SITA TU ZINATOSHA, MKWANJA KAMA WOTE LEO

Bingwa - - IJUMAA SPESHO - USICHANE MKEKA

BAADA ya kivumbi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi ya Europa, wikiendi hii tunarejea kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu ya England (EPL) ambapo michezo sita itachezwa kesho na mingine minne kuchezwa keshokutwa.

Kwa kuanza na mechi za leo, kama ilivyo kawaida ya Usichane Mkeka, hizi ni dondoo zinazoweza kukuongoza kupiga bao kama utabeti kwa kiasi chochote cha mkwanja.

CARDIFF CITY V BRIGHTON Kabla ya mchezo wa kesho, timu hizo zimeshawahi kukutana mara 67, ambapo Brighton wameshinda 23, huku wenzao wakiambulia ushindi katika michezo 22, na mingi ikimalizika kwa sare.

Brighton wataingia uwanjani wakiwa na morali zaidi kwani mechi yao ya mwisho kufungwa ni ile waliyochezwa dhidi ya Everton na hiyo ilikuwa Oktoba.

Utabiri: Cardiff 2 v 1 Brighton

LEICESTER CITY V BURNLEY Leicester City watarejea dimbani kesho wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Cardiff City. Kwa bahati nzuri, wanakutana na Burnley ambayo iko ovyo, imepoteza mechi tatu zilizopita.

Ubovu mkubwa wa Burnley unapatikana katika eneo lake la ulinzi, ambalo hadi sasa limeshapitisha mabao 13 katika mechi tatu mfululizo. Katika mechi nne zilizopita kati ya timu hizo, iliyokuwa nyumbani ndiyo iliyoshinda.

Utabiri: Leicester 2 v 0 Burnley

HUDDERSFIELD V WEST HAM Ushindi wao wa mabao 4-2 katika mchezo uliopita dhidi ya Burnley, uliwaokoa West Ham wasizikose pointi tatu katika mechi nne mfululizo.

Mechi mbili za msimu uliopita wa Ligi Kuu ziliwashuhudia West Ham wakishinda zote, ikiwamo kuwachapa wenzao hao mabao 4-1.

Huddersfield watarudi wakiwa na nguvu ya ushindi wa bao 1-0 walioipata kutoka kwa Fulham katika mchezo uliopita lakini kwa West Ham itakuwa ngumu kwao kutamba.

Utabiri: Huddersfield 0 v 1 West Ham NEWCASTLE V BOURNEMOUTH Newcastle United waliweza kuitandika Watford katika mchezo uliopita, hivyo huenda hali ya kujiamini imeanza kurejea kwa vijana hao wa kocha Rafa Benitez. Ilikuwa ni mechi yao ya kwanza kushangilia pointi tatu.

Watakutana na Bournemouth waliowahenyesha vilivyo Manchester United, hata kuwafanya Mashetani Wekundu hao kupata bao la ushindi katika dakika za majeruhi.

Ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Bournemouth kufungwa nyumbani tangu kuanza kwa msimu huu. Mechi ya mwisho kuzikutanisha Newcastle na Bournemouth ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Utabiri: Newcastle 0 v 1 Bournemouth

SOUTHAMPTON V WATFORD Southampton inaifuata Watford kwa hasira kwani katika mechi iliyopita walitandikwa mabao 6-1 na Manchester City. Ni mechi saba Southamton hawajaambulia ushindi, hivyo huenda wakataka kuanza na Watford.

Kwa upande wao, Watford nao wanarudi wakiwa na hasira inayotokana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Newcastle United, hivyo leo nyasi za Uwanja wa St. Mary zitawaka moto.

Mwaka huu, timu hizo zimekutana mara moja na hiyo ilikuwa kwenye mchezo wa Kombe la FA, ambapo Southampton walishinda kwa mbinde bao 1-0.

Utabiri: Southamton 1 v 0 Watford

PALACE V TOTTENHAM Crystal Palace hawajakaa sawa kwani katika mechi sita (za mashindano mbalimbali) zilizopita, hawajashinda hata moja, wamepoteza tano na kuambulia sare.

Wanakutana na Tottenham ambayo wameokota pointi tatu katika mechi nne walizocheza wakiwa ugenini hivi karibuni, kwa mujibu wa takwimu za Ligi Kuu pekee na si michuano mingine.

Changamoto kubwa waliyonayo Palace ni kwamba, Spurs wameshinda mechi sita kati ya saba walizokutana hivi karibuni.

Utabiri: Palace 0 v 2 Tottenham

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.