NI REAL MADRID DHIDI YA DUNIA

Bingwa - - MBELE -

MWAKA 2014 Real Madrid ikiwa chini ya Carlo Anclotti akisaidiwa na Zinedine Zidane, tulitwaa taji la Ligi ya Mabingwa. Mwaka 2016 na 2017 pia chini ya Zinedine Zidane, tulitwaa mataji mawili hayo mfululizo.

Fainali zote tatu tumecheza dhidi ya timu kabambe; Atletico Madrid mara mbili; 2014 na 2016. Juventus mwaka 2017. Uzuri ni kwamba, Zinedine Zidane amevunja mwiko uliozoeleka kuwa bingwa huwa hatetei taji lake.

Zidane tena ameipeleka Madrid katika fainali ya tatu mfululizo akiwa kocha. Anapozungumza na wachezaji anawaambia kuwa wanacheza dhidi ya dunia nzima ambayo haipendi Madrid ishinde.

Kwamba, idadi kubwa ya watu hawataki kuona ikishinda na hivyo wajibu wao ni kushinda tu si kingine. Katika hali hiyo unaposhuhudia makundi ya washabiki wa soka wakilalamika kila ushindi wa Real Madrid unapopatikana.

Utasikia Madrid imebebwa. Chukulia mfano hakuna anayezungumzia ushindi wa mabao 3-0 pale Italia dhidi ya Juventus. Ndiyo maana mwamuzi Michael Oliver analalamikiwa kutoa penalti dakika za nyongeza katika pambano la marudiano pale Santiago Bernabeu, ambapo Juventus walishinda mabao 3-1.

Eti angeacha tu kwakuwa ni ubinadamu. Watu hawa wanasema hivi bila kuangalia sheria za soka. Eti mwamuzi angetumia tu busara muda ule. Vituko hivi, futeni penalti basi!!

Hakuna anayezungumzia ushindi wa mabao 2-1 pale Allianz Arena nchini Ujerumani dhidi ya Bayern Munich. Hakuna anayezungumzia miujiza ya Karim Benzema na nusu fainali. Msimu uliopita aliwachachafya Atletico Madrid katika nusu fainali.

Alipiga bao moja muhimu baada ya kuwalamba chenga mabeki watatu kwenye chaki, kabla ya kutoa pasi kwa Mzee Visu Toni Kroos aliyepiga shuti lililopanguliwa na kumkuta Isco. Mpira ulikuwa ukiambaa ambaa, hakufanya ajizi, akautumbukiza wavuni.

Fainali ya mwaka 2018 mjini Kiev, inalekea katika utamaduni uleule, Real Madrid inapambana na dunia nzima. Nitakwambia sababu.

Real Madrid ndiyo timu ambayo imekuwa ikinunua wachezaji kwa bei za juu. Achana na PSG au Manchester City waliokuja juzi juzi tu. Real Madrid ndiyo klabu inayoongoza kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Madrid imetwaa mara 12 na asa tunalisaka taji la 13.

Madrid ndiyo timu ambayo inawakera wengi kwa sababu ya mafanikio yao. Madrid wametwaa La Liga mara nyingi zaidi kuliko klabu nyingine yoyote Hispania. Madrid ndipo mahali ambapo wachezaji bora wa dunia hujipatia tuzo.

Afredo Di Stefano, Luis Figo, Zinedine Zidane, Michael Owen, Cristiano Ronaldo kwa kuwataja wachache. Madrid ni sehemu ambayo wachezaji wengi wanatamani kupata nafasi ya kucheza. Mtihani wa kuikataa Rea Madrid ni mgumu sana kwa wachezaji.

Sasa hivi mtihani huu unaelekea kwa Eden HJazard ambaye klabu yake itacheza mashindano ya Europa League msimu ujao. Hazard alishazoea kucheza Ligi ya Mabingwa, itakuwaje sasa hivi akubali kwenda Europa League?

Sehemu pekee ambayo itampatia furaha na kuota tuzo ya mchezaji bora wa dunia ni Real Madrid. Sehemu pekee ambayo mchezaji anaweza kufanikiwa na kutimiza ndoto zake ni Real Madrid.

Ni klabu hii ndiyo inatoa jasho wengi wakiamini kila hatua ya ligi ya mabingwa eti inabebwa. Kulaumiwa huku ni matunda ya mafanikio yao. Wengi wanalaumu kila hatua. Hakuna timu kongwe isiyocheza na Real Madrid miaka ya karibuni.

Kuanzia Serie A, EPL, Bundesliga, Ligue 1 hadi klabu bingwa dunia. Madrid wametamba kila kona ya dunia kitu ambacho hakuna klabu iliyofanikiwa kama hii.

Ndiyo maana kila linapokuja suala la mashindano ya Ligi ya Mabingwa idadi kubwa ya mashabiki wanataka Madrid itolewe. Wamejaribu kwa kubeti, wameshindwa. Wamewakejeli wachezaji, bado wameshindwa. Wanawalaumu waamuzi, lengo likiwa waitoe Madrid mashindanoni, bado nako wanaelekea kushindwa.

Kwahiyo katika mchezo wa fainali wa mwaka huu, Real Madrid itaingia uwanjani kama kawaida ikielewa kuwa inapambana na dunia nzima. Idadi kubwa ya mashabiki wanataka Liverpool itwae taji.

Wanasimulia uzuri na umahiri wao. Wanaisifu Liverpool kwa kufika fainali baada ya kutembeza vichapo kwa FC Porto kwenye mtoano, Manchester City kwenye robo fainali na AS Roma kwenye nusu fainali.

Wamesahau Real Madrid imewatoa wakali wa PSG kwenye mtoano. Wakaichabanga Juventus kwenye robo fainali, kisha kuivuruga Bayern Munich kwenye nusu fainali.

Wenye kiu ya kuona Madrid inafungwa hawaangalii uwiano huu wa timu walizokutana nazo. Wanachojali ni umahiri wa washambuliaji wa Liverpool, Sadio Mane, Roberto Firmino na Mohammed Salah.

Wanamdharau Karim Benzema wetu. Nasi tunasema, karibuni kwenye ulimwengu wa mapambano. Ulimwengu wa kutifuana kweli dhidi ya timu inayokabiliana na dunia nzima na ikaishinda mara 12. Zimebaki siku chache kabla ya kutia mguu mjini Kiev, nchini Ukraine. Tutaonana huko.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.