Tajiri wa masikini

Bingwa - - HADITHI -

Ilipoishia Nilizidi kuona mabadiliko mengine kwa mke wangu, mabadiliko yaliyonikondesha na kuniweka katika wasiwasi mkubwa. Rumia hakuwa na mapenzi tena kama yale ya zamani alibadilika siku hata siku, lakini nilijipa moyo nikiamini muda wowote atarudi kama zamani, maana kwa kipindi hicho kila mtu alikuwa na mawazo juu ya hatima ya maisha yetu ya baadaye.

Baada ya miezi sita, hali yetu ya maisha ilianza kuwa mbaya, baadhi ya vyakula na mahitaji yalianza kuisha ndani ya nyumba, wadogo zangu Satia na Lukia wakiwa wamekwishaingia darasa la nane, walianza kutokwenda shule kutokana na kukosa ada. Nilishindwa kutoa hela kwenye ile akiba yangu kutokana na kuwa fedha hiyo ndiyo ilikuwa msingi wa maisha yetu yajayo. Nilijibana vyovyote vile ninavyoweza ili pesa ile nisiitumie, kwa sababu bila kufanya hivyo, nilijua kuwa nitaharibu kila kitu na kuwa kama masikini wengine wa Adorra na Katanga.

SASA ENDELEA

NYUMBANI kwangu hatukula tena tambi wala wali, chakula kilichoendelea kutusogeza, kilikuwa ni ugali na mboga za majani, wakati mwingine tulilalia matunda. Tulikula sana vyakula tunavyolima wenyewe, hakika ugumu wa maisha ulianza, si kwangu pekee, hata kwa familia ya mama yangu na ndugu zangu hali ilikuwa ni ile ile, Rumia alishakuwa amechoshwa kabisa na hali hiyo.

Kiukweli nilizidi kuchanganyikiwa, maana Rumia alishakuwa ameionyesha hasira yake ya wazi na jinsi alivyo ndani ya nafsi yake. Alichukia maisha hayo kwani ni kweli yeye kama aina fulani ya msichana, hayakuwa saizi yake. Yeye alishakuwa amezoea kutunzwa vizuri na Franco Mazimbe, mtu aliyekuwa akimlisha vizuri yeye pamoja na shangazi yake.

Rumia alianza kunichukia zaidi kwa jinsi hali ilivyozidi kuwa mbaya, pamoja na kuwa na hela nyingi ndani lakini bado sikuweza kupata kitu cha kufanya, sikutaka kuitumia pesa ile hata kwa kuwalipia ada wadogo zangu, wala kuitumia kwenye mahitaji mengine.

Ilibidi nisafiri hadi jijini Port Villa kwenda kuonana na mtu niliyemwona kama ndugu yangu Mhai wa Tofauti kijana Rahimu aliyekuwa msaada wangu wa siku zote. Nilikutana naye na kumwomba ushauri wa namna ya kufanya ili niweze kufungua biashara nyingine.

Lakini kwa kuwa mtu yeyote

wa kabila langu la Wapache, alikuwa akichukiwa na Wahai, ilikuwa ni ngumu kufanya biashara yake katika jiji hilo. Ilibidi Rahimu aniambie kuwa ili iwe rahisi kuanza maisha mengine ya biashara ni lazima niendelee kuutumia mgongo wake ili kufanya biashara katika soko hilo kuu la jiji Port Villa. Alinishauri kuwa pesa nyingi nilizokuwa nazo ni vema nikainganisha kwenye biashara yake ya viungo ili nami niwe sehemu ya umiliki wa biashara hiyo.

Ulikuwa ni ushauri wa maana sana na wenye kuniletea ukombozi, nilimshukuru sana Rahimu, maana ni watu wachache sana wenye uwezo wa kukubali kuchanganya biashara yake na mtu mwingine. Ukizingatia yeye alikuwa ni Mhai ilikuwa ni ajabu kuona anataka ushirikiano huo.

“Asante sana ndugu yangu Mungu akubariki kwa wema wako. Sitapoteza muda, haraka nitakuletea pesa nawe ufanye vile uwezavyo ili nami niweze kuyasogeza maisha, sina mwanga mwingine zaidi ya nuru yako,” niliongea kwa nidhamu nikishuka chini kumpigia magoti. Lakini alinikataza kuyashusha magoti yangu sakafuni.

“Usifanye hivyo Vanuell sisi wote ni wanadamu ni wajibu kusaidiana,” aliongea huku akininyanyua.

Wakati tukiongea hayo tulikuwa sokoni katika sehemu yake ya biashara, tukiwa tunaendelea na maongezi walikuja watu watatu, watu hao walikuwa ni wafanyabishara wa pale sokoni. Watu hao walimwambia Rahimu maneno yaliyoniumiza sana kiasi cha kunikatisha tamaa.

“Bwana Rahimu mtu huyu alikatazwa kufanya biashara katika soko hili hapa anafanya nini?” mmoja aliuliza.

Kwa hasira kidogo Rahimu aliinuka kwenye kiti na kuwauliza.

“Mnaona kuna matunda au mbogamboga hapa?”

“Tunakupa tahadhari tu asije akaleta tena biashara yake hapa sokoni, kwanza kuna Mpache anayefanya biashara katika soko hili?” aliongea mwingine.

“Kwa hiyo kama hayupo mnatakaje.”

“Hatuwataki Wapache hapa maana vyakula vyao haviko salama.”

“Kama anauza nguo au biashara nyingine tofauti na vyakula?” aliuliza Rahimu kwa hasira ile ile.

“Pamoja na hayo sisi hatumtaki hapa sokoni, alishahatarisha maisha ya Wahai wenzetu kwa kutuletea vyakula vya kwao vilivyo vichafu. Awe anauza nguo au biashara nyigine au ile ile hatumhitaji, kwanza eneo hili si la biashara nyingine zaidi ya

vyakula.”

“Sikilizeni nyinyi yeye kuwepo hapa haiwahusu biashara gani anataka kufanya, hilo pia si juu yenu. Alishakatazwa kuuza mboga na matunda basi aliitii agizo hilo ndio maana hafanyi tena, naomba muondoke hapa.

“Sawa pamoja na hayo sisi hatumhitaji, tutahakikisha hafanyi biashara yoyote hapa,” aliongea mtu mmoja kwa hasira kidogo.

Waliondoka pale eneo la Rahimu kwa jeuri na hasira zao nyingi. Niliumizwa sana na maneno yao, ulikuwa ni zaidi ya ubaguzi kiasi cha kunishangaza, nilijiuliza watu hao walikuwa ni wanadamu kama mimi au walikuwa ni viumbe kutoka sayari nyingine. Nilijisemea moyoni hata kama ulikuwa ni ubaguzi wa kikabila ule ulikuwa umezidi. Hata Rahimu alishangazwa na maneno yao.

Lakini kamwe sikutambua kuwa nyuma ya watu hao alikuwepo Franco, mtu aliyekuwa amewalipa kwa kazi ile, kazi ya kuhakikisha napatwa na magumu ya kufanya biashara katika soko hilo ili nisijipatie kipato, ili niwe masikini kama watu wengine wa Adorra na Katanga, lengo likiwa ni kumrudisha mpenzi wake wa zamani ambaye ni mke wangu wa ndoa, Rumia ninayempenda.

Rahimu alinifariji na kunitaka nisiwaze kuhusu maneno yao, aliniambia kuwa

suala hilo atalishughulikia yeye mwenyewe.

“Usijali rafiki yangu wewe zingatia mambo tuliyoongea, leta ile pesa ili biashara yangu iwe yako na yako iwe yangu, najua hakuna mtu atakayejua kuwa tunamiliki biashara moja.”

“Asante ndugu yangu lakini isije ikatokea nikakupotezea wateja wako, naogopa sana,” niliongea mimi kwa woga na huruma.

“Hilo usizingatie sana Vanuell hakuna chaguo zaidi ya hilo. Nami sina budi kufanya hivyo kwa sababu sitaki wewe na familia yako mfe kwa njaa, nikiacha hivyo, hakika Mungu ataniadhibu.”

“Asante sana ndugu ninamwomba Mungu azidi kukubariki.”

“Usijali Vanuell ila kwa sasa nenda kakae nyumbani kwa wiki mbili mimi nikiwa naandaa mazingira ya hapa sokoni. Nataka niongee na uongozi wa soko niwaeleze kuwa baada ya wewe kupoteza haki ya kufanya biashara ya matunda na mboga hapa sokoni, nimeamua kukuajiri kwenye biashara yangu ya viungo ili wakikuona wasianze kuleta maneno au wasiwasi wao.”

“Sawa kaka nashukuru sana,” nilimjibu fukara mimi kwa nidhamu ya hali ya juu. ********* Nilirudi Adorra nikiwa na furaha na matumaini ya kurejesha maisha mazuri,

nilimwona Rahimu kuwa ndiye Mungu wangu wa tatu. Nilipofika nyumbani nilimweleza Rumia kila kitu kuhusu matumaini hayo. Lakini hata hivyo hakuonyesha kufurahishwa sana na taarifa hiyo nzuri sikujua ni kwanini.

Tuliendelea kuishi maisha ya shida, mke wangu Rumia alifika ukomo wa uvumilivu, alianza kunichukia zaidi, alininyima haki yangu ya ndoa, hakuwa mtii tena kwangu, hasira yake ilikuwa ya karibu kiasi cha wakati mwingine kunimwagia hadi maji, usiku niliteseka kwa kukosa chakula cha usiku, niliishia kuyatazama mapaja yake mazuri na mwili wake uliomvutia kila mwanaume, nilimmezea mate kuku wangu mwenyewe. Kwa wiki mbili nilikuwa nimekosa haki yangu ya ndoa.

Jumamosi jioni nikiwa narudi nyumbani nilipishana na Franco Mazimbe aliyepita kwa kasi na pikipiki yake, maji machafu aliyoyapitia yalinimwagikia. Alipogundua kuwa ni mimi alisimamisha pikipiki yake na kunirudia.

“Habari yako fukara,” alinisalimia.

Sikumjibu nilibaki nikimtazama tu kwa hasira. Yeye aliendelea kuongea kwa kejeli nyingi.

“Hata usiponijibu lakini tambua jua kali linakuja kwako, naye Rumia atarudi kwenye kivuli changu na kutulia haa! haaa! haaa!” aliongea huku akinicheka.

Baadaye alipanda pikipiki yake na kuondoka mbele yangu. Aliniacha na wasiwasi mkubwa maana nilijua kuwa alikuwa ametoka nyumbani kwangu. Siku hiyo nilipanga kwenda kumuuliza Rumia kuhusu Franco Mazimbe. Siku zote sikuwahi kumuuliza kuhusu ujio wake nyumbani, lakini siku hiyo nilipanga kufanya hivyo kwa sababu mabadiliko ya Rumia yalikuwa makubwa sana.

Nilifika nyumbani na kumkuta Rumia akila viazi vya mayai na karanga za kizungu, pembeni akinywa soda aina ya Cola, moyo ulinilipuka paaaaaa! Nilianza kuhema kwa pupa huku nikimsogelea karibu kabisa na meza. Nakumbuka wakati naondoka nyumbani nilikuwa nimeacha maharage na ugali wa ngano, nilijiuliza chakula kizuri kama hicho ambacho hakipatikani kote Adorra wala Katanga alikuwa amekipata wapi.

Moja kwa moja nilijijibu mimi mwenyewe kuwa Franco Mazimbe alikuwa amemletea, hakika moyo uliniuma kupita kawaida, nilimtazama Rumia usoni, huku nikakaa taratibu karibu yake, yeye hakuwa na wasiwasi aliendelea kula kwa raha zote. “Mke wangu umepata wapi chakula hichi cha bei ghali?” nilimuuliza. Nini kitaendelea? Usikose kesho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.