NYSA tupa imara inayonoa wanasoka wa haiba kubwa

Taifa Leo - - GUMZO LA SPOTI - NA RICHARD MAOSI

KIKOSI cha NYSA FC U-13 kinajumuisha vijana kutoka familia maskini viungani mwa mji wa Nakuru ikiwemo Kaptembwa, Langalanga, Freehold, Rhonda na Lanet. Wamevalia njuga mchezo wa soka wakiamini kipaji kinalipa endapo kitatumika vizuri. Mkufunzi Kevin Adiko alitengeneza kikosi cha vijana 30 mnamo 2014 akipania kutambua talanta za wanafunzi wa shule za msingi. Alisuka timu ya Nakuru Youths Sports Association (NYSA) kwa weledi kabla ya kuishirikisha katika michuano ya FKF nchini.

Akizungumza na Dimba, Adiko alisema aliteua kikosi cha kwanza kulingana na uwezo wa wachezaji.

“Baada ya majaribio ya muda mrefu, safu ya kiufundi ilikuwa na mchango wa aina yake kutengeneza kikosi cha kwanza,” alisema. Uwanja wao wa nyumbani ni Liberty stadium Afraha. Siku za wiki wao hufanya mazoezi katika shule ya msingi ya Freehold au Mazembe Grounds. Wakivalia jezi rasmi ya manjano na kaptura nyeusi. Mbali na kuwavutia mashabiki wengi ni mfano bora wa kuigwa kwa timu za mashinani.

Lengo la kubuni NYSA lilikuwa ni kuimarisha ushindani katika ligi za mitaani almaarufu kama Inter-estate Competition. Kuendeleza vipaji hivyo vilihitaji ushirikiano wa washika dau wote huku wazazi wakiwa nguzo muhimu katika ufanisi wa timu. NYSA ni timu ambayo desturi yake kutandaza mpira uliokwenda skuli ni wa kipekee, aidha inaibukia kuwa miongoni mwa vikosi vya wachezaji wachanga katika kaunti ya Nakuru na ukanda wa bonde la ufa tawi la Magharibi.

Wakiwa wapinzani wasiokuwa na mfano, msimu uliopita 201819 walimaliza ligi ya FKF kaunti ya Nakuru, wakiwa nambari moja baada ya kuzoa jumla ya alama 68. NYSA imevuka mipaka na kuwa hazina ya kuzalisha zana katika ligi ya KPL. Mmoja wa wachezaji aliyechipukia hapa ni Sydney Lokale wa Kariobangi Sharks alianzia taaluma yake katika timu hii ya mtaa ambayo zamani ilifahamika kama Nakuru Youth. Akapanda daraja hadi aliposajiliwa na Nakuru All Stars na baadaye Kariobangi Sharks.

Wachezaji wanasema ufanisi wa timu unatokana na uwelewa baina yao na mkufunzi. Kujituma uwanjani pamoja na kufanya mazoezi kila siku. Wanatumia kila fursa wanayopata kujifua wakipania kutengeneza kikosi cha timu za baadaye nchini kwa mfano Harambe Stars. Kampeni yao mwaka huu imeanza kwa mshindo.

Picha/richard Maosi

Nakuru Youth U-13 kabla ya mechi ugani Afraha dhidi ya Twomoc FC.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.