengwa wakati wowote mwaka huu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.