YANGA SIKIO LA KUFA

Yashindwa kuichapa Rayon nyumbani

Bingwa - - MBELE - NA SALMA MPELI

MIAMBA ya Tanzania, Yanga jana wameendelea kufanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa safari hii wakiwa kama sikio la kufa kwa kushindwa kuutumia uwanja wa nyumbani wa Taifa na kutoka sare ya bao 0-0 dhidi ya Rayon Sports katika mchezo wa makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Huo ni mchezo wa pili wa Kundi D kwa Yanga, baada ya ule wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita mjini Algiers nchini Algeria na kuchapwa mabao 4-0 dhidi ya USM Alger, ambapo walimakosa nahodha Kelvin Yondani na wachezaji wengine kama mshambuliaji Ibrahim Ajib, ambaye hata jana hakuwapo.

Katika mchezo huo uliochezwa usiku, ulianza kwa kasi ya kawaida na timu zote mbili zikishindwa kucheza soka la kuvutia, huku Rayon ambao walitoka sare bao 1-1 dhidi ya Gor Mahia kwenye mchezo wao wa kwanza walionyesha kujiamini pamoja na kuwapo katika ugenini.

Katika dakika ya 28, nahodha wa Yanga, Yondani alifanya kazi kubwa baada ya kuokoa bao la wazi kwa kubinuka ‘tiki taka’ akiucheza mpira uliopigwa na mshambuliaji wa Rayon, Ismaila Diarra.

Dakika ya 32, Diara alikwamisha mpira wavuni lakini wakati mshika kibendera Ivanildo Meirelles alishainua kuonyesha kwamba mfungaji alikwishaotea kabla ya kutumbukiza mpira huo wavuni.

Nyota wa Mali, Diarra aliendelea kulisakama lango la Yanga, lakini alikosa umakini na kupoteza nafasi kadhaa ambazo zingeweza kuwafanya wageni hao kuondoka na ushindi kwenye uwanja huo wa Taifa.

Hadi mwamuzi Helder Martins Rodrigues De Carvalho anapuliza kipyenga cha mapumziko timu hizo zilikuwa hazijafungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Rayon kufanya shambulizi langoni kwa Yanga dakika ya 54, lakini vijana hao wanaonolewa na makocha Noel Mwandila na Shedrack Nsajigwa waliokoa hatari hiyo.

Dakika tatu baadaye Rayon walifanya mabadiliko kwa kumtoa Manishimwe Djabel na nafasi yake ilichukuliwa na Muhire Kelvin, kabla ya dakika chache Hassan Kessy na Yondani kuonyeshwa kadi za njano.

Diara aliendelea kuikosesha Rayon ushindi baada ya kupata nafasi nzuri na kuishindwa kuitumia dakika ya 63 kwa kupiga shuti lililopaa juu, dakika moja baadaye Yanga walimpumzisha Thaban Kamusoko na nafasi yake kuchukuliwa na Raphael Daud, ambaye dakika tano tangu kuingia uwanjani alimtengenezea Obrey Chirwa nafasi nzuri ya bao na kugongesha mwamba.

Rayon walifanya mabadiliko dakika ya 73 kwa kumtoa Diarra na kumwingiza Mbondi Christ, ambaye aliongeza nguvu kwenye kikosi hicho na kutingisha nyavu dakika ya 82, lakini alikuwa amezidi na bao lake lilikataliwa.

Yanga walifanya mabadiliko dakika ya 84 na 88 kwa kumpumzisha Chirwa na kuingia Amis Tambwe kisha Geofrey Mwashiuya kumpisha Emmanuel Martin dakika ya 88, lakini mabadiliko hayo hayakusaidia kitu na mchezo huo kumalizika kwa sare na kuifanya Yanga kuambulia pointi moja katika mechi zake mbili.

Kikosi cha Yanga kilikuwa na mlinda mlango Youthe Rostand, Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vicent, Yondani, Kamusoko/ Daud, Pius Buswita, Yusufu Mhilu, Chirwa/Tambwe, Juma Mahadhi na Mwashiuya/Martin.

Nao Rayon Sports waliwakilisha na Eric Ndayishimiye, Gabriel Mugabo, Eric Rutanga, Thierry Manzi, Mutsinzi Ange, Shabani Hussein, Sadam Nyandwi, Diarra/Mbondi, Pierre Kwizera, Mugisha Francois na Manishimwe Djabel.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.