SIMBA INA MADENI MAWILI YANGA

Bingwa - - MBELE - NA AYOUB HINJO

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, bado wana mtihani mkubwa wa kuhakikisha wanavunja rekodi ya Yanga ya idadi kubwa ya pointi na mabao ya kufunga.

Japo Wekundu wa Msimbazi wameshatwaa ubingwa, wamekuwa wakipigania rekodi ya kumaliza msimu bila kufungwa kama ilivyokuwa msimu wa 2009/10.

Kwa upande wa pointi na mabao, wanapigania kuweka rekodi ya aina yake msimu huu kama ilivyokuwa kwa mabingwa wa Ligi Kuu England, Manchester City.

Man City wameweka rekodi ya kumaliza ligi wakiwa na pointi 100, lakini pia wakiwa wamefunga mabao 106, mengi zaidi kuwahi kufungwa tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo mwaka 1992.

Rekodi hizo walizovunja vijana wa Pep Guardiola msimu huu, ziliwekwa na Chelsea msimu wa 2004/05, walipotwaa ubingwa kwa pointi 95, lakini waliweka rekodi ya kufunga mabao 103 msimu wa 2009/10.

Kwa upande wa Yanga, wanachojivunia hadi sasa ni rekodi yao waliyoweka msimu wa 2015/16 ya kufunga mabao mengi na kuvuna pointi nyingi katika Ligi Kuu Bara.

Ndani ya msimu huo, mabingwa hao wa zamani, walivuna pointi 73 na kufunga mabao 70, kitu ambacho hakikuwahi kufanywa na timu yoyote katika historia ya ligi hiyo.

Hadi sasa, Simba wamefanikiwa kupata pointi 68 na kufunga mabao 61, huku wakiwa na michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar na Majimaji.

Endapo mabingwa hao wakifanikiwa kushinda michezo yote miwili, wataweka rekodi ya kumaliza na pointi 74, zikiwa ni moja zaidi ya zile za Yanga msimu wa 2015/16, huku mtihani mkubwa ukiwa katika rekodi ya mabao.

Wekundu wa Msimbazi hao watahitajika kufunga mabao 10 ndani ya mechi hizo mbili ili kuweka rekodi yao, kitu ambacho kinaonekana kuwa kigumu, kutokana na timu hiyo kushinda kwa idadi ndogo ya mabao hivi karibuni.

Hadi sasa, Simba wameshinda mara 20 na kutoa sare nane, lakini bado watahitajika kushinda michezo miwili ya mwisho ili kufikia rekodi ya ushindi ya Yanga waliyoweka msimu wa 2015/16 kwa kushinda mara 22, lakini waliofungwa mchezo mmoja na kutoa sare saba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.