Emery

mguu mkubwa uliochana kiatu cha Moyes

Bingwa - - UCHAMBUZI -

KILA lilipotajwa jina la Unai Emery katika mawazo ya wengi wanamkumbuka kocha wa zamani wa Manchester United, David Moyes, aliyerithi mikoba ya Sir Alex Ferguson.

Unajua kwanini? Basi, hakukuwa na jingine zaidi ya kufananisha kile alichokifanya Moyes ndani ya miezi tisa aliyodumu na Manchester United, kisha kusubiri kitu gani Emery atakwenda kukifanya ndani ya Arsenal.

Moyes alifeli, ndiyo maana alifukuzwa ndani ya Old Trafford, kwa muda mfupi alishindwa kwenda na uhalisia wa timu hiyo iliyoachwa na Sir Alex ikiwa na kombe la Ligi Kuu England.

Na mwisho wa siku, wasifu wake ndani ya Manchester United ulisomeka kwa ufupi sana kama sekunde za kutema mate chini, imebaki stori na mifano kwa wengine tu hivi sasa.

Ilikuwa rahisi kumfananisha Emery na Moyes, sababu wote wameingia sehemu ambazo makocha waliokuwa awali walijenga misingi na tamaduni ya klabu hizo kwa zaidi ya miaka 20.

Kwa namna moja au nyingine, si rahisi kuondoa kile kilichowekwa na kuingiza chako kwa muda mfupi, ndio maana mara zote makocha wote walipewa mikataba mirefu ili kujenga ngome zao kupitia kile wanachokiamini.

Tuanzie hapa kwenye tofauti ya Emery na Moyes kwanza, mafanikio waliyopata katika timu zao kabla ya kuingia katika klabu hizo kubwa nchini England ni tofauti.

Kitabu cha Emery kina historia ya kuvutia na kupendeza juu karatasi ya wasifu ‘CV’ wake aliyoipeleka kwa mabosi wa Arsenal.

Kwa kifupi unaweza kusema tayari anajua njia za ushindi, kutokana na kile alichokivuna katika timu alizofundisha kabla ya kuingia Arsenal.

Achana na klabu ya Valencia, Spartak Moscow na nyingine, Emery alifanikiwa kujenga jina lake alipokuwa Sevilla, ambako alifanikiwa kushinda mataji matatu ya Ligi ya Europa mfululizo.

Huku kwa kipindi chote alichokuwa na kikosi cha PSG alifanikiwa kushinda taji la Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1 mara mbili, huyo ndiye Emery, aliyevaa viatu na koti la Arsene Wenger, ndani ya Uwanja wa Emirates.

Mapema wakati Ligi Kuu England inaanza, Arsenal alipangwa kucheza dhidi ya Manchester City na Chelsea, michezo ambayo klabu hiyo ya Emery walipoteza.

Mashabiki wa Arsenal waligawanyika, wapo walioamini kocha huyo haiwezi timu na wengine walisimamia katika muda wa kuijenga klabu hiyo iliyokuwa chini ya mikono ya Wenger, ambaye alipoteza nuru ya mafanikio. Mbili, tofauti nyingine ya Emery na Moyes, ipo katika misimamo yao. Kwa kipindi kifupi tu, Emery alikuwa muwazi juu ya kile ambacho atakifanya ndani ya Arsenal.

Ndiyo maana hakusita kuongea juu ya misimamo yake huku ikikumbukwa kuwa Jack Wilshere aliambiwa bila kupepesa macho kuwa hahitajiki.

Pia, alishikilia falsafa ambayo anaiamini kutokana na kile alichokiona na kwa wachezaji na kipi akifanye ili timu hiyo iende katika mstari anaouhitaji.

Tazama usajili alioufanya, kisha tulia kidogo, fuatilia mipango yake juu ya kuinyanyua klabu hiyo ambayo haijashinda taji la Ligi Kuu England kwa zaidi ya miaka 10.

Inawezekana matunda ya Emery yasionekane katika kipindi hiki cha karibuni sababu wapinzani wake kwa kiasi kikubwa wamewekeza fedha nyingi ndani ya uwanja kwa ajili ya kununua wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi.

Vilevile inawezekana akaondoka Arsenal bila kushinda taji la Ligi Kuu England, lakini akawa mmoja wa makocha waliofanya kazi kubwa kwa kipindi chote atakachokaa kwa kuijenga timu anayoihitaji.

Naamini hizo ndizo tofauti alizokuwa nazo na Moyes, ambaye kwa kiasi kikubwa ukubwa wa Manchester United ulimwelemea katika mabega na kupoteza matumaini ya wengi bila kujua anafanya nini na anakwenda wapi.

Kupoteza michezo miwili dhidi ya Manchester City na Chelsea, ulikuwa mwanzo mwema kwa Emery kutambua ni kipi anatakiwa kukifanya ili kuijenga timu anayoitaka.

Kwanza, alikutana na wapinzani ambao walikuwa imara zaidi ya Arsenal, kimbinu na kiuwezo kwa mchezaji mmoja mmoja ndani ya uwanja, wala halikuwa jambo la kushangaza.

Lakini kwa Emery ilikuwa ni njia sahihi ya kuisuka timu kupitia makosa yaliyojitokeza kwenye michezo hiyo, mpaka hivi sasa tunavyozungumza tunaitazama Arsenal iliyocheza michezo tisa bila kupoteza.

Wanacheza, wanafunga mabao na kufanya kile kitu ambacho Emery anakihitaji, inawezekana kuna kitu kikubwa zaidi anakipika pale Emirates.

Hofu yangu ipo katika michuano ambayo Arsenal wanashiriki msimu huu, ni ngumu kufanya vizuri kwenye Ligi ya Europa na Ligi Kuu kwa pamoja.

Kwa namna moja au nyingine, inabidi achague njia ya kupita ili kufikia malengo yake, hasa kwa upande wa Ligi ya Europa kutokana na kile alichokifanya Sevilla, labda kwa kushinda taji hilo na Arsenal.

Au ahamishie nguvu kubwa katika Ligi Kuu England kushinda na Manchester City, Liverpool, Chelsea, Tottenham na Manchester United katika mbio za ubingwa.

Binafsi naamini hawezi kufanya vizuri kote, kwa kiasi kikubwa wote waliofanikiwa kushinda taji la Europa, waliitupa Ligi Kuu na kuwekeza nguvu kubwa huko, lakini nje ya hapo atatudanganya, labda awe mtu wa kwanza kufanya hivyo.

Pamoja na hayo yote, mpaka sasa Emery ameonyesha mwanga mzuri ndani ya Arsenal kuliko Moyes aliyeiangusha Manchester United.

Mguu wa Emery ni mkubwa ndani ya kiatu kidogo cha Moyes, hakuna kingine zaidi ya kuchana kiatu hicho.

Kwa namna moja au nyingine, inabidi achague njia ya kupita ili kufikia malengo yake, hasa kwa upande wa Ligi ya Europa...

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.