TFF yakana kumng’oa Kakolanya Yanga SC

Bingwa - - HABARI/TANGAZO - NA WINFRIDA MTOI

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemaliza mzizi wa fitina juu ya sakata la kipa wa Yanga, Beno Kakolanya, baada ya kusema halijatoa ruhusa ya kuondoka kwenye kikosi hicho cha Jangwani..

TFF wametoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho hilo imebariki Kakolanya kuachana na Yanga, huku akihusishwa kujiunga na mahasimu wao Simba.

Katika taarifa zinazosambaa zinadai kuwa kamati hiyo imemuweka huru kipa huyo na klabu ya Yanga inatakiwa kumlipa malimbikizo ya mishahara ya miezi miwili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana na Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo, ni kwamba habari zinazosambaa ni upotoshaji unaofanywa na watu wachache kwa masilahi yao binafsi.

Aidha, alisema hakuna kikao cha kamati kilichokaa na kujadili kuthibitisha kuwa Kakolanya yupo huru au kutakiwa kulipwa mishahara ya miezi miwili na Yanga.

“Taarifa inayosambaa si sahihi na kuendelea kusambazwa ni upotoshaji na kinyume na sheria ya mitandao ya kijamii, hivyo TFF inawataka watu wanaohusika kuacha mara moja,” alisema Ndimbo.

Kakolanya hajaonekana kikosini Yanga tangu kuvunjwa kwa kambi ya timu ya Taifa, Taifa Stars, wakati walipokwenda kucheza dhidi ya Lesotho katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Tayari Yanga imecheza mechi nne za Ligi Kuu Tanzania Bara bila kuwepo kwa kipa huyo, ambapo majukumu yake yamekabidhiwa kwa kinda, Ramadhani Kabwili na Klaus Kindoki.

Kindoki alidaka katika mechi dhidi ya Mwadui FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, ambayo Yanga walishinda mabao 2-1.

Kwa upande wa Kabwili alisimama langoni wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar ambayo Yanga walishinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, pamoja na ile ya JKT Tanzania waliyoshinda 3-0 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.