Salamba kurekebisha hali ya hewa Azam FC?

IKIWA zimebaki mechi mbili kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, kikosi cha Azam kimeanza harakati za kusaka wachezaji kwa usajili wa msimu ujao.

Bingwa - - MAKALA - NA WINFRIDA MTOI

Katika mchakato huo, tayari uongozi wa timu hiyo umetua Lipuli FC wakitaka saini ya mshambuliaji wa kikosi hicho aliyeonyesha uwezo mkubwa msimu huu, Adam Salamba.

Salamba amekuwa akiwaniwa na timu kubwa mbili za jijini Dar es Salaam, ikiwamo Yanga kutokana na kuwashawishi viongozi wa klabu hizo.

Ukiangalia hali ya Azam msimu huu, ni wazi wanahitaji marekebisho makubwa kwenye kikosi chao. Je, Salamba anaweza kuwa mchezaji sahihi wa kukata kiu ya Wanalambalamba hao?

Ikumbukwe kuwa, licha ya Azam kufanya uwekezaji mkubwa kupitia mmiliki wake, Said Salim Bakhresa, huku wakipata udhamini mnono wa Benki ya NMB pamoja na bidhaa za kampuni inayomilikiwa na wawekezaji hao, bado haijafikia malengo yaliyotarajiwa na wengi.

Pia Azam ni timu iliyowahi kunolewa na makocha tofauti wa kigeni, lakini haijafanya mambo makubwa na kuendelea kuwa sawa na klabu nyingine zisizokuwa na uwekezaji kama wao.

Msimu huu umekuwa mbaya zaidi kwa kikosi hicho, hasa baada ya mabadiliko ya sera ya uendeshaji yaliyofanyika yakilenga kubana matumizi, hivyo kusababisha nyota wake kutimkia Simba. Wachezaji hao waliokwenda Simba ni John Bocco, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na kipa namba moja wa timu ya Taifa, Aishi Manula na nyota wengine wa kigeni na hivyo kuathiri kikosi hicho kwa kiasi kikubwa.

Baada ya kuondoka nyota hao, Azam iliwasajili wachezaji wazawa kama Mbaraka Yusuf, Waziri Junior, Salmin Hozza, kipa Benedict Haule na Waghana Bernard Arthur, Razack Abarola.

Hata hivyo, bado kikosi hicho kimeendelea kusuasua na leo hii wanahitaji kumsajili Salamba, wakiamini anaweza kubadilisha hali iliyopo kwenye timu hiyo ambayo haiwaridhishi mashabiki wake.

Salamba ni mchezaji mzuri na ndiyo sababu amekuwa akifukuziwa na timu nyingi, lakini cha kujiuliza ni kwamba anaweza kubadilisha hali ya hewa ya Azam?

Ikumbukwe kuwa mapema mwaka huu, NMB iliongeza udhamini wake kwa klabu hiyo kutokana na kuvutiwa na mwenendo wake, wakiamini sapoti yao ingewapandisha mzuka wachezaji, benchi la ufundi na viongozi na hivyo kufanya vizuri zaidi msimu huu.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa udhamini huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo bora iliyoshamiri mafanikio iliyopata katika kipindi cha miaka 10 ya uwapo wao, ikiwamo minne ya kuidhamini.

“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa kutwaa taji la Mapinduzi Cup 2018 kwa mara ya pili mfululizo, tunaongeza mkataba wa udhamini na Azam FC ambao naamini utaongeza sana maendeleo yao ya sasa ya kukuza vipaji katika klabu yao na kuhakikisha wanakuwa kwenye nafasi yao kama klabu kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Kwa miaka minne sasa, tumekuwa wadhamini wakuu wa Azam FC na tumeona mafanikio makubwa kwenye klabu na tunayo furaha kuendelea kushirikiana na Azam FC, kupitia mkataba huu, Benki ya NMB tutaendelea kama wadhamini wakuu wa klabu,” alisema.

Bussemaker alisema kupitia vipengele vya mkataba huo, pande zote mbili wamekubaliana kukuza na kuendeleza soka kwa faida ya pamoja (Azam FC na NMB) na kutumia soka kama gari la kuimarisha mahusiano yao pamoja na ushirikiano.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdul Mohamed Mohamed, aliishukuru NMB kwa kuendelea kuwadhamini na kuahidi kuendeleza moto wao wa kutwaa mataji chini ya udhamini wa benki hiyo baada ya kuanza na Mapinduzi Cup msimu huu.

“Tutalipa fadhila za kuaminiwa huku kwa kutwaa taji la VPL, kwa sababu Azam FC inaamini katika mafanikio kama kichocheo cha kuvutia wadhamini wengine klabuni Azam Complex, Chamazi, moto wetu wa kutwaa mataji utaendelea kwa kutwaa taji la ligi msimu huu ambalo nalo tutalileta hapa kwa mdhamini wetu mwishoni mwa msimu huu,” anasema.

Mkataba huo uliendeleza ndoa ya misimu minne tangu NMB ilipoanza kuidhamini Azam FC mwaka 2014 ilipoibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambapo hii ni mara ya tatu wanarefusha ushirikiano huo na mabingwa hao mara mbili mfululizo wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar.

Domayo

Salamba

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.