MKOSI WA KLOPP KUINYIMA LIVERPOOL MATAJI 2018-19?

Bingwa - - SPORTS -

MERSEYSIDE, England

ALIPOTEULIWA kuchukua mikoba ya kuliongoza benchi la ufundi la Liver Oktoba 8, 2015, mashabiki wa timu hiyo walikuwa na matarajio makubwa, wakiamini Jurgen Klopp anawarejeshea heshima yao.

Kipindi hicho, Klopp alikuwa ametoka kuipa Borussia Dortmund mataji mawili ya Bundesliga (2010-11 na 2011-12), tena akifanya hivyo mbele ya wababe wa soka la Ujerumani, Bayern Munich. Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, hadi sasa Klopp hajaipa Liver ubingwa wa michuano yoyote na hilo limeanza kuibua wasiwasi. Licha ya kukiri kuwa ameiwezesha Liver kuwa tishio, bado wengi wameanza kuamini kuwa huenda hawezi kuipa timu yao ubingwa. Msimu huu, tayari kuna shaka kuwa huenda Klopp na Liver yake wakaambulia patupu. Kwanza, wameshasukumwa nje ya Kombe la Ligi walipotandikwa mabao 2-1 na Chelsea. Pia, wako tayari kutolewa katika mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kutandikwa mabao 2-0 na Red Star Belgrade kwani mchezo ujao watakutana na PSG, kabla ya kuvaana na Napoli. Huko kwenye mbio za kuwania taji la Ligi Kuu nako hakuna matumaini makubwa ya kuwaona Reds wakilitwaa taji hilo. Bado ni mapema pia kuipa uhakika katika michuano ya Kombe la FA, hasa ikiwa wataelekeza nguvu kubwa kwenye vita ya ubingwa wa Ligi Kuu. Lakini sasa, mkufunzi huyo wa zamani wa Mainz 05, Klopp, ana rekodi mbaya ya kuvikosa vikombe vikubwa katika hatua za fainali. Katika msimu wa 2012-2013 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, michuano ya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), akiwa na Dortmund, alipangwa Kundi D lililokuwa na Real Madrid, Manchester City na Ajax. Aliiongoza Dortmund kumaliza mechi za makundi ikiwa kileleni baada ya kujikusanyia pointi 14. Hakuishia hapo, akatinga fainali kwa kuing’oa Madrid kwa kichapo cha jumla ya mabao 4-3.

Lakini sasa, alipoteza mtanange wa fainali dhidi ya Bayern, ambapo Bavarians walichukua ubingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.

Msimu wa 2015–16, akiwa na Liver, aliifikisha Liver fainali ya Kombe la Ligi (Carabao Cup). Katika hatua hiyo, walikutana na Manchester City.

Mtanange huo ulimshuhudia Fernandinho akiitanguliza Man City kabla ya timu hizo kwenda mapumziko, bao lililotokana na uzembe wa kipa, Simon Mignolet.

Bahati nzuri ni kwamba, Philippe Coutinho, aliisawazishia Liver katika dakika za majeruhi lakini timu yake ‘ikafa’ kwa penalti 3-1.

Ni kipindi hicho pia Klopp alipoipeleka Liver fainali ya Ligi ya Europa. Kuzifunga Manchester United, Borussia Dortmund na Villareal, kuliwafanya wengi wakaamini kuwa Liver inakwenda kutwaa ubingwa.

Lakini haikuwa hivyo kwani dakika 90 za mtanange wao wa fainali dhidi ya Sevilla, ulimalizika kwa Sevilla kuibuka kidedea.

Liver walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa straika wake, Daniel Sturridge, lakini kipindi cha pili kilikuwa kibaya kwao baada ya Kevin Gameiro, kusawazisha na Coke kutupia mawili, hivyo mchezo kumalizika kwa Sevilla kushinda mabao 3-1.

Mwisho, wengi watakumbuka mkosi huo ulivyomwandama Klopp msimu uliopita alipoingia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Madrid.

Huenda hiyo ndiyo itakayochukua muda mrefu zaidi kufutika katika kumbukumbu za Klopp. Ndiyo, baada ya kuiondosha Man City kwa jumla ya mabao 5-1, Liver ilipewa nafasi kubwa ya kuilaza mapema Madrid.

Kama ilivyo kawaida ya Klopp, timu yake ikatandikwa mabao 3-1 katika mechi hiyo ya fainali, adui wao mkubwa usiku ule akiwa na Gareth Bale aliyefunga mara mbili.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.