MR PUAZ

BOSI WCB ANAYEFICHUA YANAYOMKERA KUTOKA KWA HARMONIZE

Bingwa - - MAKALA - NA JESSCA NANGAWE

MIONGONI mwa mastaa wa Bongo Fleva ambaye kwa sasa hakauki midomoni mwa mashabiki wake ni pamoja na Rajab Abdul ‘Harmonize’ ambaye amekuwa akifanya vyema katika muziki wake na kuwavuta mashabiki wengi.

Harmonize ambaye ni zao kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), kwa sasa ni habari nyingine kutokana na uwezo wake kuendelea kukua na kujikuta akifurahia matunda ya kile anachokifanya.

Harmonize amekuwa akifanya vyema kupitia nyimbo zake kama Atarudi, Aiyola, Matatizo, Shulala na Happy Birthday ambazo zimekuwa na mapokeo mazuri kutoka kwa mashabiki zake huku zikizidi kumwongezea idadi kubwa ya mashabiki ndani na nje ya Tanzania.

Uwezo wa msanii huyu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na staa wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu kama Diamond Platinumz ambaye aliona kipaji chake na kuamua kukiendeleza hadi kuchangia mafanikio yake kwa kiasi kikubwa.

Baada ya Harmonize kuamua kusimama na kuweza kuwa msanii mwenye ushawishi mkubwa hasa kwa vijana wenzake, aliona ni vyema kuwa na uongozi ambao utaweza kusimamia kazi zake kutokana na ukubwa wa jina lake na mipango ya kujiendeleza zaidi kimataifa.

Joel Vincent mzaliwa wa mkoani Arusha, alipewa jukumu la kumsimamia msanii huyu ambaye kwa sasa anakiri kuchangia mafanikio yake kwa asilimia kubwa huku akiwa na ndoto nyingi za kumfikisha anga za kimataifa ili kuhakikisha muziki wake unamletea matunda mazuri.

Katika kuhakikisha kundi la Wasafi linakuwa na kupata wasimamizi wazuri, kiongozi wa lebo hiyo, Diamond, aliamua kusaka wasimamizi wa lebo hiyo akiwamo Sallam, Babu Tale, Mkubwa Fella, Makame pamoja na Joel ambao walipewa jukumu la kuwasimamia wasanii wa lebo hiyo.

Safari ya Joel ilianzia katika uandishi wa vitabu ambapo alikuwa akimiliki jarida lililojulikana kama ‘Usiku wa Leo’, ambalo lilikuwa likiandika habari za mastaa na ndipo alipoanza kukutana na mastaa kama kina Vanessa Mdee, Shetta, Chegge pamoja na Diamond ambaye walipokutana alijikuta akitua katika lebo ya Wasafi.

Anasema baada ya kukutana na Diamond na kumweleza mipango yake aliridhika na uwezo wake na ndipo alipomwingiza ndani ya lebo hiyo kwa lengo la kufanya kazi pamoja.

Mbali ya kusimamia wasanii, pia Mr. Puaz amekuwa akijishughulisha na biashara mbalimbali huku akimiliki jarida lake, pia kaigiza baadhi ya filamu za kibongo sambamba na kuandika vitabu mbalimbali vyenye kutoa elimu kwa jamii. Walivyofanyiwa ‘uhuni’ Kenya

Pamoja na kupata mialiko mingi nje ya Tanzania, lakini Mr Puaz ametaja changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kazi yao ikiwemo ile ishu ya kufanyiwa uhuni wakati wakijiandaa na shoo yao nchini Kenya.

Ishu iko hivi, anasema baada ya kuitwa na kampuni moja nchini Kenya walikwenda lakini saa chake kabla ya shoo walishindwa kumalizana na mabosi hao na kujikuta wakiingia katika wakati mgumu na kusababisha kuleta tafrani kubwa kati yao na mashabiki.

“Ni tukio ambalo lilituumiza sana ukizingatia sisi tulikuwa kibiashara, tulikubaliana kulipana kabla ya shoo lakini wenzetu walitaka kuleta uhuni na kusababisha sisi kuahirisha, ilitupa wakati mgumu sana kwa sababu mashabiki tayari walikuwa uwanjani na tulikuwa tunasubiriwa sisi tu, walishindwa hata kutulipia fedha ya hoteli na kutuacha kwenye mazingira magumu,” anasimulia.

MIPANGO YAKE NA HARMONIZE Joel maarufu kama Mr. Puaz, pamoja na uchanga wake katika tasnia ya burudani, amekuwa na ushawishi kwa staa huyo kuweza kupata michongo mbalimbali ya kufanya kazi katika nchi mbalimbali, ambapo ameweza kupata ziara katika nchi kubwa ndani na nje ya Tanzania.

Anasema amekuwa akihakikisha anaweka mipango ya kuhakikisha msanii wake anafanya vyema na kujitangaza zaidi kimataifa sambamba na muziki wake kutambulika zaidi kimataifa.

“Nashukuru Harmonize amekuwa akipata ziara nyingi za kuutangaza muziki wake, tumekuwa tukialikwa nchi mbalimbali na imetuletea matunda mazuri kwani kila tunapokwenda tumekuwa na matokeo mazuri ya kile tulichokifanya,” anasema.

HAPATANI NA UBISHI WA HARMONIZE

Joel anasema kero kubwa anayokutana nao dhidi ya msanii wake ni ubishi uliopitiliza ambao wakati mwingine unachangia kuharibu sehemu ya mipango yao mikubwa.

“Unajua Harmonize ni mbishi sana msimuone hivi, inafika kipindi ubishi wake unaathiri hadi kazi zetu, ananikwaza sana lakini nashukuru kazi zetu zinakwenda vizuri na matokeo yanaonekana, mbali na hilo ni mtu safi sana na anachapa kazi ila pia namshauri kupunguza starehe,” anasema.

KAFANYA KAZI NA SHETA, NAY Mbali ya kufanya kazi na msanii huyo, pia Joel alishafanya kazi na wasanii wakubwa hapa nchini kama Shetta pamoja na Ney wa Mitego ingawa hawakudumu nao muda mrefu.

“Nilishafanya kazi na Ney wa Mitego pamoja na Shetta ingawa haikuwa kwa kipindi kirefu, ni watu ambao nilikuwa nikishibana nao na niliweza kuwasaidia katika kuendeleza muziki wao,” anasema.

Kumtengeneza Harmonize anga za Bieber

Anasema miongoni mwa wasanii wakubwa ambao tayari wameanza mipango ya kufanya nao kazi ni pamoja na mastaa wakubwa nchini Marekani, Kanye West, Justine Bieber pamoja na TI ambao tayari ameanza mazungumzo na mameneja wao kwa ajili ya kufanya kazi pamoja.

Anasema si hao tu bali kuna wasanii wengi wakubwa ambao wana mipango ya kufanya kazi pamoja na kutokana na ushawishi wa kazi za msanii huyo, wamekua pia wakipata mialiko mbalimbali.

ZIARA YA MAREKANI YAJA NA NEEMA

Joel ambaye ziara yake na Harmonize inatarajia kukamilika Oktoba 20, nchini Marekani, amesema imekuwa na manufaa makubwa kwake na kwa msanii wake kwani imeweza kuwakutanisha na watu mbalimbali ambao wameweza kuwasapoti kwa kiasi kikubwa.

“Nashukuru tangu tuanze ziara yetu kwanza mwitikio umekuwa mkubwa tofauti na tulivyofikiria, tumepata sapoti hasa ya Watanzania wengi wanaoishi huku, Harmonize amekuwa na ushawishi mkubwa sana huku kwa wenzetu hilo kwangu nimelipokea kama ushujaa kuona kumbe tunakubalika kwenye nchi za watu kwa kiasi hiki,” anahoji Mr Puaz.

Nashukuru tangu tuanze ziara yetu kwanza mwitikio umekuwa mkubwa tofauti na tulivyofikiria, tumepata sapoti hasa ya Watanzania wengi wanaoishi huku, Harmonize amekuwa na ushawishi mkubwa sana huku kwa wenzetu hilo kwangu nimelipokea kama ushujaa kuona kumbe tunakubalika kwenye nchi za watu kwa kiasi hiki,” anahoji Mr Puaz.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.