NANI ATUKUMBUSHE YANGA NI KUBWA KULIKO MANJI?

Bingwa - - IJUMAA SPESHO - HASSAN DAUDI 0685 183 040

HAKIKA inashangaza kama si kuacha maswali yasiyo na majibu juu ya kile kinachoendelea katika klabu ya Yanga ‘Watoto wa Jangwani’.

Kwamba klabu hiyo imekuwa ikiendeshwa bila mwenyekiti kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu sasa, sababu kubwa ikiwa ni baadhi ya wanachama na mashabiki wake kutokubaliana na uamuzi wa Yusuf Manji kuupa kisogo wadhifa huo!

Nani atukumbushe kuwa Yanga ni kubwa kuliko Manji? Hicho ndicho ninachojiuliza, nikiwa sehemu ndogo ya wadau wengi wa soka la Tanzania.

Wanachama na mashabiki wa timu hiyo wamevurugwa, wakishindwa kukubaliana na uamuzi wa tajiri huyo kuachia ngazi.

Binafsi sioni ubaya wowote wa mchango wa Manji kuthaminika kiasi hicho, ikizingatiwa kuwa ndiye aliyemaliza mgogoro wa muda mrefu klabuni hapo, ukiachilia mbali fedha zake kuipa jeuri Yanga, hasa katika soko la usajili.

Sipingani pia na hatua yake ya kujiuzulu, nikiamini alikuwa na haki ya kufanya hivyo kutokana na misukosuko aliyopitia kipindi fulani.

Hata hivyo, sidhani kama ni sahihi kwa wanachama na mashabiki wa Yanga wanaomng’ang’ania kutuaminisha kuwa kuondoka kwake ni tatizo ndani ya Yanga.

Ni kweli kwa muda mrefu fedha za bilionea huyo zimekuwa zikiipa jeuri Yanga, lakini isisahaulike kuwa hapa tunaizungumzia moja kati ya timu mbili zenye mashabiki wengi zaidi hapa nchini na Afrika kwa ujumla.

Kwa kuutazama mtaji wa mashabiki pekee, naiona Yanga ikimwacha mbali Manji, ikiwa tu kutakuwa na mipango thabiti, nikitolea mfano walichokifanya wenzao Simba kwa kuanza kujiendesha kwa mfumo wa hisa.

Yanga, iliyoanzishwa mwaka 1935, miezi michache baadaye ikazaliwa Simba, haitofautiani sana kiushawishi na Mamelodi Sundown, Orlando Pirates au Zamalek, ambazo pia zina idadi kubwa ya mashabiki Afrika Kusini, Misri na kwingineko barani Afrika.

Ukizitazama timu hizo hivi sasa, zina utajiri wa kutisha, ukichangiwa kwa kiasi kikubwa na fedha zinazotoka mifukoni mwa mashabiki kupitia mapato ya mlangoni na mauzo ya vifaa vya michezo, zikiwamo jezi.

Kwa mantiki hiyo, licha ya kutambua mchango wake, naamini Manji ni sehemu ndogo tu Yanga na si kama wanavyofikiri hao wanaomlazimisha kurejea kwenye kiti chake.

Mbaya zaidi, hata ukiwauliza kinachowafanya wamng’ang’anie Manji, hawatakuwa na sababu za msingi. Zaidi ya yote, usishangae kusikia wakikwambia ana fedha! Hicho ndicho wanachokitazama zaidi kwa bilionea huyo.

Nikiongezea katika hilo, kwao mafanikio ya Yanga yanatafsiriwa katika mambo matatu; matokeo mazuri ya uwanjani, kuifunga Simba katika mchezo wa ‘derby’, na kulinyakua taji la TPL.

Hawatakwambia kuwa chini ya Manji timu yao imefika walau robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika au kumiliki uwanja wa kisasa kama ilivyo Azam FC, ambayo ina miaka 11 pekee tangu ilipotinga Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL).

Wanachokisahau mashabiki na wanachama hao ni kwamba kwa umri wa Yanga, haiwezi kuendelea kuwa tegemezi kwa tajiri mmoja au kikundi cha watu wachache wanaojiita vibopa.

Nikisisitiza kile ambacho kimekuwa kikipigiwa kelele na wadau wengi wa soka hapa nchini, Yanga na klabu nyingine za soka ni taasisi zinazopaswa kujiendesha kutokana na vyanzo vyake vya mapato.

Katika mfumo wa soka la kisasa duniani kote, hakuna unakoweza kusikia kiongozi akitumia fedha zake kukamilisha usajili wa mchezaji, kulipa mishahara na posho, au kuajiri kocha.

Kuzuia hali hiyo, Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), lina sheria ya Nidhamu ya Utumizi wa Fedha (Financial Fair Play), ambayo inazipiga marufuku klabu kutumia mkwanja unaotoka nje ya mapato yake.

YUSUF MANJI

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.