MADEGA, KIFUKWE WAKATAA KUJITOSA UCHAGUZI YANGA

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - NA HUSSEIN OMAR

WAKATI Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), ikitangaza kuwa fomu za uchaguzi wa Yanga zinaanza kutolewa leo, viongozi wa zamani wa klabu hiyo, Francis Kifukwe na Imani Madega, wamekataa kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ndiyo iliyobeba jukumu la kusimamia uchaguzi huo baada ya ile ya Yanga kutokidhi mahitaji na sasa zoezi la kuchukua fomu linaanza rasmi leo kwa ajili ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mapema Januari 13.

Wakizungumza na BINGWA, Kifukwe na Madega, ambao walipata nafasi ya kuiongoza Yanga katika nafasi ya Mwenyekiti kwa nyakati tofauti, walisema kwa sasa wanawapisha watu wengine kutoa mchango wao.

“Mimi binafsi sina mpango wa kugombea nitabaki kuwa sehemu ya bodi ya wadhamini, kwani mpira wa sasa unahitaji watu wenye nguvu na mawazo mapya,” alisema Kifukwe.

Kwa upande wake Madega ambaye aliiongoza Yanga kwa mafanikio makubwa kabla ya kustaafu mwaka 2010 na nafasi yake kuchukuliwa na Lloyd Nchunga, alisema hana mpango wa kurudi tena kuiongoza klabu hiyo kongwe hapa nchini.

“Tumewaachia vijana nao waonyeshe uwezo wao, sisi wengine tutabaki washauri na wanachama tu, sifikirii kuchukua fomu kugombea,” alisema Madega.

Madega alisema licha ya kufuatwa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kuombwa kuchukua fomu katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti, lakini amekataa maombi hayo na kuwaambia kwa sasa hivi hafikirii kurejea tena katika nafasi ya uongozi.

Katika hatua nyingine tayari kuna baadhi ya matajiri akiwemo bosi wa GSM, Ghalib Mohamed, Abbas Tarimba, Mkumbo na wengine wametajwa kuwa wanaweza kurithi mikoba ya Manji.

Imeelezwa kuwa mabosi hao hivi sasa wanasubiri upepo mbaya upite, kwani kuna baadhi ya wanachama wa timu hiyo wameanza vurugu za kupinga uchaguzi huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.