STARS ITUMIENI VIZURI KAMBI YA AFRIKA KUSINI

Bingwa - - MAONI -

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kipo mafichoni nchini Afrika Kusini kujiandaa na mchezo wao wa kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) dhidi ya Lesotho.

Timu hiyo ambayo inanolewa na kocha kutoka Nigeria, Emmanuel Amunike, itashuka dimbani katika mchezo huo muhimu Novemba 18, mwaka huu.

Mchezo huo ambao Stars anatakiwa kushinda ili kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo, itakayofanyika Cameroon mwakani utapigwa kwenye Uwanja wa Setsoto, jijini Maseru nchini Lesotho.

Nahodha wa kikosi hicho cha Taifa Stars, Mbwana Samatta ataukosa mchezo huo wa Lesotho kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, lakini Amunike amemjumuisha kikosini kuwapa wenzake hamasa.

Kwasasa timu hiyo ya Taifa Stars inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi L, ikiwa na jumla ya pointi 5, baada ya kucheza michezo minne, wakishinda mmoja na kufungwa mmoja na sare mbili.

Kundi hilo linaongozwa na Uganda wenye pointi 10, nafasi ya tatu ikishikwa na Cape Verde wenye pointi nne na Lesotho ambao watakutana na Stars wakiburuza mkia wakiwa na pointi mbili.

Hivyo Stars wanapaswa kushinda mchezo huo dhidi ya Lesotho, ili wakija kumalizia mchezo wao wa mwisho dhidi ya Uganda wakiwa na point nane kibindoni ambazo zitawapa nguvu katika mchezo huo wa mwisho utakaopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Machi mwakani.

BINGWA tunasema wachezaji wa Stars watumie vizuri kambi hiyo ya Afrika Kusini, ili kuweza kushinda mchezo huo muhimu ambao utaisaidia timu hiyo kushiriki tena michuano hiyo ya Mataifa ya Afrika, kwa mara ya kwanza Stars ilishiriki mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria.

Kitendo hicho cha kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa maandalizi hayo kinapaswa kuwa hamasa kwao, kwa kujiandaa vizuri ili kucheza kwenye kiwango ambacho kitasiaidia timu kuibuka na ushindi.

Lakini pia miundo mbinu ikijumuisha viwanja na vitu vingine navyo ni sababu kubwa ya kuwafanya Stars, washawishike kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii ili wapate matokeo mazuri.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.