TAIFA STARS USHINDI MUHIMU CAPE VERDE

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

TIMU ya Taifa Stars leo jioni inatarajiwa kushuka uwanjani kucheza na wenyeji Cape Verde katika mchezo wa Kundi L, kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Taifa Stars waliondoka juzi jijini Dar es Salaam kwenda Cape Verde kwa mchezo huo, utakaochezwa katika Mji wa Praia.

BINGWA tunautazama mchezo huo ni muhimu kwa Taifa Stars kushinda kwa kuwa itaiweka katika mazingira bora ya kufuzu fainali hizo.

Lakini ushindi kwa Taifa Stars utaongeza morali ya wachezaji kufanya vyema katika mchezo wa marudiano dhidi ya timu hiyo utakaochezwa Jumanne wiki ijayo, jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wetu BINGWA tunaamini Watanzania zaidi ya milioni 45 watafuatilia mchezo wa leo, lakini kubwa wakitaka ushindi kwa Taifa Stars.

Tunaamini kwamba, Taifa Stars imekwenda Cape Verde kwa lengo moja la kupata pointi tatu ili waweze kujisafishia njia ya kufuzu fainali za mwakani.

Tunasema hivyo tukijua kwamba, mara ya mwisho Tanzania ilifuzu fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 zilizofanyika nchini Nigeria, hivyo kiu yao ni kutaka kuona Taifa Stars ikifuzu kwa mara nyingine.

BINGWA tunasema kwa mchezo wa leo Taifa Stars wanatakiwa kucheza kufa kupona ili wasiache pointi tatu ugenini, kutokana na umuhimu wa mchezo huo.

Tunasema kwamba, Taifa Stars wanatakiwa kujua kwamba mchezo huo utakuwa ni mgumu kwa kuwa wenyeji nao watataka ushindi ili waweze kuongeza pointi tatu, hivyo ndani ya dakika 90 hawatakiwi kufanya makosa ambayo yanaweza kuigharimu timu.

Kama tulivyosema kwamba, ushindi ni muhimu kwetu kutokana na msimamo wa Kundi L, kwani tukishinda tunaweza kupaa hadi nafasi ya mbili za juu.

Kwa sasa Uganda ndio wanaongoza katika msimamo wa kundi hilo, kutokana na pointi nne wakifuatia Lesotho na Tanzania, hivyo Taifa Stars wakichanga vizuri karata zao wanaweza kuwamo katika safari ya kwenda Cameroon mwakani.

BINGWA na Watanzania wote tunaitakia kila la heri Taifa Stars na kama tulivyosema ushindi dhidi ya Cape Verde ni muhimu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.