MB Golden

Mkali wa Bongo Fleva anayepaisha Kiswahili Marekani Atamba kufungua shoo za Davido, Tiwa Savage

Bingwa - - JUMANNE SPESHO | UNAKOSAJE? - NA CHRISTOPHER MSEKENA

KUTOKA Portland Oregon, Marekani, msanii wa kizazi kipya, MB Golden,ameendelea kuipaisha lugha ya Kiswahili kupitia sanaa ya muziki anayoifanya kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto kadhaa.

Hivi karibuni MB Golden anayetamba na nyimbo kama Kibega na Wara Wara, amefanikiwa kufanya mahojiano na BINGWA na kufunguka mengi yanayohusu maisha na sanaa yake kwa ujumla, karibu.

BINGWA: Mashabiki wanataka kufahamu historia yako kwa ufupi kuhusu familia mpaka ulivyohamia Marekani na kuendelea kufanya muziki.

MB Golden: Baba yangu ni Mtanzania na mama ni Mkongo, kuna kipindi Wakongo walikuwa wanasakwa Tanzania kwa hiyo mama alikamatwa wakamrudisha kwao na wakati huo alikuwa anawasiliana na baba ambaye alikuwa ni mgambo.

Baba akaingia Kongo huko walipokutana ndiyo wakazaliwa dada na kaka yangu mkubwa, wakarudi Tanzania ndiyo nikazaliwa mimi mkoani Kigoma, nilipofika miaka minne tukahamia Msumbiji tukakaa miaka 12 ndiyo tukapata nafasi ya kuja Marekani mwaka 2012 na kabla ya hapo nilikuwa dansa wa msanii mmoja aliyekuwa anafahamika kama Ngasa na nilikuwa nimekulia kwenye dini ila nilipofika huku sasa hivi sina dini.

Nikaanza kuimba, nikarekodi wimbo mmoja ambao kaka mkubwa akaanza kunisapoti, shoo zikaanza kuingia mpaka leo hii.

BINGWA: Muziki unahitaji uwekezaji mkubwa kwenye audio na video je, unafanya jitihada gani kuhakikisha haukwami katika shughuli zako za muziki?

MB Golden: Ninamshukuru Mungu kwa sababu amenipa vipaji vingi vya kuimba, kucheza mpira, kuchora nk, mwanzoni ndiyo nilikuwa nakwama lakini sasa hivi shoo zinalipa, kwa shoo moja kuimba nyimbo tano kwa dola 500 si mbaya pia nafungua shoo za wasanii wakubwa Afrika hapa Marekani, jambo linalonisaidia kurekodi audio na video bila tatizo.

BINGWA: Wasanii gani hapa Bongo unafuatilia kazi zao?

MB Golden: Wasanii ninaowakubali ni Bob Junior ambaye tayari tumefanya nyimbo kubwa tatu bado hatujazitoa mwakani nitakuja Tanzania kufanya naye video, Diamond Platnumz, Harmonize, Mbosso na Q Chief ni watu ambao wana mchango mkubwa kwangu.

BINGWA: Changamoto zipi unakutana nazo katika kufanya muziki wa Kiswahili hapo Marekani?

MB Golden: Unajua mimi nafanya muziki kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, utaona nilipotoa wimbo wangu unaitwa Wamoyoni, watu wengi huku hawakuipokea vizuri kwa sababu wengi ni Wamarekani walikuwa hawaelewi nilichoimba, lugha nilikuwa ni tatizo hiyo ndiyo changamoto japo nakomaa nayo kwa sababu Bongo Fleva ndiyo muziki niliouchagua.

BINGWA: Kuna siri gani ya wewe kuonekana kwenye majukwaa na wasanii wakubwa kama Davido, Iyanya, Diamond Platnumz na wengine?

MB Golden: Wakati ninafanya shoo na Davido nilikuwa tayari nimetoa nyimbo zangu za Kibega na Wara Wara ambazo ni ngoma kubwa sana, nikaanza kupata shoo kubwa na kabla ya Davido na Iyanya tayari nilifanya shoo na Tiwa Savage kule Texas, juzi tu nimefanya na Harmonize sema nilikuwa nimelewa sana nilikuwa mimi na promota DMK Global.

BINGWA: Nje ya muziki huwa unapenda kufanya starehe gani?

MB Golden: Napenda sana kucheza mpira, kuchora, kufanya matembezi na marafiki, kunywa pombe na kujiachia na wanawake.

BINGWA: Unadhani kwanini inakuwa ngumu kwa wasanii wa Afrika Mashariki hasa Tanzania kupenya Marekani?

MB Golden: Wengi hawajaomba visa ya kuja Marekani, kwa sababu niliwahi kuongea na Q Chief nilitaka nimualike huku Marekani lakini akaniambia tatizo ni hilo, kwa hiyo ninachoona mimi wasanii wanaweza kupata shoo huku lakini wakawa hawana hata ‘Passport’.

BINGWA: Mwaka unaelekea ukingoni, je, umewaandalia nini mashabiki zako?

MB Golden: Hapa Marekani naamini hakuna msanii anayefanya ‘African Bongo Fleva’ kunishinda mimi, kabla ya mwaka kuisha nadhani kwenye Desemba 10 nitatoa video mpya na mwakani nitaendelea kuachia kazi ambazo tayari nimerekodi nasubiri ‘director’ wangu arudi kutoka New York tufanye video. BINGWA: Asante kwa ushirikiano. MB Golden: Shukrani pia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.