Kabras waselelea kileleni Quins, Nondies, Mwamba wakipaa katika Kenya Cup

Taifa Leo - - SPOTI - NA GEOFFREY ANENE

KENYA Harlequin, Nondescripts, Mwamba na Homeboyz zimeruka juu nafasi moja kila mmoja kwenye Ligi Kuu ya Raga nchini (Kenya Cup) ambayo ilirejea Januari 12 baada ya likizo ya Krismasi na kushuhudia Kabras Sugar na KCB zikikwamilia nafasi mbili za kwanza. Mabingwa wa mwaka 2016 Kabras walishinda mechi yao ya sita mfululizo kwa alama ya bonasi baada ya kucharaza washiriki wapya Menengai Oilers 41-5 mjini Kakamega. Wanasukari hawa wanaongoza ligi hii ya klabu 12 kwa alama 30. Wako alama tano mbele ya mabingwa watetezi KCB, ambao walipepeta wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi almaarufu Mean Machine 50-3 mtaani Ruaraka. Harlequin na Nondescripts wamepiga hatua moja mbele hadi nambari tatu na nne, mtawalia. Timu ya Harlequin ilijiongezea alama tano muhimu baada ya kulipua Nakuru 36-21 uwanjani RFUEA Grounds jijini Nairobi na kufikisha alama 21. Nondescripts wako alama mbili nyuma. Walizidi maarifa wenyeji wao Impala Saracens waliokuwa wamepigiwa upatu 22-20. Kufuatia kuimarika kwa Harlequin na Nondescripts, Impala imeteremka nafasi mbili hadi nambari tano. Imezoa alama 18, moja mbele ya Mwamba, ambayo ilizima wanyonge Strathmore Leos 47-25 mtaani Madaraka katika mechi ambayo nyota wa timu ya raga ya wachezaji saba kila upande Collins Injera alipachika miguso mitatu. Kutokana na ushindi huu, Mwamba iliimarika kutoka nafasi ya saba hadi nambari sita. Homeboyz inafuata katika nafasi ya saba baada ya kupaa nafasi moja kufuatia ushindi wake wa alama 35-23 dhidi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta almaarufu Blak Blad. “Madeejay” wa Homeboyz wana jumla ya alama 16. Nakuru, ambayo ilishikilia nafasi ya sita kabla ya kulimwa na Harlequin, sasa iko chini nafasi mbili katika nafasi ya nane kwa alama 15. Blak Blad ni ya tisa kwa alama 10 nayo Oilers inafunga 10-bora kwa alama sita. Nafasi mbili za mwisho zinashikiliwa na Machine (alama tano) na Strathmore Leos (tatu). Timu zitakazomaliza katika nafasi mbili za mwisho zitatemwa. Strathmore haijashinda msimu huu.

Picha/maktaba

Ivan Chirabo wa Kabras RFC (aliye na mpira) apigwa breki na mwanaraga Keith Wasike wa Homeboyz katika mchuano wa awali wa Kenya Cup uwanjani Jamhuri Park.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Kenya

© PressReader. All rights reserved.