VIGOGO YANGA WAJA JUU

ZAHERA ATAKA ‘KUFIA’ JANGWANI

Bingwa - - MBELE - NA HUSSEIN OMAR

KUTOKANA na baadhi ya wanachama wa Yanga kupinga uchaguzi mdogo unaotakiwa kufanyika kufuatia agizo la Baraza la Michezo la Taifa (BMT), vigogo wenye majina makubwa wamewajia juu wanaopinga uchaguzi huo.

Vigogo hao wa Yanga wakiongozwa na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, wamevunja ukimya na kuwataka wanachama wanaopinga uchaguzi huo wa kuziba nafasi zilizoachwa ikiwamo ya aliyekuwa Mwenyekiti, Yusuf Manji na wajumbe wanne, kukubali uchaguzi huo ufanyike.

Ridhiwani akiwa na wenzake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde na Venance Mwamoto, waliwashangaa wanachama wenzao wanaopinga uchaguzi huo. Wakizungumza kwa nyakati tofauti vigogo hao wakiongozwa na Ridhiwani, walisema namna pekee ya kuinusuru Yanga kwa sasa ni kufanya uchaguzi huo.

"Nashangazwa na kilichofanywa na wanachama wa Yanga jana, kama mpenda maendeleo lazima watu wakubali mambo yabadilike, juzi wenzetu wamefanya uchaguzi lazima tukubali kuiga. Tutaendelea na malumbano hadi lini, hakuna maana ya kuendelea kupiga kelele na ndio maana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) wameingilia,” alisema Ridhiwani.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa timu hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Newala, Mtwara, George Mkuchika, alisema hakuna namna kwa timu hiyo kukwepa uchaguzi kwani kufanya hivyo ni kupinga maamuzi ya Serikali kupitia BMT ambao wametaka ufanyike uchaguzi.

“Uchaguzi hauepukiki, hakuna namna lazima wanachama watambue hilo, hakuna namna yoyote ya kupinga uchaguzi, ’’ alisema Mkuchika.

Naye Mwenyekiti wa Marafiki wa Yanga Bungeni, Mwamoto ambaye ni Mbunge wa Kilolo, Iringa na kocha wa timu ya Bunge alisema kwa namna yoyote lazima uchaguzi ufanyike ili kupata viongozi imara ambao watailetea maendeleo timu hiyo.

“Wapinzani wetu Simba wamefanya uchaguzi tayari sasa kwanini sisi tusifanye, naomba tuwe watulivu tupate viongozi ambao watailetea Yanga maendeleo,” alisema Mwamoto.

Hivi karibuni Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka iliyopewa na BMT, ilitangaza kuanza mchakato wa uchaguzi maalumu wa kujaza nafasi hizo zilizo wazi.

Kamati hiyo iliyochini ya Mwenyekiti, Ally Mchungahela, iliweka wazi kuwa zoezi la kuchukua fomu kwa wagombea litaanza Novemba 8 hadi 13, mwaka huu.

TFF ilikabidhiwa na BMT jukumu la kusimamia uchaguzi baada ya klabu hiyo kushindwa kuitisha uchaguzi kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja sasa, tangu Manji ajiuzulu Mei, mwaka jana.

Hatua hiyo imepingwa vikali na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo wakisema hawatakuwa tayari kusimamiwa uchaguzi wao na TFF, wakidai wao kama wanachama wanaweza kujisimamia wenyewe kila kitu bila kusimamiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.