Monalisa anavyowakimbiza akina Wema, Uwoya

Bingwa - - JUMANN | UNAKOSAJE? - NA ZAINAB IDDY

STAA wa Bongo Movie, Yvonne Cherrie maarufu Monalisa, ameendelea kuwadhihirishia wapenzi wa tasnia hiyo kuwa yeye bado ni bora kutokana na kuendelea kupata tuzo mfululizo, akiwafunika wenzake lukuki wakiwamo Wema Sepetu, Irene Uwoya, Aunty Ezekiel na wengineo.

Kwa mara nyingine, nyota ya Monalisa imeendelea kung’ara baada ya usiku wa juzi kufanikiwa kupata tuzo ya ‘Woman of Africa Icon of Substance’ zilizofanyika nchini Uganda.

Hii ni tuzo ya tatu kwa mwaka huu kutwaliwa na Monalisa, baada ya ‘African Prestigious Award’, aliyoshinda kama msanii bora wa kike Afrika aliyokabidhiwa mjini Accra, Ghana, Aprili.

Baada ya tuzo hiyo ya Aprili, Monalisa, alitwaa nyingine mwezi uliofuata iliyopewa jina la Heshima ya Uongozaji Bora wa Filamu wakati wa tamasha la filamu la The African Festival (TAFF) lililofanyika nchini Marekani.

Katika tuzo iliyotolewa Ghana, Monalisa alikuwa akichuana na wasanii wengine maarufu, akiwemo Lupita Nyong’o ambaye ni mwigizaji wa Hollywood mwenye asili ya Kenya na Jack Apia kutoka Ghana.

Kwa hapa nyumbani, Monalisa ana tuzo ya ZIFF (Zanzibar International Film Festival) ya mwigizaji na mwongozaji bora wa filamu mwaka 2010, lakini pia mara kwa mara amekuwa akipata mialiko ya matamasha ya filamu nje ya nchi.

Uwezo wa Monalisa katika kazi yake, unazidi kumweka kwenye ramani nyingine kwani licha ya kutosikika sana katika mitandao ya kijamii, lakini ameendelea kufanya kazi kubwa katika kuinua na kutangaza sanaa hapa nchini.

Ni wazi tuzo ya ‘Woman of Africa Icon of Substance’ imeendelea kumpa heshima Monalisa na

kumtofautisha na wasanii wenzake wa kike nchini ambao wanaonekana ni maarufu kuliko yeye.

Kwanini Monalisa? Ni swali linalotembea katika vichwa vya wapenda burudani wengi, hususanwa sanaa na hii inatokana na uwepo wa wasanii ajina zaidi yake,wengi wenye m lakini yeye ndiye mwanamama pekee anayeonekana kuibeba Tanzania kimatifa. Wapo akina Wema, Jackline, Irene Uwoya, Aunt Ezekiel na wengine wengi, lakini wote hao, Monalisa ameweza kujitofautisha nao kwa kiasi kikubwa baada ya kuibeba vizuri Bendera ya Tanzania.

Ni ukweli kuwa Monalisa ni zaidi ya wasanii wengine wengi wa kike kwani wakati yeye anaitangaza Tanzania, wenzake kila kukicha wameendelea kuzungumziwa zaidi katika mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyo na faida kwa taifa la Tanzania.

Kila uchwao, wasanii wenzake wa kike wamekuwa wakisikika katika vyombo vya habari kwa skendo na kiki, ndicho kitu pekee kinachomtofautisha yeye na wengine.

Kiuhalisia huenda wapo watu hawamfahamu kabisa Monalisa, lakini utakapolitaja jina la Wolper, Irene Uwoya, Wema na wengine, watakuwa wanawafahamu vilivyo kutokana na jinsi walivyoamua kuyaweka maisha yao na kusahau kuwa wao ni kioo cha jamii.

Pongezi kwa Monalisa na ni wazi anastahili kuigwa kwa kile anachokifanya kwani amedhihirisha ule usemi unaosema ‘mwanamke akiwezeshwa, anaweza’ kutokana na matunda yake yanayoonekana.

Monalisa anaendelea kufanya mambo makubwa katika taifa lake licha ya kuwa kimya kwani licha ya tuzo anazopata, lakini

mama huyo wa watoto watatu, ameweza kuanzisha miradi mingi ya kukuza sanaa, ukiwamo ule wa klabu ya uigizaji katika shule za msingi na sekondari ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mtwara.

Ili sanaa ikue, inahitaji watu kama Monalisa ambao wanajitambua na kutambua majukumu yao kiasi cha kulifanya taifa la Tanzania kung’ara kimataifa kwenye anga za sanaa.

Ni nadra sana kulikuta jina la Monalisa katika mambo ya kipuuzi kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wa filamu na sanaa nyinginezo hapa nchini.

Ufike wakati wasanii wa kike nchini wajitambue na kujua majukumu yao lakini si dhambi hata kukopi maisha ya Monalisa kwa masilahi yao na taifa kwa ujumla, hii itajenga heshima kwao kwani kuna maisha nje ya sanaa yao ya leo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.