Zahera: Jamani tuoneeni huruma

Bingwa - - HABARI - SAADA SALIM NA SALMA MPELI

KOCHA mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amewashukia wadau wa timu hiyo wanaowabeza wachezaji wake na kuwataka kuwaonea huruma kutokana na mazingira magumu wanayofanyia kazi ndani ya klabu hiyo.

Kauli hiyo ya Zahera ilikuja wiki hii baada ya timu yake kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na BINGWA jijini Dar es Salaam jana, Zahera, alisema iwapo mashabiki wa timu hiyo waliowalalamikia wachezaji kufanya vibaya wangejua hali za wachezaji hao na jinsi wanavyojituma kufanya vizuri, wasingesema walichokisema.

Aliwataka mashabiki wanaoongea vibaya wajaribu kuvaa viatu vya wachezaji wa Yanga ili wapate kujua ugumu wa maisha wanaopitia.

“Nashangaa sana mashabiki wanavyowalalamikia wachezaji kwamba fulani hafanyi vizuri, niwaombe siku moja wafike mazoezini na kupata muda wa kuzungumza na wachezaji kujua nini kinawasibu, kwa kufanya hivyo watajua tatizo liko wapi,” alisema Zahera.

Alisema alipofika mara ya kwanza na kupata muda wa kuzungumza na wachezaji hao, alitokwa na machozi kwa sababu kuna mambo ambayo kama binadamu wa kawaida lazima uelewe.

Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikipita katika kipindi kigumu cha ukata tangu alipoondoka aliyekuwa Mwenyekiti wao, Yusuph Manji, jambo lililosababisha baadhi ya wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kuikacha timu hiyo. Hali hiyo ya malimbikizo ya mishahara pia inadaiwa kusababisha migomo ya mara kwa mara kutoka kwa wachezaji.

Yanga wanaendelea kujifua katika Uwanja wa Chuo cha Polisi kilichopo maeneo ya Kurasini jijini Dar es Salaam, kujiandaa na mchezo ujao wa ligi ambapo watakuwa ugenini kucheza na Mwadui FC.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.