Washairi waomboleza kifo cha Malenga wa Mvita

Ahmad Nassir Juma Bhalo ni kakaye mshairi Abdilatif Abdalla ambaye ni mtunzi wa diwani maarufu ya ‘Sauti ya Dhiki’

Taifa Leo - - UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI - Na CHRIS ADUNGO [email protected]

PENGINE njia maridhawa zaidi ya kumpa tunu marehemu Ahmad Nassir Juma Bhalo si kuomboleza kifo chake kilichotokea wiki jana baada ya kuugua kwa muda mfupi – hasa wakati ambapo taaluma ya Kiswahili ilikuwa bado ikimhitaji mno – bali ni kutafakari kuhusu upekee wa mchango wake katika uwanja wa ushairi aliouchangamkia kwa moyo wa dhati.

Si kauli wala tungo zenye maneno yaliyo na uzito sawa na huu zilitolewa wiki jana na wapenzi, wakereketwa, wasomi, wataalamu na watetezi wa Kiswahili pindi baada ya Ustadh Juma Bhalo almaarufu ‘Malenga wa Mvita’ kuaga dunia.

“Jina lake halitawahi kukosekana katika orodha ya watetezi na wafia-lugha waliojihini na kujikusuru kwa hali na mali kuchangia ustawi na maendeleo ya Ushairi wa Kiswahili.”

“Kifo kimetupiga pute johari adimu na kito cha thamani. Kuondoka kwa Malenga wa Mvita ni msiba mkubwa mioyoni mwa wapenzi wa Kiswahili na pengo aliloliacha kitaaluma haliwezi kabisa kuzibika,” akasema Mwalimu Henry Mjileo Indindi aliyenukuu beti chache za ‘Utenzi wa Mtu ni Utu’ uliotungwa na marehemu Ahmad Nassir: Ukimuona mwenziyo, Afanya mambo yasiyo, Mkenye hali iwayo, Asaa akaridhiya. Mkanye kwa taratibu, Wambe naye kwa adabu, Wala usione tabu, Kumuonya lenye ndiya.

Malenga wa Mvita ni kaka wa Profesa Abdilatif Abdalla, mtunzi wa diwani maarufu ya ‘Sauti ya Dhiki’. Pia ni kakaye mutribu maarufu wa Uswahili, marehemu Mohamed Khamis almaarufu Profesa Juma Bhalo, Sheikh Abdillahi Nassir, Sofia Khamis na Khalid Khamis.

Beti za hapa chini zilitungwa na Bw Indindi, mwandishi mahiri ambaye kwa sasa ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Laikipia: “Maisha ni mshumaa, kuwaka na kuyeyuka, Hakuna wataokaa, pasi kilele kufika,

Kama matwana hutua, msafiri akifika,

Sasa zamu imefika, ya kushuka Ustadh”. Ni pigo kwa washairi, toka Kenya hadi Bongo, Ametuwacha mahiri, aliye nguli wa tungo, Mungu kampa safari, katuwachia ulingo, Mola mfanzie kheri, Ahmad Nassir Bhalo.

Wakitumia mtandao wa Facebook na Ukumbi wa Sokomoko katika gazeti hili la Taifa Leo, watetezi wengi wa Kiswahili walimkumbukia Ahmad Nassir kupitia beti za ushairi. Katika mojawapo ya beti zake, Swaleh Suheil Abeid kutoka Mombasa alisema: Tuombe kwake Karima, radhize kumridhia, Apate malazi mema, dhunubi kumfutia, Abarikiwe neema, na peponi kuingia, Ewe Mola mrehemu, Ahmadi wa Nasiri.

Mawazo yake yaliendelezwa na mshairi Hassan R. Hassan kutoka Tanga, Tanzania ambaye aliandika: Alikuwa ni wakili, wa Kiswahili bayana, Kakikuza kila hali, wala tabu hakuona, Hae! Kafa huyu nguli, uchungu mkubwa sana, Katutoka muungwana, Ahmad wa Nassir. Nia yake njema kweli, alitaka kuiona, Lugha inafika mbali, kwa usiku na mchana,

Kifo kimetukatili, kumtwaa huyu bwana, Katutoka muungwana, Ahmad wa Nassir.

Akielezea masikitiko yake kutokana na kifo cha Ahmad Nassir, mshairi Edison Wanga kutoka Mombasa aliandika: Vichwa vyetu vinagonga, kupata hizi habari, Mawazo yanatuzonga, kutuondoka Nasiri, Kwa ushairi ni kunga, wa kupanga misitari, Makiwa kwa familia, ya Malenga wa Mvita. Ushairi naboronga, simfikii Nasiri, Ni shaha wa umalenga, waziwazi nalikiri, Kwenye safu ni nyakanga, kwa kutunga ni hodari, Makiwa kwa familia, ya Malenga wa Mvita. Na ‘Taa Ya Umalenga’, ni diwani ya Nasiri, Kuna zingine katunga, zinavutia si siri, Uliza Mwana wa Kanga, atoka kwa yake mbari, Makiwa kwa familia, ya Malenga Wa Mvita. Washairi wengine waliomboleza kupitia beti zao kama ifuatavyo: SALIM HUSSEIN NG’ANZI ‘Jemedari’

Tanzania.

Washairi tumefiwa

Makiwa jama makiwa, umetufika msiba, Washairi tumefiwa, huzunini tumeshiba, Tumebaki ja wakiwa, pengole gumu kuziba, Washairi tumefiwa, katutoka Juma

Bhalo. Duniani tunapita, na hakuna wa kubaki, Ni Malenga wa Mvita, ameitwa na Razaki, Kuitika hakusita, kuliendea handaki, Washairi tumefiwa, katutoka Juma Bhalo. Ana diwani kadhaa,

Juma Bhalo kazitunga, Mojawapo ya sanaa, ni

‘Taa ya Umalenga’, Waswahili zatufaa, Kiswahili kukichunga, Washairi tumefiwa, katutoka Juma Bhalo.

Tumefiwa tena!

Ai! Tena tumefiwa, mekigwa mti mkuu, Watu tumeondokewa, amefariki mkuu, Twalia kama ngekewa, kwa nini msimu huu? Ustadhi Juma Bhalo, Ahmadi hayu nasi. Ai! Malenga hisiwa, enda kwa aliye juu, Guru alojaaliwa, alotumega makuu, Na haikutarajiwa, hasa kwetu wake nduu, Ustadhi Juma Bhalo, Ahmadi hayu nasi. ULEDI BRYAN ‘Kinda Mtunga Nudhumu’ Anester Victory, Nakuru

Kwaheri Malenga

Ai! Ametoka nguli, malenga alosifika, Amemtaka Jalali, siku zimekamilika, Ni msiba kwelikweli, watunzi twahuzunika, Mungu ampe sahali, peponi aweze fika. Ai! Ahmadi Nassiri, Juma Bhalo kaukata, Yatiririka tiriri, machozi siwezi futa, Mjuzi wa mashairi, Mwenyezi amemuita, Safiri njema safari, we Malenga wa Mvita. Ai! Hayuko mfunzi, jagina wa mapokeo, Ametutia majonzi, anakafiniwa leo, Dua yetu wanafunzi, aendapo jongomeo, Ing’ae yake kurunzi, kuzimu apande cheo. SULEIMAN ABDALLAH BAMBAULO ‘Nge Mpole’

Buriani Malenga

Hayaniishi machozi, kila nikifikiria, Ameondoka mlezi, hayupo tena dunia, Ingawa imi siwezi, kudura nakubalia, Buriani Juma Bhalo, Malenga wetu Mvita. Sina amani moyoni, kwa kututoka farisi, Alifunza limbukeni , tukiwa ni wafuasi, Kwa amri ya Manani, ameondoka wepesi, Buriani Juma Bhalo, Malenga wetu Mvita. Aliumanya utunzi, tena wa kimapokeo, Ungedhani mfinyanzi, aliyebobea cheo, Kweli tunayo simanzi, bingwa amelala leo, Buriani Juma Bhalo, Malenga wetu Mvita. MOSES CHESIRE ‘Sumu ya Waridi’

Kitale

Malenga wa Mvita

Mola walile na hilo, Muumba naliombalo, Nitimiziya timilo, takalo nilitakalo, Lijiri hilino lilo, himahima malomalo, Ahmadi Nasiri Bhalo, nalale mema malalo. Naomboleza halilo, peponi nawe malalo, Andamane milomilo, palo masahaba palo, Jaza za dhawabu zilo, njema jazano ziwalo, Ahmadi Nasiri Bhalo, nalale mema malalo. Sikuye yafufulilo, hiyo siku midahalo, Siku ya ndilo lisilo, siku yako magagalo, Amali zilo za kilo, yujuru zuru yuwalo, Ahmadi Nasiri Bhalo, nalale mema malalo. ABDALLA ALI SHAMTE “DP” Mwembekuku, Mombasa

Malenga ameondoka

Ilahi natakadimu, jinalo kulibashiri, Kwa hino nzito yaumu, kwetu iliyotujiri, Meondoka muadhwamu, wa tungo za ikirari, Mjomba Ahmad Nassiri, nmeondoka duniani. Ilahi sina kauli, na fikira zatatana, Mate yakuwa subili, ya utungu tena sana, Ya Rabbi nipa sahali, nipate viunga vina, Mjomba alo jagina, meondoka duniani. Ndiye nguli wa manguli, mbuji alotimiya Atongowapo kauli, na vina kupaliliya, Urari uso mithali, tungoni utaeneya, Yailahi mnyosheya, ndiyae aendako. Ya sahali mjombangu, kaburile mkunduliye, Alohiti kilimwengu, dhambize mghufiriye, Umpee jema fungu, peponi ashukiye, Ya Rabbi msahilishiye, mjombangu Ahmadi. AWADH BASHIEKH ‘Mwana wa Kanga’ MAISHAYA AWALI Ustadh Ahmad Nassir ni Mswahili

wa Mombasa ambaye babaye alitokea katika nasaba ya Tangana huku mama akitokea ukoo wa Kilindini. Haya ni miongoni mwa makabila ya asili ya Waswahili wa Mvita, yaani mombasa.

Ustadh Ahmad alizaliwa mtaani Kuze, Mombasa mnamo Mei 26, 1936 na akaaga dunia mnamo Januari 9, 2019.

Baada ya kupokea mafunzo ya dini kutoka kwa babu yake Ustadh Mohamed Ahmad Matano, alijiunga na shule ya msingi ila akaachia masomo katika darasa la nne na kuanza kufanya kazi.

Mashairi yake ya kwanza kabisa kuwahi kuchapishwa ni yale yaliyoko katika kitabu cha Poems from Kenya kilichofyatuliwa mnamo 1966.

Kitabu chake cha pili, ‘Malenga wa Mvita’ kilitokea muda mfupi kabla ya kile cha ‘Irshadi’. Ameandika pia

‘Utenzi wa Mtu ni Utu’ na ‘Taa ya Umalenga’.

Mbali na mashairi aliyokuwa nayo mwenyewe, kuna mengine kadha wa kadha yaliyo kwenye maktaba ya vyuo vikuu kote ulimwenguni. Mengi ya mashairi yake yameimbwa na Bin Ammi katika nyimbo zake za Taarab.

Mbali na ushairi, alikuwa na ujuzi wa kuchora na mweledi wa kutunga nahau za lugha ya Kiarabu.

Watoto wake ni: Mohamed Ahmad Nassir, Amran, Momo, Athman, Sofia, Mahmood, Shihabudin, Nagibu na wengine wa mkewe anayemkalia eda, Mama Fatuma.

Marehemu Ustadh Nassir Juma Bhalo ni mjombawe mtunzi chipukizi wa mashairi aitwaye Awadh Basheikh almaarufu ‘Mwana wa Kanga’.

Picha zote/chris Adungo

wa Nassir Bhalo almaarufu Malenga Baadhi ya diwani za marehemu Ahmad Mvita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.