Nyani wahangaisha walevi kwa kuwapokonya pombe

Siku hizi uhalifu unatekelezwa na nyani na wakati mwingine huwapokonya watoto vitabu kila wanapotoka shuleni

Taifa Leo - - FRONT PAGE - NA RICHARD MAOSI

KATIKA mji wa Nakuru, mitaa imepewa majina kutokana na sifa zake au hali halisi ya maisha. Mojawapo ya maeneo hayo ni mtaa wa Manyani ambapo kwa muda mrefu nyani na tumbili wamekuwa wageni bila mwaliko katika nyumba za watu.

Idadi kubwa ya nyani hufunga safari kutoka kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Nakuru, na kuelekea kwenye mashamba na makazi ya watu bila kuogopa chochote.

Wakati Taifa Leo ilikita kambi eneo hili kupekua taarifa hizi kwa kina, tulikumbana na viumbe hawa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida lakini walipogundua sisi si wenyeji walionekana kusitisha shughuli zao na kututazama.

Wakazi wengi wanasema wamekuwa na changamoto kuwakabili, na juhudi zao za kuwaangamiza zimeambulia pakavu huku wakiomba usaidizi kutoka kwa serikali ya kaunti ambayo imefumbia macho janga hili.

MAHANGAIKO

Waliokuwa wakiweka ulinzi mkali wa mbwa nao wamebadilisha mtindo walipogundua mbinu hiyo haisaidii, pale wanaposhambuliwa na kutiwa majeraha kutokana na kichapo cha kundi la nyani usiku.

Dickens Ngota anasema amekuwa akiishi hapa kwa miezi sita. Anaungama kuwa wakazi wanafaa kujilaumu kwani wao ndio waliamua kuwakaribisha nyani katika maisha yao ya kibinafsi kwa dhana kuwa wangekuwa marafiki.

Aidha, nyani wanapokosa chakula msituni, huruka seng’enge iliyozunguka mbuga ya Nakuru na kuvunja nyumba za watu bila kujali wakitarajia kulishwa kwa lazima au kuiba.

“Wiki iliyopita nilimkuta nyani akitokea dirishani baada ya kuchukua mayai ya kuku wangu. Siku hizi uhalifu unatekelezwa na nyani ambao wamegeuka kuwa majambazi sugu, wakati mwingine hata wamekuwa wakiwapokonya watoto vitabu wanapotoka shuleni,” alisema.

Tony Mogaka asema nyani hawaogopi wanawake, na ndio sababu wanapenda kuzuru makazi yanayolindwa na akina mama. “Wanawake wamekuwa wakiwabembeleza, kuwapa chakula na kuwakaribisha nyumbani na hii ndiyo sababu kuwatimua itakuwa ni kazi ngumu,” Tony alisema.

WANAPENDA MLO

Wameendeleza tabia ya kuteka mali peupe na kuwapokonya wakazi vitu kama vile mkate na maziwa wakitoka dukani. Wengine hufika katika maboma ya watu wakiwa wamebeba mikebe ya kutiliwa chakula.

Betty Maina anasema alilazimika kuhama mtaa wa Manyani hadi Free Area kwa sababu siku moja kundi la tumbili lilimvamia jikoni na kubeba unga wote alipokuwa akitaka kuandalia familia yake chakula cha jioni baada ya kazi.

“Hawa wanyama hawana adabu hata kidogo. Wamekuwa kizingiti kikubwa cha maendeleo, hata sijui walitoka dunia gani,” alilalama.

Kitoweo cha nyama choma barabarani sasa ni maarufu katika mtaa wa Manyani baada ya mtindo wa nyani kuuawa na wakazi kisha kuliwa kuongezeka.

Lakini wafanyabiashara kwa hakika wanaendelea kujipatia hela za haraka na kuwavutia wateja wengi wanaomiminika kila siku vibandani kula mutura ya bei nafuu.

NYAMA YA NYANI

Inahofiwa wengi wa wakazi hapa wamekuwa wakiburudika kwa nyama ya nyani au tumbili bila kujua huku maswali mengi kuliko majibu yakiibuliwa kwa walinzi wa mbuga endapo wamekuwa wakishika doria.

“Mchana utawakuta nyani wameshinda na watu lakini baadaye wanatoweka bila kujulikana wameenda wapi,” alitufichulia Dan Misik. Wakazi hapa walikoma kula nyama za mutura njiani baada ya kukuta mizoga ya nyani vichakani inayoshukiwa imekuwa ikitumika kuandaa nyama na supu.

Walevi kwa upande mwingine wamelalamikia taabu wanazopata mikononi mwa nyani.

Baadhi yao huhofia kurejea nyumbani wakiwa wamechelewa wakiogopa kushambuliwa na kucharazwa na nyani wanaowasubiri njiani.

KUPOKONYA WALEVI POMBE

Erick Sule anasema alilazimika kukomesha mwenendo wa kubugia vileo jeshi la nyani lilipompokonya chupa ya bia usiku wa kuamkia mwaka mpya.

“Walinifuata hadi karibu na nyumba yangu kisha wakachukua bia niliyokuwa nimenunuliwa na rafiki yangu. Waliinywa kwa zamu wakikimbilia usalama wao mbugani nilipotaka kuwatia adabu!” alisimulia.

Wanyama hawa pia hawawaogopi wanabodaboda ambao wanakiri biashara yao imevurugwa sana huku wakati mwingine nyani hao wakiwapokonya funguo za pikipiki zao.

“Majuzi niliacha ufunguo kwenye pikipiki yangu. Niliporudi nikataka kuiwasha nihudumie mteja, nilipata nyani mmoja amechukua ufunguo huo na kuukatalia. Sasa ilinibidi nimbembeleze anipe lakini wakati mwingine wao hukataa na kutokomea msituni,” anasimulia Gabriel Kiptoo ambaye ni mwanabodaboda eneo hili.

Mtaa wa Manyani unapakana na mbuga ya Nakuru katika sehemu ya Kusini ambapo nyani hawa huingiliana kuwa cha wakazi wakilia hoi.

“Nyani na wanyama wengine wamekuwa wakivuka uzio na kuingia mitaani Kaptembwa, Shaabab, Rhonda na Free Area. Hata uweke ulinzi namna gani, bado watavuka ua,” Sule alieleza.

Hata hivyo, walinzi wa mbuga wanawalaumu wakazi kwa kuwalisha nyani, licha ya marufuku kutoka kwa Wizara ya Utalii.

Kila unapokaribia mbuga ya Nakuru utaona mabango yaliyoandikwa ‘Usimpe Nyani Chakula’.

Lakini raia wamekuwa wakipuuza ilani hii na kuwarushia maganda ya ndizi na mabaki ya chakula mita chache karibu na mbuga jambo linalowaka r ibisha mita ani.

Naibu Kaunti Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Bw Herman Shambi alisema wakazi ni wa kulaumu kwani ndio huwapatia nyani chakula na kuwavutia kutoka mbugani.

“Ni lazima wakazi wakomeshe tabia ya kuwapatia nyani njugu na ndizi sokoni endapo wanataka kupunguza kero la nyani mitaani,” alisema.

Picha/richard Maosi

Nyani akiwa amepanda kwenye pikipiki bila kuogopa watu.

Picha/richard Maosi

Mkazi akimfukuza nyani.

Picha/richard Maosi

Nyani mtundu akipanda kwenye ukuta wa makazi ya watu bila woga.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.