Makorora FC yang’ara Banda Cup

Bingwa - - HABARI - NA OSCAR ASSENGA, TANGA

TIMU ya soka ya Makorora FC, juzi ilianza vema mashindano ya Banda Cup baada ya kuibamiza Jiji FC mabao 3-1, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja Mkwakwani, Tanga.

Timu zote zilianza mchezo kwa kasi na kushambuliana kwa zamu, lakini Makorora ndio waliokuwa wa kwanza kufunga bao katika dakika ya kwanza lililofungwa na Ally Shiboli.

Licha ya kupata bao hilo, Makorora waliendeleza mashambulizi langoni kwa Jiji na kufanikiwa kuongeza bao la pili dakika ya 12 kupitia kwa Moud Hassan.

Hata hivyo, mabao hayo yaliwachanganya Jiji ambao walilazimika kujipanga upya na kulisakama lango la wapinzani wao, lakini juhudi zao hazikuzaa matunda.

Kasi hiyo iliwazindua Makorora na kufanya shambulizi kali langoni mwa Jiji ambalo liliwawezesha kupata bao la tatu katika dakika ya 42 kupitia kwa Mussa Kidole.

Kipindi cha pili Jiji walizinduka baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wake na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 62 lililofungwa na Mansour Ramadhani.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.