Rayon Sports yawafufua wakongwe Yanga

Bingwa - - MBELE - NA HUSSEIN OMAR

KANDANDA lililoonyeshwa na Yanga dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi, limewaibua wakongwe wa timu hiyo na kuwaweka kitimoto wachezaji kuwataka waache utoto na kuipigania timu kwa nguvu zao zote.

Tukio hilo lilitokea baada ya mchezo huo wa pili wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hizo zilitoka suluhu.

Hata hivyo, Yanga walikuwa na nafasi kubwa ya kushinda, kwani wapinzani wao hao walionekana kuwa wa kawaida, lakini Wanajangwani hao wakashindwa kuutumia vema udhaifu wao, ikiwamo faida ya kucheza uwanja wa nyumbani.

Miongoni mwa wakongwe wa Yanga waliowavaa wachezaji wa timu hiyo, ni nahodha wa zamani wa timu hiyo, Ali Mayay, aliyeongozana na Charles Mkwasa, ambao walizungumza na vijana wao hadi usiku wakiwa katika vyumba vya kubadilishia nguo uwanjani hapo.

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam jana, Mayay alisema jambo kubwa lililosababisha kuwaweka kitimoto wachezaji hao ni kutoridhishwa na kiwango walichokionyesha katika mchezo wa juzi na mingine iliyopita.

“Nililazimika kuzungumza na wachezaji, kama unavyofahamu Yanga ni timu yangu, inapofanya vibaya najisikia huzuni sana, jambo kubwa ambalo nimeongea nao nimewasisitiza mpira ndio kazi yao, hivyo wajitahidi kupambana na kupata matokeo,” alisema Mayay.

Alisema soka ni kazi yao, hivyo changamoto wanazokutana nazo hawatakiwi kurudi nyuma, ili waweze kwenda mbele wanatakiwa kufunga mkanda kama walivyofanya akina Simon Msuva na Mbwana Samatta wakati wakicheza soka hapa nchini.

“Ile ni kazi yao, nimewataka wasahau matatizo, japo wanakosa uzoefu katika mashindano ya kimataifa, lakini wanatakiwa kupambana kupiga hatua zaidi mbele kama walivyofanya Msuva na Samatta, wasiangalie Yanga tu,” alisisitiza Mayay.

Mayay alisema kuna upungufu mkubwa katika kikosi cha Yanga katika suala zima la nidhamu ya kimchezo, kwani wachezaji wake wanafanya makosa mengi ambayo yanastahili kufanywa na timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Nne na si Ligi Kuu.

“Kuna mapungufu makubwa sana katika kikosi cha Yanga, ikiwamo kukosa maarifa kwa wachezaji, nidhamu ya kuanza mpira ipo chini… kuna vitu vingi sana vya kiufundi vinatakiwa kufanyiwa marekebisho na benchi la ufundi,” alisisitiza Mayay.

Kiungo huyo aliyewahi pia kuichezea timu ya Taifa, Taifa Stars, kwa sasa akiwa ni mchambuzi mahiri wa soka, aliongeza: “Niliwaambia hakuna sababu ya kukata tamaa, uwezo wanao, kama wakiamua bado kuna mechi tatu zimebaki ambazo wanaweza kufanya maajabu.”

Kabla ya Mayay kuzungumza na wachezaji hao, aliyekuwa beki mahiri wa kushoto wa Yanga, Kenneth Mkapa, aliyekuwapo uwanjani hapo juzi, muda wote alionekana kusikitishwa na jinsi timu yake hiyo ilivyokuwa ikicheza dhidi ya Rayon.

Kuna wakati alikuwa akiinamisha kichwa chini pale mchezaji wa Yanga alipoboronga kuonyesha jinsi alivyokuwa akiumizwa na timu yake hiyo aliyoitumikia kwa mafanikio na nidhamu ya hali ya juu.

Katika michuano hiyo, Yanga ipo Kundi D pamoja na USM Alger ya Algeria, Rayon na Gor Mahia ya Kenya, ambapo Wanajangwani hao tayari wamepoteza mechi mbili, ikiwamo dhidi ya Waalgeria walipolala mabao 4-0 ugenini.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.