Niyonzima ‘kuwasurprise’ Simba

Bingwa - - HABARI - NA WINFRIDA MTOI

KIUNGO wa Simba, Haruna Niyonzima, ameweka wazi kuwa tayari kocha mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, amemkubali kwa mazoezi anayofanya, anasubiri siku akipewa nafasi awaonyeshe Wanasimba vitu vipya.

Tangu Niyonzima amesajiliwa Simba, amekuwa katika kipindi kigumu cha kupata namba kikosi cha kwanza kutokana na kusumbuliwa na majeraha mara kwa mara.

Akizungumza na BINGWA jana baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani, jijini Dar es Salaam, Niyonzima alisema anaamini siku atakayoingia uwanjani atawafurahisha wapenzi wa Simba na watasahau yote yaliyopita.

Niyonzima aliweka wazi tatizo lililokuwa linamsumbua kuwa ni mguu, hali ambayo ilikuwa inampa hofu anapocheza na kufanya mazoezi chini ya kiwango kinachotakiwa na mwalimu.

“Jinsi ninavyofanya mazoezi ni tofauti na nilivyokuwa kipindi cha nyuma, kitu cha kwanza nilichokuwa na hofu nacho ni mguu wangu, sasa hivi nashukuru Mungu niko vizuri na ipo siku watu wataniona na watasahau kila kitu,” alisema Niyonzima.

Katika hatua nyingine, Niyonzima, amewashauri wachezaji wasiopata nafasi katika kikosi hicho wasikate tamaa, waishi kwa imani wakiamini ipo siku watacheza na kukubalika.

“Ninachowashauri wachezaji wenzangu ni kwamba waishi kwa imani, unajua unapojikwaa inakupa akili nyingine na kujisikia mwenye nguvu, hivyo wasikate tamaa.

“Katika maisha, sisi kama Waislamu, tunaamini kitu kinatokea kwa mipango ya Mungu, kwa mfano mimi mpaka leo naamini kuwa sichezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alipanga iwe hivyo, ila siamini kuwa siwezi kucheza tena, nitacheza tu.

“Mtu unaweza kujijua ni mzuri lakini uzuri utajulikana zaidi kutokana na vikwazo unavyokutana navyo, bado mpira tunaujua na nguvu tunazo, hivyo nisipocheza leo nitacheza kesho,” alisema Niyonzima.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.