BAADA YA FIFA, BALLON D’OR NAO WAMEAMUA KUTUVURUGA

Bingwa - - IJUMAA SPESHO -

WIKI chache zilizopita, safu hii ya Danadana za Ubongo ilizikosoa tuzo za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Mbali na makosa mengi waliyokuwa wameyafanya Fifa, kubwa lilikuwa ni kuwaacha Mohamed Salah na Kevin De Bruyne katika kikosi chao cha mwaka.

Pia, binafsi sikushangazwa na uamuzi wao wa kumtaja Thibaut Courtois kuwa Kipa Bora, ila kilichoniacha hoi ni kwamba eti hakuingia katika ‘first eleven’ yao na badala yake nafasi hiyo alipewa David de Gea.

Tuachane na hayo ya Fifa na leo tuangazie kituko kingine kilichofanywa na waandaaji wa tuzo za Ballon d’Or, ambapo majina ya wachezaji 30 watakaoifukuzia tuzo hiyo kwa mwaka huu yaliwekwa hadharani mwanzoni mwa wiki hii na mshindi atatangazwa Desemba 3, jijini Paris.

Ni ngumu kuwataja wote ila itoshe tu kukudokeza kuwa Sergio Aguero, Gareth Bale, Cristiano Ronaldo, Kylian Mbappe, Lionel Messi, Luka Modric, Neymar, Paul Pogba, Mohamed Salah nao wamo.

Hata hivyo, binafsi bado nimebaki na maswali juu ya vigezo vilivyotumika kuwaingiza baadhi ya wachezaji katika kinyang’anyiro hicho.

Nikianza na Alisson Becker, binafsi sikuona sababu ya waandaaji wa Ballon d’Or kumweka katika kinyang’anyiro hicho, tena wakimfungia vioo David De Gea.

Ni kweli msimu uliopita Alisson alikuwa moto wa kuotea mbali akiwa na Roma, ambako aliweza kucheza mechi 17 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Pia, ubora wake langoni ulimpa nafasi ya pili nyuma ya Keylar Nevas, aliyetwaa tuzo ya Kipa Bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Lakini je, Allison aliipa nini Roma? Pia, ni tuzo gani binafsi aliyoibeba hadi kumalizika kwa msimu? Hakuna.

De Gea, licha ya Man United kuwa hoi msimu uliopita, bado aliweza kutwaa tuzo ya Kipa Bora. Ni kwa mazingira hayo ndipo inapoonekana wazi kuwa waandaaji wa Ballon d’Or wametudanganya.

Mario Mandzukic kuingia ‘top 30’ ya Ballon d’Or nako kuliniachia maswali. Ukiacha kufika fainali ya Kombe la Dunia akiwa na Croatia, ambako hata hivyo alifunga mabao matatu pekee, Mandzukic hakuwa msaada kwa Juventus wakati iking’aa msimu uliopita.

Katika mechi 43 alizoshuka dimbani akiwa na uzi wa timu hiyo kongwe mjini Turin, Italia, alifunga mabao 10 pekee, ambapo yale ya Ligi Kuu ‘Serie A’ yalikuwa matano tu.

Hakuna ubishi kuwa nafasi yake katika kinyang’anyiro cha Ballon d’Or ilistahili kuchukuliwa na Robert Lewandowski, ambaye msimu uliopita alipachika mabao 41, akaipa Bayern Munich taji la Bundesliga, na kuchukua tuzo ya mfungaji bora.

Sadio Mane naye alistahili kuingia? Binafsi naamini kinyume chake, yaani alipaswa kuachwa na ingependeza zaidi kuona Paulo Dybala akipewa nafasi yake.

Mane alifunga mabao 20 katika mechi za michuano mbalimbali, lakini ukweli ni kwamba hayakuipa chochote timu yake hiyo ya mjini Merseyside.

Unawezaje kumpa nafasi ya kuingia katika kinyang’anyiro cha Ballon d’Or na kumwacha Dybala, ambaye alifunga jumla ya mabao 26 kuipa Juve mataji ya Serie A na Coppa Italia msimu uliopita?

Mwisho, hebu jiulize, waandaaji wa Ballon d’Or walitumia kigezo gani kumpa nafasi Karim Benzema katika orodha yao ya nyota 30 wanaoifukuzia tuzo hiyo mwaka huu?

Benzema alikuwa katika kiwango kibovu msimu uliopita, akifunga mabao 12 pekee. Licha ya mabao yake matano Ligi ya Mabingwa, bado kiwango chake hakikuwa cha kuridhisha.

Mechi zake 32 za Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ zilimshuhudia akiingia kambani mara tano pekee, hivyo haikushangaza alipotoswa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kilichokwenda Urusi kucheza Kombe la Dunia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.