Mo Banka hajaonewa, ila adhabu yake iwe fundisho

Bingwa - - MAONI | MTAZAMO | KATUNI -

KAMATI ya Kuzuia na Kupambana na Dawa zisizoruhusiwa Michezoni Kanda ya Tano Afrika (RADO), hivi karibuni kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imetangaza kumfungia Mohamed Issa ‘Mo Banka’, miezi 14 baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Mo Banka ambaye amesajiliwa na Yanga Julai mwaka huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, alikutwa na hatia hiyo ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni aina ya bangi, Desemba 9 mwaka jana baada ya kufanyiwa vipimo wakati wa michuano ya Cecafa iliyofanyika nchini Kenya.

Katika michuano hiyo ya Cecafa, kiungo huyo alikuwa moja ya wachezaji tegemeo wa Zanzibar Heroes ambaye pia alifunga bao la ushindi mchezo wa nusu fainali wakiitoa Uganda Cranes 2-1 kabla ya kufungwa mabao 3-2 na wenyeji Kenya, mchezo wa fainali kwa mikwaju ya penalti.

Baada ya hapo, kiungo huyo akawa kimya na zikawa zimesambaa taarifa kwamba alikutwa na hatia hiyo huko Kenya, lakini hakuna aliyejitokeza kulisemea hilo mpaka TFF kupitia kwa msemaji wake, Clifford Ndimbo, alipoamua kuliweka wazi.

Wakati taarifa hizo zikiwa zimezagaa mitaani siku za nyuma, binafsi niliwahi kuzungumza na baadhi ya viungozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ili kulitolea ufafanuzi lakini wakairushia mpira TFF ambao nao walikuwa wazito kulizungumzia hadi hivi karibuni walipoamua sasa kukata mzizi wa fitina.

Baada ya jambo hilo kuwekwa bayana, yameibuka maneno kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka hasa wale wa Zanzibar, wakidhani Mo Banka ameonewa huku akitajwa kiongozi mmoja pale TFF kwamba anahusika.

Mbali na kiongozi huyo wa TFF, pia ametajwa Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye, kwamba naye hakuridhika Zanzibar Heroes kutinga fainali michuano hiyo ndiyo maana wakafanya mpango kuwafitini baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho.

Baadhi ya mashabiki hao wanadai huyo kiongozi aliyeko TFF alitaka Mo Banka aende kusajiliwa Simba na alipoona ameenda Yanga, ndipo akakasirika na sasa anamfanyia mbaya. Imenishangaza sana.

Rafiki yangu mmoja kutoka Zanzibar akahoji, eti mbona timu nyingi zilikuwa zikishiriki michuano hiyo ya Cecafa lakini wachezaji wao hawakupimwa badala yake wakapimwa wa Zanzibar Heroes?

Alikwenda mbali na kudai Wazanzibari wote wameumizwa sana na jambo hilo ambalo mwenyewe ameliita la uonevu na kimya chao hicho eti kina mshindo, wakisubiri tu mamlaka zao zitoe tamko.

Binafsi nimewashangaa sana wanaosema Mo Banka ameonewa na eti kwa sababu anaichezea Zanzibar Heroes. Sasa kama mchezaji mwenyewe kwa mujibu wa taarifa kwamba alikiri anatumia dawa hizo zisizoruhusiwa michezoni, hao wanaomtetea wanapata wapi

ujasiri huo?

Nadhani huu si wakati wa wapenda michezo kuanza kuchukiana kwa vitu ambavyo vipo wazi. Mo Banka hajapimwa na Musonye wala huyo kiongozi aliyepo TFF ambaye baadhi wanamshutumu kwamba anamchukia kiungo huyo.

Nakumbuka katika michuano hiyo ya Cecafa, baada ya Zanzibar kuifunga Kilimanjaro Stars mabao 2-1, baadhi ya mashabiki na hata wachezaji waliporomosha matusi makali sana, hiyo ikanijengea picha kwamba huenda kuna kitu hakiko sawa.

Mashabiki hao kutokea Zanzibar walionekana wakiwa na furaha baada ya Zanzibar kuifunga Tanzania Bara na hakuna aliyewazuia ila kilichoharibu ni maneno ya kuudhi yaliyokuwa yakitoka midomoni mwao.

Huku Bara wadau wa soka walikuwa mstari wa mbele kusifia kandanda safi lililochezwa na Zanzibar Heroes, idadi kubwa walionekana kama kuunga mkono kikosi hicho lakini cha ajabu baadhi ya wadau wasiokuwa waungwana kutoka Zanzibar, wakatukana sana wakiwamo wachezaji.

Mimi nadhani kama Wazanzibari wanataka kupiga hatua waache imani zao kwamba wanaonewa, hii si sawa kabisa, hakuna anayependa kuwaonea.

Nakumbuka katika michuano hiyo ya Cecafa, baada ya Zanzibar kuifunga Kilimanjaro Stars mabao 2-1, baadhi ya mashabiki na hata wachezaji waliporomosha matusi makali sana, hiyo ikanijengea picha kwamba huenda kuna kitu hakiko sawa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.