Basata yawataka wanaochezea fisi, nyoka kupata vibali

Bingwa - - IJUMAA SPESHO - NA HARRIETH MANDARI, GEITA

BARAZA la Sanaa Taifa (Basata), limewataka wasanii wa ngoma za asili wanaotumia wanyama kama fisi na nyoka kufuata utaratibu wa kupata kibali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii juu ya umiliki na kuwatumia.

Hayo yalisemwa juzi na Ofisa Habari Mkuu wa Basata, Agnes Kimwaga, mara baada ya kufungua rasmi mkutano uliojumuisha maofisa utamaduni kutoka mikoa yote ya Kanda ya Ziwa uliofanyika mjini Geita hivi karibuni.

“Kiutaratibu msanii anatakiwa aende Wizara ya Maliasili ili kupata kibali vinginevyo ni kukiuka sheria hivyo nawakumbusha wasanii kufuata utaratibu, nina uhakika wakifuatilia kibali watapata tu, utamaduni wa Tanzania unafifia kutokana na utandawazi sasa hivi wasanii wameanza kuiga vionjo vya nje jambo ambalo si zuri,” alisema Agnes.

Naye Ofisa Utamaduni wa Mkoa wa Geita, Yohana Galomwa, alisema bado kuna tatizo la kufanana kwa majina ya vikundi vya kwaya jambo ambalo linaleta mkanganyiko.

Aidha, akijibu hoja hiyo, Agnes, alisema Basata imeliona tatizo hilo na hivyo kuwaelimisha wasanii hao kuhakikisha wanasajili mapema majina ya vikundi ili kuepuka mkanganyiko.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.