Mwalusako alazwa Muhimbili

Bingwa - - HABARI / TANGAZO - NA HUSSEIN OMAR

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kupooza.

Akizungumza na BINGWA jana, mjumbe wa Kamati ya Utendaji

ya Yanga, Tobias Lingarangala, alisema Mwalusako alifikishwa hospitalini hapo juzi na kulazwa katika wodi ya Sewahaji namba moja kwa ajili ya matibabu.

“Ni kweli Mwalusako amepatwa na maradhi ya kupooza na bahati nzuri Mungu amesaidia amewahi kupata matibabu kwahiyo hali halisi ndiyo hiyo,’’ alisema Lingarangala.

Lingarangala alisema kutokana na huduma za matibu ya katibu huyo wa zamani wa Yanga kuwa juu, amewaomba wadau, wanachama na mashabiki wa timu hiyo kumchangia.

“Gharama za matibabu ni kubwa sana, hivyo tunaomba kwa yeyote atakayeguswa na suala hili afikishe mchango wake kwa Emmanuel Mpangala na bila shaka utafika mahali husika,’’ alisema Lingarangala.

Lingarangala amewaomba Wanayanga kushikamana katika kipindi hiki ambacho wanamuuguza katibu huyo wa zamani, kwani katika kipindi chake cha uongozi aliifanyia mengi mema klabu hiyo.

Kabla ya kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Mwalusako alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioisaidia timu hiyo kufanya vizuri miaka ya nyuma kwa uwezo wake wa kumudu kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.

Nyota huyu alianza kujulikana katika ulimwengu wa soka mwaka 1979, wakati huo akiichezea klabu iitwayo Waziri Mkuu ya Dodoma, akicheza kama beki wa kati.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.