KABLA YA MIMBA BINTI TAFAKARI HILI SUALA

Bingwa - - MALAVIDAVI - NA RAMADHANI MASENGA ramadhanimasenga@yahoo.com 0719 053327

MABINTI wengi wenye umri kati ya miaka 16 mpaka 25, wamepoteza matumaini ya maisha kwa sababu ya mapenzi.

Wengi wao utawakuta na vichanga migongoni, sura zikiwa zimekata tamaa wakiwa mitaani wakibangaiza pesa kwa ajili ya matunzo ya watoto wao, baada ya baba wa watoto husika kuwakana na mzigo kubaki kwao pekee.

Ndani ya nafsi za hawa mabinti kuna maumivu ya aina mbili. Yale ya kukataliwa na wanaume waliowaamini na kuwa na matumaini nao, na yale ya kuwa na majukumu bila ya kujiandaa vya kutosha.

Mateso na dhiki zote zinazowaandama chanzo chake ni mahali padogo sana kimtazamo, ila ni kubwa kimaana. Ni pale walipoaamua kuwaamini sana wanaume husika na kujisahau na kuona kama wako ndani ya ndoa na kujikuta wakijiona inafaa wao kuitwa mama. Matokeo yake sasa ni majuto makubwa sana kwao.

Leo wanaitwa mama katika mazingira magumu bila msaada na wale walioshiriki nao katika kutengeneza huo umama. Umama ambao unakosa faraja na raha wanazostahili na wanazopata wamama wengine wenye kuishi na baba za watoto wao.

Wao wakati wakikonda kwa maumivu na dhiki za dunia, wenzao wanatafuta wengine wa kuwapa dhiki za namna hiyo. Inauma sana.

Labda niseme kitu kimoja. Najua mabinti wengi mnaishi katika changamoto nyingi kiasi cha kuamini ni ngumu kuishi bila kuwa na mahusiano ya kingono.

Wengi mnaona hiyo ni ngumu kwa kuona mnapitwa na baadhi ya mambo ama kuna mahitaji fulani mtayakosa. Siyo mada yangu leo.

Ila ninachoweza kusema hata baada ya kuwa katika mahusiano bado una nafasi ya kufanya usipate mimba. Mimba si suala dogo.

Mimba huleta amani na furaja baina ya watu wawili wenye mahusiano halali yenye uhakika wa safari. Kwako binti, mimba ya nje ya ndoa bado ni utata.

Wavulana wengi mnaokutana nao wao wenyewe hawana jeuri ya kujihudumia, vipi wewe na mimba yako? Kuwa makini sana na maamuzi yako.

Wengine wana uwezo hata wa kuhudumia familia yenye watu 20, ila hawako tayari kwa hilo. Sasa vipi unajiachia upate mimba ambayo baadaye utapata mtoto utakayemlea katika mazingira ya dhiki na shida? Acha maisha ya kwenye filamu na mitandaoni. Ishi kiuhalisia kuepuka kudanganywa na yeyote.

Unaweza kushindwa kujizuia kumpenda Fulani, ila una uwezo wa kujizuia kupata mimba. Anayetaka akupe mimba kabla ya ndoa mtazame vizuri. Kama kakwambia ana uwezo wa kuihudumia mimba na wewe, kwanini sasa asikuoe ili mtoto awakute tayari ndani ya ndoa?

Wale mabinti wanaoonekana mtaani wakiteseka kwa ajili ya lishe ya watoto wao, na wao walikuwa wakifurahia mapenzi kabla. Usione wakiwa wamechakaa ukadhani yale ndiyo yalikuwa maisha yao toka mwanzo, hapana.

Walikuwa wakila vizuri, tena usikute kila mara wao na wapenzi wao walikuwa wakikutana maeneo ya starehe na chakula chao siku zote hakikuwa ugali wala makande. Ni chipsi kuku na vinywaji murua, ila leo kula tu inakuwa mtihani kwao.

Zamani walikuwa ‘wakibeep’ wenzao wanapiga, ila leo hata wakipiga simu zao hazipokelewi. Kuweni makini sana dada zangu.

Watoto si ‘fashion’ wala si jambo la kukupatia sifa. Utapendeza na kupongezwa ikiwa utapata mtoto ukiwa katika ndoa yako. Tofauti na hapo fikiria zaidi.

Maisha hayo unayoishi leo, kesho utayaona kwa wenzako kama ukiwa na pupa katika suala la mapenzi. Kila kitu huwa na taratibu zake.

Acha kupelekeshwa na maisha ya kuigiza na kutaka mtoto haraka. Jifikirie wewe, maisha yako ya baadaye na huyo anayetaka kukupa mimba.

Anaweza kuwa na kipato kikubwa na bado asiwe na mipango ya kweli na wewe, hivyo kukimbilia kubeba mimba bila ndoa ni kamari.

Heshimu utu wako, epuka kucheza kamari na maisha yako. Kwa kila hali hakikisha huyo anayesema ana shida ya mtoto akuoe kwanza ndiyo ampate. Ukiamua kuzaa tu hautateseka peke yako, bali hata huyo kiumbe unayemleta duniani.

Mtoto ili akue vyema anahitaji malezi ya baba na mama. Acha kuwa na papara, mtoto anahitaji maandalizi na mshikamano wa kweli kutoka kwa baba na mama. Akikukacha utalia peke yako na utamtesa mtoto wako.

Kumbuka leo anakwambia maneno mazuri na matamu ni kwa sababu ni yeye mwenye shida kubwa kwako. Tambua ukipata mimba wewe ndio utakuwa na shida zaidi na yeye. Sasa hapo ili suala hili liende vizuri, inakupasa umfunge katika kiapo cha ndoa.

Wale wakina dada waliojazana katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutaka malezi ya watoto si kwamba wana bahati mbaya sana katika maisha.

Kilichowaponza ni kutoa hukumu ya haraka kwa mambo wasiyoyajua kwa kina.

Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu mbobezi katika masuala ya mahusiano na maisha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.