JPM

AKUBALI KUWAKABIDHI SIMBA KOMBE

Bingwa - - MBELE - ZAITUNI KIBWANA na EZEKIEL TENDWA

Msimbazi roho kwatu, mashabiki watakiwa kuutapisha uwanja kuweka rekodi ya karne Mexime atamba kutia ‘kitumbua mchanga’

IKULU imethibitisha kupokea mwaliko wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtaka Rais Dk. John Magufuli kuikabidhi Simba kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Kagera Sugar, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi.

Simba ilitangazwa kuwa mabingwa wa ligi hiyo Alhamisi iliyopita, baada ya Yanga kufungwa mabao 2-0 na Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya.

Kipigo hicho kilizima ndoto za Yanga kutetea ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo, kwani pointi walizokuwa nazo hadi siku hiyo, yaani 48, zisingeipiku Simba, iliyokuwa na pointi 65, hata kama Wanajangwani hao wangeshinda zote zilizobaki.

Wakiwa wamebakiwa na mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar na Majimaji, Simba kwa sasa wanasaka rekodi ya kumaliza ligi bila kufungwa, kuvuna pointi na mabao mengi zaidi katika historia ya ligi hiyo.

Awali, TFF iliandika barua kwenda Ikulu kumwalika Rais Magufuli kuikabidhi kombe Jumamosi, kitendo kilichoungwa mkono na uongozi wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Akizungumza na BINGWA juzi, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema kuwa, kitendo cha Rais Magufuli kukubali ombi hilo, kitalifanya tukio hilo la Jumamosi kuwa la kihistoria, kwasababu kwa miaka ya hivi karibuni, haijawahi kutokea.

“Tunamuomba Rais Dk. John Magufuli akubali aje ashuhudie mchezo wetu na Kagera ambao tunataka kuendeleza rekodi yetu ya kutofungwa, pia atuwekee rekodi kwa kuwa mara ya mwisho tukio la rais kukabidhi kombe ilikuwa mwaka 1972,” alisema.

Aliwataka mashabiki wa Simba kila kona nchini kufika uwanjani kwa wingi Jumamosi kushuhudia timu yao ikiweka historia kwa kukabidhiwa kombe na kiongozi wa juu wa nchi.

“Ni tukio la kihistoria litafanyika, kama mnavyofahamu, tuna miaka mitano tulikuwa tunausaka ubingwa huu kwa kila staili, ila mwaka huu, Mungu ametuona, hivyo mashabiki wanapaswa kujaa kwa wingi Taifa,” alisisitiza Try Again.

Akithibitisha juu ya mwaliko huo wa Rais Magufuli, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Greyson Msigwa, alisema: “Taarifa imefika, walioleta mwaliko ni TFF kupitia Wizara ya Habari, kikubwa ilikuwa ni kupokea kikombe cha Serengeti Boys, TFF wakafanya ubunifu pale kwamba badala ya kupokea tu, basi ashuhudie na mechi …kwasababu Jumamosi kuna mechi ya Ligi Kuu, basi pia akabidhi na kombe la mshindi wa Ligi Kuu.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, alisema kuwa, tukio hilo litakuwa la kihistoria, kwani mara ya mwisho kufanyika ilikuwa mwaka 1972 pale hayati Rais mstaafu wa awamu ya pili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, alipoikabidhi Yanga ubingwa.

“Aboud Jumbe aliikabidhi Yanga kombe ambapo ni mara ya mwisho rais wa nchi kukabidhi ubingwa, hivyo tuna imani Rais Magufuli ni mwanamichezo, ni baba wa watu wote, anaweza kukubali na kuhudhuria”.

Naye Mwenyekiti wa Matawi ya Simba, Iddy Kajuna, alisema maandalizi ya sherehe hizo za ubingwa yanaendelea na kila tawi limetakiwa kuhakikisha linatoa wanachama wake kufika uwanjani siku hiyo.

“Kila awamu na zama na mambo yake, huu ni mwaka wetu, tuliutafuta ubingwa huu kwa tochi, dua na kila staili, hatimaye tumeupata, hivyo tuna kila sababu ya kufurahi, nawaomba wanachama na mashabiki wote kila sehemu nchini kuhudhuria kwa wingi,” alisema.

Katika hatua nyingine, kuelekea Mkutano Mkuu wa dharura wa Simba unaotarajiwa kufanyika Jumapili ya wiki hii, uongozi wa klabu hiyo umesema taarifa zinazozagaa mitaani kwamba bilionea wao, Mohamed Dewji ‘Mo’ amekataa kupewa zile asilimia 49 si za kweli.

Msemaji wa Wekundu hao wa Msimbazi, Haji Manara, alisema: “Napenda kuwatoa wasiwasi Wanasimba wote kwamba taarifa zinazozagaa mitaani kuwa Mo Dewji amekataa zile asilimia 49 si za kweli, kwani amekubali na kila kitu kimekwenda sawa”.

Kwa upande wake, Mwanasheria ya Klabu hiyo, Evodius Mtawala, alisema kama mambo yote yatakwenda sawa, timu hiyo itaendeshwa kwa mfumo wa Kampuni, jina lake likiwa ‘Simba Sports Club Company Limited’.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.