Yanga yabeba kifaa Simba

Bingwa - - HABARI - NA WINFRIDA MTOI

TIMU ya soka ya Yanga Princess, imefanikiwa kumsajili mchezaji wa Simba Queens, Grace Tonny, kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajia kuanza mwezi ujao.

Yanga Princess imekata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu ya wanawake msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa katika Ligi Daraja la Kwanza iliyomalizika Oktoba, mwaka huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Maalim Saleh ‘Romario’, alisema kwa sasa wanaimarisha kikosi chao na tayari wameshasajili wachezaji wanane.

Alisema kwa kutambua ugumu wa Ligi Kuu Wanawake wanatengeneza kikosi cha ushindani, hivyo wachezaji 10 kati ya wale walioipandisha timu wameachwa.

“Ligi inatarajia kuanza Desemba, licha ya kwamba tulichukua ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza lakini kikosi chetu hakikuwa bora, hivyo ni lazima tutengeneze timu mpya,” alisema Romario.

Aidha, kocha huyo alieleza kuwa timu yao inatarajia kuanza mazoezi leo katika Uwanja wa Shule ya Msimbazi Center, jijini Dar es Salaam kujiandaa na ligi hiyo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.