ABDALLAH SAID ‘DALLA’

Chipukizi Bongo Fleva aliyevutwa na Salome ya Dully Skyes *Aelezea Bob Junior alivyomfungia mlango, ajipanga kuhamishia majeshi Sauzi

Bingwa - - JUMANN | UNAKOSAJE? - NA GLORY MLAY

WASANII chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva siku zote wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali zinazotishia safari yao ya mafanikio kupitia fani hiyo, japo wapo baadhi yao ambao wamekuwa wakitoka kiulaini.

Miongoni mwa wasanii ambao walipata bahati ya kushikwa mikono na kung’ara ndani ya muda mfupi ni Rajab Abdul ‘Harmonize’ ambaye aliibuliwa na Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Hata kama Harmonize alihaha kufikia alipo lakini huwezi kumlinganisha na Diamond Platinumz ambaye safari yake ya mafanikio katika muziki, ilikumbana na changamoto lukuki huku akikosa mtu wa kumshika mkono.

Kwa mujibu wa simulizi ya safari yake kimuziki, ni mama yake pekee aliyekuwa akihaha kusaka fedha katika mazingira magumu na wakati mwingine kuuza vidani vyake ili kumwezesha mwanawe kutimiza ndoto zake.

Lakini leo hii Diamond amekuwa nguzo muhimu kwa wasanii wengine kupata mafanikio, pia akisaidia kuendesha maisha ya wengi waliopo nyuma yake kuanzia uongozi wake na timu nzima inayounda kundi la Wasafi Classic Baby (WBC).

Abdallah Said ‘Dalla’ ni msanii chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva ambaye naye amekumbana na changamoto nyingi hadi kufika aliposasa.

Msanii huyo kwa sasa ametambulisha wimbo wake mpya unaiotwa Itakuwa So, ambao umeanza kufanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya redio na runinga nchini.

BINGWA lilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano alipotembelea ofisi za New Habari (2006) Limited, zilizopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam ambao ni wazalishaji wa magazeti ya BINGWA, DIMBA, MTANZANIA na RAI ambapo alielezea safari yake hadi kufika alipo sasa.

HISTORIA YAKE Jina langu ni Abdallah Said kwa jina la kisanii ni Dalla, akiwa amezaliwa jijini Dar es Salaam na elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Ilala na kuhitimu darasa la saba mwaka 2007, lakini hakuweza kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na matatizo ya kifamilia.

“Baada ya kumaliza shule ya msingi nilijiingiza katika muziki wa Bongo Fleva na nikafanikiwa kurekodi baadhi ya nyimbo kama Nibembeleze, lakini hazikuweza kufika popote kutokana na kutokuwa na ubora.

“Baada ya hapo nilivyoona muziki haueleweki, niliamua kuondoka kwenda Tanga kwa ndugu zangu ambapo nililima na kuuza mazao na nilipata faida kubwa na sasa nimerudi kuanza upya muziki,” anasema Dalla. KWANINI MUZIKI Dalla anasema ameamua kurejea katika muziki kwa kuwa ni kipaji ambacho kilikuwa ndani yake tangu akiwa mdogo, ambapo alikuwa akiimba katika matamasha mbalimbali ya shule aliyosoma na kuonyesha kipaji cha hali ya juu.

“Nilikuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzangu pamoja na walimu kutokana na tungo zangu za kishairi, nilikuwa pia nikiwaburudisha wazazi wakati wa hafla za kutoa tuzo na matamasha mengineyo,” anasema.

ALITEMVUTIA Dalla anasema aliyemvutia kwenye tasnia hiyo ya muziki ni mkali wa Bongo Fleva, Dully Sykes, kutokana na uimbaji wake mzuri tangu zamani.

Anasema Dully Sykes ndiye aliyemsababisha kushindwa kuendelea na masomo kwani alitamani kuwa kama yeye.

“Kipindi Dully anatamba na ngoma yake ile ya Salome, nilitamani sana kuwa kama yeye kwani nilikuwa naamini kwamba tungeendana, nampenda na ninamuheshimu sana kutokana na kazi yake.

“Japo kipindi naanza kazi hii ya muziki nilimfuata kwa ajili ya msaada akanikubalia, lakini mwisho wa siku hakuna msaada wowote ambao niliupata kutoka kwake, alikuwa akinipa ahadi zisizotekelezeka…njoo leo, mara kesho; hivyo nikaamua kuachana na muziki nikaenda kijijini kulima,” anasema.

CHANGAMOTO Dalla anasema amepitia changamoto mbalimbali kama kukataliwa na baadhi ya wasanii ambao aliwafuata kuomba msaada wao wa kimuziki, akiwamo Raheem Nanji ‘Bob Junior’, lakini alikuwa akimpa ahadi hewa na wakati mwingine akimfungia milango kila alipokwenda nyumbani kwake.

“Changamoto ni nyingi hata wakati nilikuwa na nyimbo yangu, nilienda kwa mtayarishaji T Touch, sikuweza kupata nafasi ya kuonana naye kwani alisema hawezi kuonana na wasanii chipukizi, yeye anachotaka ni wale wenye majina tu,” anasema.

MIKAKATI YAKE Anasema mikakati aliyonayo kwa sasa anatamani kwenda kuishi Afrika Kusini kuendeleza kipaji chake cha muziki.

Anasema uongozi wake unaomsimamia katika kazi zake, unahamishia makazi huko hivyo hana budi kuongozana nao kwa ajili ya kwenda kukuza kipaji chake.

“Kule kuna wanamuziki wengi wazuri, naamini nikienda maisha yangu yatakuwa mazuri na nitapata umaarufu na nitaweza pia kupata nafasi ya kufanya kazi zangu na wasanii wakubwa wa nchi mbalimbali…nitajituma kadiri ya uwezo wangu ili nipate jina,” anasema Dalla.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.