NANDY AZINDUA MAFUTA YA KUJIPAKA NA SABUNI

Bingwa - - IJUMAA SPESHO - NA MWANDISHI WETU

MSANII wa Bongo Fleva nchini, Faustina Charles ‘Nandy’, leo amezindua bidhaa zake mbili alizoingia ubia na Kampuni ya Grace Natural Production. Nandy alizindua bidhaa hizo za sabuni ya kuogea na mafuta ya kujipaka katika Fukwe za Escape One, zilizopo eneo la Mikocheni. Akizungumza katika uzinduzi huo, Nandy alisema amekuwa akisumbuliwa na watu mbalimbali juu ya mafuta anayotumia kutokana na mwonekano wake asilia, jambo lililomfanya apate wazo la kuwa na mafuta na sabuni yake. “Nimekuwa nikisumbuliwa kwa muda mrefu na watu juu ya mafuta ninayotumia, lakini sikuweza kuwaambia ukweli, kwani ningetaja kama natumia bidhaa za Kampuni ya Grace Production na mimi ni msanii ningekuwa nimefanya tangazo, lakini hali hiyo ilinifanya nipate wazo la kwanini nisiingie ubia na kampuni hiyo,” anasema Nandy. Nandy aliongeza kuwa, baada ya kuzungumza na wasimamizi wake, waliamua kuonana na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Dk. Elizabeth Kilili. “Tulichukua muda na kukaa vikao vingi hadi kuingia ubia na kampuni hiyo,” alisema Nandy, ingawa hawakuweka wazi asilimia ya ubia huo na utakuwa wa muda gani. Naye Dk. Elizabeth alisema wamefurahishwa kuingia ubia na Nandy, wakiamini itaisaidia kampuni yao katika kufanya biashara. “Nandy ni msanii mzuri na mwenye uwezo wa kuimba, hivyo ubora wake wa uimbaji utasaidia kwa kiasi kikubwa kuuza bidhaa hizo,” alisema Dk. Elizabeth.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.