POGBA AUPOTEZEA UNAHODHA MAN UTD

aupotezea unahodha Man Utd

Bingwa - - MBELE - PARIS, Ufaransa

KIUNGO wa timu ya Manchester United, Paul Pogba, amesisitiza kwamba, hana haja ya kuvaa kitambaa cha unahodha ndio aonekane kiongozi bora ndani ya kikosi hicho cha kocha Jose Mourinho.

Ikumbukwe kuwa, wiki mbili zilizopita, Mourinho alimueleza wazi Pogba mbele ya wachezaji wenzake kwamba hatampa tena kitambaa hicho cha unahodha kutokana na mgogoro uliopo kati yao.

Pogba alikaimu nafasi ya unahodha Man United ambayo ni ya beki wa kulia, Antonio Valencia, lakini kwa nyakati tofauti alinukuliwa akiponda mbinu za Mourinho na hata kubishana naye katika mazoezi mwezi uliopita.

Lakini mara baada ya kumalizika kwa mtanange wa wikiendi iliyopita ambao United walishinda mabao 3-2 dhidi ya Newcastle, ripoti zilidai kuwa Pogba aliibuka kuwa mchezaji mwenye ushawishi mkubwa kwa wenzake katika mapumziko, wakati kikosi hicho kilipokuwa nyuma kwa mabao 2-0.

Ilisemekana kuwa Mourinho alimtumia Pogba kuongea na wenzake kuhusu mabadiliko ya kiufundi ambayo yalichangia United kufunga mabao matatu yaliyowapa ushindi, suala ambalo limemuibua kiungo huyo na kusema ushawishi wake hauna haja ya kusindikizwa na kitambaa cha unahodha.

“Unajua hata ninapocheza timu ya taifa sifanyi hivyo kwa sababu nataka niwe nahodha, kuvaa tu jezi ya Ufaransa ni kitu kikubwa sana kwangu,” alisema Pogba, alipohojiwa na Kituo cha Habari cha Ufaransa, AFP.

“Kama una uwezo wa kuzungumza, huna haja ya kuwa nahodha. Na kwa ufahamu wangu, wapo viongozi wazuri uwanjani wasio na haja ya kuzungumza kabisa,” aliongeza Pogba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.