RT KUWAJADILI 'WATOVU WA NIDHAMU'

Bingwa - - HABARI -

KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), linatarajia kukutana mwanzoni mwa Juni mwaka huu kwa ajili ya kuwajadili wanariadha watatu wanaodaiwa kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.

Wanariadha hao ni Sarah Ramadhan, Failuna Abdi na Agustino Sulle ambao wanadaiwa kufanya vitendo tofauti vya utovu wa nidhamu wakati wa maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyika nchini Australia kuanzia Aprili 4 hadi 15, mwaka huu.

Wanariadha hao wanadaiwa kuonyesha vitendo vya ujeuri kwa kuwadharau makocha, matroni na kugoma kulala kambini na kwenda kusikojulikana wakati wa kambi.

Lakini pia baada ya kurejea nchini wakiwa katika uwanja wa ndege, bado waligoma kurejea katika kambi ya Kibaha mbele ya viongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC).

Akizungumza na BINGWA jana kutoka mkoani Arusha, Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday, alisema tayari kamati ya utendaji imeshapokea ripoti ya kocha mkuu wa timu ya riadha iliyoshiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola, Zacharie Barie.

Alisema kwa pamoja watakaa na Kamati ya Ufundi ya RT na kuyafanyia kazi yale yaliyozungumzwa.

“Kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika katiba ya RT, makosa ya utovu wa nidhamu yaliyotajwa adhabu zake zinaweza kuwa ni kufungiwa au kupewa onyo.

“Kwa mujibu wa maelezo ya kocha, vitendo walivyofanya wanariadha hawa si vizuri, hivyo hatutaweza kuvifumbia macho kwani tunahitaji kila mwanariadha kwa nafasi yake awe na nidhamu itakayoweza kumbeba katika mbio,” alisema Gidabuday.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.