SIMBA YAZIDI KUNOGA

PIERRE ‘AJIONGEZEA’ MKATABA, AAHIDI KULETA VIFAA VYA NGUVU

Bingwa - - MBELE - NA WAANDISHI WETU Habari hii imeandaliwa na SAADA SALIM, ZAITUNI KIBWANA NA MWAMVITA MTANDA

SIKU moja kabla ya Simba kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, mambo yameonekana kuzidi kunoga ndani ya Wekundu wa Msimbazi hao, baada ya Kocha Mkuu wao, Pierre Lechantre, kuanza kuanika mikakati yake ya kuendeleza makali yao msimu ujao.

Simba wametwaa ubingwa huo msimu huu baada ya kuusotea kwa misimu mitano bila mafanikio, wakiwakodolea macho watani wao wa jadi, Yanga, wakibeba ‘mwali’ mara nne na Azam mara moja.

Cha kuvutia zaidi, Simba wametangaza ubingwa wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja, zaidi ya kushinda na kupata sare, rekodi ambayo waliwahi kuiweka msimu wa 2009/10 chini ya Kocha Mkuu, Mzambia Patrick Phiri.

Na ikiwa ni saa chache kabla ya Rais Dk. John Magufuli kuwakabidhi kombe lao kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar, Pierre ameonekana kuzidi kupagawa akitamani kuendelea kubaki Msimbazi.

Ikumbukwe kuwa, ndani ya Simba kuna watu ambao wameonekana kutomtaka Pierre, wakipendekeza msaidizi wake, Masoud Djuma, aachiwe timu badala ya Mfaransa huyo.

Kuna habari kuwa, Pierre na Djuma hawana uelewano, hali iliyoufanya uongozi wao kuwaweka chini kila mmoja kivyake ili kumaliza tofauti zao, lakini hilo limeonekana kutozaa matunda.

Mwisho wa siku, wapo wanaotamani kuona Pierre akiondoka na timu kubaki kwa Djuma, huku mfanyabiashara maarufu nchini ambaye ni mwanachama wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, akipanga kumwongezea mkataba Mfaransa huyo.

Pierre wakati anatua Simba mapema mwaka huu, aliingia mkataba wa miezi sita tu na Simba, ambao unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.

Wakati hayo yakiendelea, Pierre ameonekana ‘kutokuwa na habari’ na badala yake akiweka mkakati kabambe wa kuzidi kukiboresha kikosi chake, akiamini ‘bado yupo yupo’ Msimbazi.

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam jana, Pierre alisema kuwa, anahitaji kuboresha kikosi chake kwaajili ya msimu ujao kwa kusajili wachezaji wenye viwango bora zaidi ya nyota waliopo katika kikosi chake.

Alisema kuwa, kikosi hicho kinahitaji marekebisho kidogo kwenye safu ya ushambuliaji, kiungo mkabaji na kuimarisha ulinzi.

“Simba kama inataka mafanikio, inapaswa kufanya marekebisho kwenye maeneo hayo, wanatakiwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu, kwa kuwa timu itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Pierre.

Alisema kwa upande wake, atatafuta wachezaji wawili au zaidi wenye ubora wa hali ya juu kutoka nchini kwao Ufaransa wakati atakapokuwa huko kwa mapumziko.

Alisisitiza: “Kikosi kipo imara, nafurahi tangu nimeanza kukinoa, hawajawahi kuniangusha.

“Uzoefu wangu ni mkubwa, sichukui mchezaji kwa sababu ana jina, naangalia yule ambaye ana uwezo wa kucheza mpira katika kiwango cha juu, ninaamini nikifanikiwa kuwaleta hawataniangusha.”

Hadi sasa wakiwa wameshatwaa ubingwa, tayari wamefikisha pointi pointi 68 na mabao 61, huku wakiwa wamebakiwa na michezo miwili dhidi ya Kagera Sugar na Majimaji.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.