Timu hizi Ligi Kuu mbele butu, nyuma mdebwedo

Bingwa - - ALHAMISI SPESHO - NA ZAINAB IDDY

WAKATI ligi mbalimbali duniani zikisimama kupisha mechi za timu za taifa, hadi sasa timu nne pekee za Ligi Kuu Tanzania Bara ndizo zimefungwa mabao machache na zilizofunga mengi zikiwa nne pia.

Timu hizo ambazo zimefungwa mabao machache ni Azam FC ambayo nyavu zake zimetikiswa mara mbili, Simba wakiruhusu mabao manne, Yanga matano na JKT Tanzania ikiruhusu nyavu zao kuchezewa mara sita.

Timu nne zilizofunga mabao mengi tangu msimu huu uanze zinaongozwa na Simba iliyofumania nyavu mara 23, ikifuatiwa na Yanga na Mtibwa Sugar kwa mabao 17, huku Azam ikifunga15.

Lakini wakati Simba, Yanga na Azam FC zikifunga mabao mengi na kuruhusu machache, huku JKT Tanzania ikifunga machache na kufungwa machache na Mtibwa Sugar ikifungwa mengi na kufunga mengi, kuna timu ambazo zimetia fora kwa kufungwa mabao mengi na kutofunga mengi.

BINGWA limechambua timu chache ambazo safu zao za ushambuliaji ni butu na mabeki wao ni mdebwedo.

1.BIASHARA UNITED Ikiwa inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, wamegeuka jamvi la wageni kutokana na kupokea vipigo mara kwa mara.

Timu hii iliyokuwa na washambuliaji mahiri kama Uhuru Selemani, Jarome Lambele na nyota wa kigeni kama Balora Nouridine (Burkina Faso), Astin Amos (Ivory Coast) lakini wamefunga mabao manne pekee.

Pamoja na safu yao ya ulinzi kuwa na mabeki kama Juma Mpangala, Wilfried Kourouma (Nigeria), langoni akiwa Alex Olumide (Guinea), lakini wameruhusu mabao tisa katika mechi zao 12 walizocheza.

2.ALLIANCE FC Hii nayo ni kama Biashara United, imepanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu lakini tayari wameshaanza kutabiriwa kurejea walipotoka kutokana na kiwango kibovu wanachokionyesha.

Timu hii iliyopo chini ya uongozi wa Shule ya Sekondari ya Alliance, imecheza mechi 13 na kubugizwa jumla ya mabao 19, wao wakifunga saba na wakijikusanyia pointi 10 pekee.

Safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho kutoka Mwanza, inaongozwa na Jamal Mtegete na Michael Chinedu, huku ngome yao ya ulinzi ikiwa chini ya Wema Sadoki, Godfrey Luseke, Israel Patrick na Hance Masoud.

3.RUVU SHOOTING Licha ya kuwa na uzoefu na Ligi Kuu baada ya kushiriki mara kadhaa, lakini bado imeshindwa kumaliza tatizo la ubutu kwa washambuliaji wao na kukosa umakini kwa safu ya ulinzi.

Ruvu yenye washambuliaji Hamis Mcha, Fullyzulu Maganga na Said Dilunga, huku upande wa mabeki safu yao ikiongozwa na Renatus Ambros, Tumba Sued, Mao Bofu na Abdul Mpambika, safu zote hizo zimeshindwa kuonyesha cheche baada ya kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 18 huku wao wakifunga mabao 10 kwenye michezo 13 waliyocheza na hivyo kushika nafasi ya 13 na alama 13.

4.NDANDA FC Chini ya kocha mzoefu wa ligi, Malale Hamsini, Ndanda inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama 13 katika msimamo wa Ligi Kuu wakiwa wamecheza mechi 13 hadi sasa.

Timu hiyo ya mkoani Mtwara ilinusurika kushuka daraja kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita na kama watashindwa kucheza vizuri katika michezo hii ya sasa, wanaweza kujikuta kwenye hali ngumu kwa sababu ya ongezeko la timu kwenye ligi.

Ndanda inayoongozwa na Atupele Green, Vitalis Mayanga na Kigi Makasi, katika safu ya ushambuliaji wamefanikiwa kufunga mabao tisa huku ngome ya ulinzi ikiruhusu kufungwa mabao 18 chini ya Aziz Sibo, Malika Ndeule, Rajab Rashid na Yassin Mustapha.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.