BABY MADAHA NYOTA ALIYEKWAMISHWA KIMUZIKI NA RUSHWA YA NGONO

Bingwa - - JUMANN | UNAKOSAJE? -

NA JEREMIA ERNEST MIAKA 10 iliyopita jina la Baby Madaha lilianza kusikika muda mfupi baada ya kutamba kwenye shindano la kuvumbua vipaji la Bongo Star Search (BSS), lililofanyika mwaka 2008.

Kutamba kwa jina hilo kulitokana na jinsi alivyofanya vizuri na kushika nafasi ya pili wakati Misojo Mkwabi akiibuka kidedea.

Baby Madaha alijijengea jina na kujipatia umaarufu kwa mashabiki wa muziki baada ya kuachia wimbo wake wa Amore.

Licha ya hivi sasa kutosikika mara kwa mara kwenye sekta ya muziki, bado jina la Baby Joseph Madaha linazungumzwa na wapenzi wa kazi zake na bila shaka wanatamani arudi tena kwenye ‘gemu’.

ASILI YAKE Asili ya wazazi wa Baby Madaha ni Mwanza, ila kutokana na kuendesha maisha yao kwa kufanya biashara, msanii huyo alizaliwa nchini Msumbiji.

Alianza elimu ya msingi mjini Maputo, Msumbiji kisha sekondari akasomea Kenya kabla ya kurejea nchini na kusoma kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Ikizu, mkoani Mara.

Miaka michache baadaye alianza masomo ya uandishi wa habari katika Chuo cha Dar es Salaam School of Jounalism ‘TSJ’, kabla ya kuchukua Shahada ya Kwanza ya Elimu ya Sayansi ya Siasa na Historia katika Chuo Kikuu Huria.

ALIPOANZA SANAA Baby Madaha ameieleza safu hii kuwa alianza kuimba akiwa shule ya msingi na mara kwa mara alipendelea kuimba nyimbo za msanii maarufu wa wa Marekani, Rihanna.

Anasema mwaka 2008 alienda BSS kujaribu bahati yake katika shindano hilo.

“Nilienda kwenye usaili wa BSS na nilifanikiwa kupita kwa kishindo hadi fainali nikawa mshindi wa pili,” anasema Madaha.

Anaongeza kuwa baada ya shindano hilo ndipo ilipoanza safari yake ya muziki hadi kupata mashabiki ndani na nje ya nchi. FAIDA NA CHANGAMOTO KATIKA SANAA

Akizungumza na safu hii anasema faida alizopata katika sanaa ni kumjengea nyumba mama yake, pamoja na kujulikana nchini na kumrahisishia mambo yake mbalimbali.

Kwa upande wa changamoto, Baby Madaha anasema rushwa ni moja ya changamoto kubwa aliyokumbana nayo kwenye kazi yake.

“Rushwa ni tatizo kubwa, nilikutana nayo wakati naanza sanaa na hata sasa nakabiliana nayo,” anasema Baby Madaha na kuongezea kuwa kutongozwa na watu tofauti wakija na sera ya kumsaidia kutoka kimuziki, nayo ni changamoto kubwa aliyokutana nayo. KILICHOMTOA KWENYE RAMANI YA MUZIKI

Anasema kilichompoteza kwenye muziki ni uongozi mbaya aliokutana nao akiwa hapa nchini, hivyo akaamua kwenda Kenya ambako hali ilikuwa mbaya zaidi kwake.

Baby Madaha alichukuliwa na lebo iitwayo Candy n Candy ya nchini Kenya mwaka 2013, hivyo alilazimika kuondoka

nchini.

“Nilivyoona hapa muziki haulipi nilienda Kenya lakini niliyokutana nayo huko ni bora ningebaki Tanzania,” anasema Madaha.

Alieleza kuwa baada ya kumaliza mkataba na lebo ya Candy n Candy, aliamua kurudi nchini na kusimamisha harakazi za muziki kwa muda mpaka atakapopata lebo nzuri inayoweza kumpa manufaa.

YUKO WAPI NA MIPANGO YAKE KATIKA SANAA

Anasema anapatikana Mbezi Beach ambako anafanya biashara zake kama kuendesha pub ambayo ameipa jina lake ‘Baby Madaha Pub.’

Pia anajishughulisha na biashara ya duka la nafaka ambazo anazitoa mikoani na kuleta Dar es Salaam kwa ajili ya kuziuza kwa jumla.

Anasema kwa upande wa muziki kuna lebo ambayo yupo kwenye mazungumzo nayo, watakapoafikiana basi atarudi kwenye ramani kwa kufanya mapinduzi.

Aidha, anasema hawezi kuacha mwaka huu uishe bila kufanya kitu katika tasnia ya muziki.

“Napenda muziki, ni kitu kilichopo ndani ya damu yangu, nimepanga kufunga mwaka kwa kutoa ngoma moja kali ambayo nafanya na mtayarishaji Allan Mapigo,” anasema Baby Madaha.

Akizungumzia masuala ya kujenga familia, Baby Madaha anasema bado hajafanikiwa kufunga ndoa wala kupata mtoto, akidai kwamba kuolewa kwake si jambo la lazima kwani anaamini si kila mwanamke lazima aolewe.

“Kuolewa si lazima cha msingi ni kuishi katika maisha mazuri ambayo unaweza kuyamudu. Haina haja ya kulazimishana kuoa au kuolewa,” anasema Baby Madaha.

“Napenda muziki, ni kitu kilichopo ndani ya damu yangu, nimepanga kufunga mwaka kwa kutoa ngoma moja kali ambayo nafanya na mtayarishaji Allan Mapigo,”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.