Sharks yazima Stima, Ulinzi Stars ikilipua kambi ya Sony

Taifa Leo - - SPOTI - NA GEOFFREY ANENE

KARIOBANGI Sharks ilivunja rekodi ya Western Stima ya kutoshindwa kwa kuichapa 2-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos na kudumisha rekodi yake ya kutoshindwa hadi mechi saba kwenye Ligi Kuu, jana.

Nayo Ulinzi Stars ilimaliza ukame wa mechi tisa bila ushindi dhidi ya Sony Sugar kwa kuinyuka 2-1 mjini Awendo kupitia mabao ya Enosh Ochieng’ yaliyopatikana dakika ya 25 na 74.

Mabingwa wa Kombe la Ngao, Sharks walivuna ushindi huo wao wa pili mfululizo dhidi ya Stima kupitia mabao ya George Abege na Harrison Mwendwa.

Bao la kwanza lilipatikana baada ya Abege kugeuka vizuri ndani ya kisanduku na kusukuma kiki nzito hadi wavuni dakika ya pili. Mwendwa aliongeza bao la pili kabla tu ya mapumziko baada ya kuukunja mpira vyema mbali na kipa Samuel Odhiambo kutoka nje ya kisanduku alipopokea kona safi. Stima ilirejesha bao moja mapema katika kipindi cha pili pale kipa John Oyemba, ambaye alikuwa anarejea kikosini, alipopangua vibaya mpira wa kutupwa na kuadhibiwa na Herbert Kopany aliyevuta shuti kali hadi wavuni.

Sharks iliingia mchuano huu bila ushindi katika mechi mbili zilizotangulia dhidi ya Mount Kenya United na KCB.

Iliteremka uwanjani Kenyatta na rekodi nzuri dhidi ya Stima ya ushindi mmoja na sare moja. Iliwika 1-0 zilipokutana mara ya mwisho Agosti 23 mwaka 2017 kabla ya Stima kutemwa mwisho wa msimu huo.

Stima, ambayo imerejea Ligi Kuu msimu huu, baada ya kushinda Ligi ya Supa mwaka jana, ilipata nafasi chache za kufunga mabao ikilinganishwa na Sharks iliyopoteza nafasi chungu nzima.

Mbali na Ulinzi, ambayo ilicharazwa na wanasukari hawa 1-0 nyumbani na ugenini msimu uliopita, kulipiza kisasi dhidi ya Sony, ilimaliza ukame wa mechi nne bila ushindi msimu huu.

Sony ilifunga bao la kufuta machozi kutoka kwa Maxwell Onyango dakika ya 80.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.