Shahidi: Malinzi alibadili watia saini benki

Bingwa - - HABARI - NA KULWA MZEE

KESI ya vigogo wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake imeanza kusikilizwa na Meneja wa Benki ya Stanbic Tawi la Centre, Kinondoni, Abelhem Msiagi, ameeleza jinsi washtakiwa walivyofanya mabadiliko ya watia saini kwenye akaunti sita za shirikisho hilo.

Meneja huyo, ambaye ni shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro.

Shahidi alidai TFF ni miongoni mwa wateja wao katika Benki hiyo na analitambua faili la mteja wao huyo kwa kuwa walikuwa na akaunti sita, aliomba faili lipokelewe kama kielelezo na mahakama ilikubali kulipokea.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa Katibu Mkuu Celestine Mwesigwa, Mhasibu Nsiande Mwanga, karani Flora Rauya na Miriam Zayumba, ambao wote wanakabiliwa na mashtaka 30.

Shahidi alidai waliokuwa watia saini katika akaunti hizo ni Jamal Malinzi, Wallace Karia, Mwesigwa Celestine na Nsiande Mwanga.

Shahidi alipotakiwa kumwonesha Malinzi ni yupi mahakamani hapo, alitoka kwenye kizimba na kwenda kwenye kizimba walipokuwa washtakiwa na kumpa mkono Malinzi huku akimpigapiga begani kwa kumsalimia.

Alimsalimia Mwesigwa, lakini alishindwa kumuona Karia, hivyo aliieleza mahakama kwamba hamuoni.

Alidai watia saini Malinzi na Mwesigwa walifika benki wakiongozana na Nsiande, kisha walimkumbulisha kama ndiye atakuwa mtia saini katika akaunti zote za TFF badala ya Edgar Masoud.

Alidai mabadiliko yalifanyika Septemba mosi, 2016, lakini muhtasari wa mabadiliko uliwasilishwa Juni 5, 2016.

Alidai mabadiliko hayo yanadaiwa kufanyika katika kikao kilichokuwa na wajumbe 20 na waliotia saini walikuwa Malinzi na Mwesigwa na baada ya kukamilika utaratibu wa benki, shahidi aliridhia mabadiliko hayo kwamba yako sahihi.

Alidai nyaraka hiyo ilikabidhiwa kwa Ofisa wa benki na Mwesigwa na kwamba muhtasari huo ulikuwa na shabaha ya kufanya mabadiliko ya kumtoa mtia saini Edgar Masoud na kumweka Nsiande.

Akielezea utaratibu, alidai kwa upande wa taasisi kufungua akaunti wanaleta makubaliano ya bodi yanayoambatana na Katiba, hati ya usajili, muhtasari wa kikao ambacho walikaa na kuamua benki ya Stanbic iwe inatumiwa na taasisi, taarifa ya walioteuliwa kuendesha akaunti hiyo na utambulisho wao.

Shahidi huyo alidai wakikamilisha nyaraka hizo wanapatiwa fomu ya kufungua akaunti na utaratibu wote ukikamilika wanatengeneza faili ambalo litakuwa na taarifa zote za mteja, zikiwamo za wenye dhamana ya kuendesha akaunti hiyo ambalo litaendelea kuwekwa taarifa.

Meneja huyo wa Benki alidai iwapo taasisi inataka kufanya mabadiliko ya ama kuongeza au kupunguza waendesha akaunti hiyo, lazima wapeleke muhtasari wa kikao kilichofikia uamuzi huo.

Alidai katika kufanya mabadiliko ya mtia saini, lazima watia saini wa awali wafike benki na mtia saini mpya.

Akihojiwa na wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko, Shahidi alidai hakushuhudia Mwesigwa akikabidhi nyaraka ya mabadiliko na aliwaona Malinzi na Mwesigwa benki walipokwenda kumpeleka mtia saini mpya, Nsiande.

Shahidi alidai nyaraka ya mabadiliko ya mtia saini ya Juni 5, 2016 ilikuwa sahihi kwa kuwa ilikidhi vigezo vyote vya kibenki.

Katika hati ya mashtaka, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha wa Dola za Marekani 173,335 na Sh 43,100,000.

Mwesigwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, na utakatishaji wa fedha, huku Nsiande akikabiliwa na mashtaka mawili ya utakatishaji wa fedha.

Mshtakiwa Miriam yuko kwenye mashtaka tisa ya kughushi na Flora anakabiliwa na shtaka la kughushi.

Malinzi, Nsiande na Mwesigwa wapo mahabusu kwa kuwa mashtaka ya utakatishaji fedha hayana dhamana.

Washtakiwa Miriam na Flora wako nje kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu ijayo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.