MTIHANI

Emery kukata mzizi wa fitina kwa Mourinho?

Bingwa - - MAKALA -

LIGI Kuu ya England itaendelea tena leo na kesho baada ya kutimua vumbi mwishoni mwa wiki iliyopita kwa timu mbalimbali kushuka viwanjani kusaka pointi tatu.

Ilikuwa wikiendi ya michezo mikubwa ndani ya ligi hiyo maarufu duniani, Arsenal waligawa dozi nzito ya mabao 4-2 kwa Tottenham ndani ya Uwanja wa Emirates huku Liverpool akifunga pazia kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Everton.

Pamoja na klabu hizo kupata ushindi bado Manchester City wameendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England na kupigiwa upatu wa kutwaa taji hilo kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo msimu uliopita.

Katika michezo ya Ligi Kuu England ambayo inatarajiwa kupigwa leo na kesho, Manchester United watawakaribisha Arsenal katika Uwanja wa Old Trafford baada ya kutoa sare ya mabao 2-2 na Southampton ndani ya Uwanja wa St. Mary.

Ni mchezo mwingine mkubwa kwa timu zote mbili, Arsenal ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 30 huku wenyeji wa mechi hiyo Manchester United wakisalia nafasi ya saba na pointi 22.

Kasi ya Arsenal chini ya Unai Emery, imezidi kuwa kubwa baada ya kushinda michezo zaidi ya 15 katika michuano yote waliyoshiriki msimu huu huku vijana wa Jose Mourinho, wakionekana kusuasua kwa kutokuwa na mwendelezo mzuri wa ushindi.

Lakini pamoja na hayo, kocha wa Arsenal, Emery, hana rekodi nzuri anapokutana na Mourinho ikiwa wamekutana kwenye michezo mitano ambayo iliisha kwa Mreno huyo kushinda mara nne na sare moja.

Mchezo wa kesho ni mtihani mkubwa kwa Emery ambaye hajawahi kupata ushindi dhidi ya Mourinho ambaye anasifika kwa kuwa na mbinu nyingi pindi michezo mikubwa inapokuwa karibu.

Hata hivyo, mwendo wa Arsenal unaweza kumshawishi kocha huyo raia wa Hispania kuwa wanayo nafasi ya kuvunja mwiko huo chini ya Mourinho kwa kuandika ushindi wake wa kwanza.

Mourinho na Emery walikutana nchini Hispania ambako mmoja alifundisha Real Madrid (Mourinho) na mwingine alikuwa Valencia na Sevilla (Emery) kwa vipindi tofauti.

Bado kocha huyo wa The Gunners anasaka ushindi wa kwanza kwa Mourinho na timu yake ya Manchester United ambazo zote kwa pamoja hawajawahi kushinda dhidi yao.

Ina maana kuwa endapo Emery akifanikiwa kushinda dhidi ya Manchester United hapo kesho, atakuwa amevunja rekodi mbili kwa wakati mmoja, ndio sababu hakuwahi kushinda dhidi ya The Red Devils wala Mourinho.

Wakati huo Valencia ilicheza dhidi ya Manchester United katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo ilimalizika kwa vijana wa Sir Alex Ferguson kushinda jumla ya mabao 2-1, mchezo wa kwanza uliopigwa Old Trafford ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na ule wa marudiano uliisha kwa ushindi wa bao 1-0 kwa United.

MOURINHO

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.