TUTU CALLUGI AELEZEA JINSI ALIVYOJIUNGA NA WENGE MUSICA BCBG

Bingwa - - KONA YA BOLINGO -

KUTOKA katikati ya Jiji la Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kona ya bolingo leo inakujuza jinsi mwanamuziki na rapa maarufu nchini humo, Yombo Lumbu ‘Tutu Callugi’, alivyojiunga na bendi ya Wenge Musica BCBG 4x4.

Haikuwa rahisi au kazi ndogo kwa mwanamuziki kujiunga na bendi hiyo mpaka uwe na kipaji halisi na cha kweli cha muziki.

Miongoni mwa wanamuziki kadhaa waliopata bahati ya kujiunga na kundi hilo ni mwimbaji, Tutu Callugi, ambaye baadaye aliamua kuwa rapa.

Hivi karibuni Kona ya Bolingo (KB) iliyanasa mahojiano ya mwanamuziki huyo alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha habari za burudani.

Callugi anaeleza kuwa haikuwa kazi rahisi kupata nafasi ya kujiunga na bendi hiyo hasa kutokana na umri aliokuwa nao kwa wakati huo, alikuwa na miaka 16 tu.

Aliendelea kueleza kuwa alikuwa na kaka zake wawili aliokuwa na urafiki wa karibu ambao ni Daddy Bakoena na Eddy Hilk Barracuda, waliokuwa jamaa zake wa karibu na Werrason.

Hawa walimweleza kuwa nina kipaji kikubwa cha kuimba, walipomweleza akawatuma wanipeleke ili apate kunisikiliza ninavyoimba.

“Kabla ya kwenda kwa Werrason ili anisikilize, Barracuda na Bakoena, walisaidia sana wakati nikijifua, nikazifanyia mazoezi ya kutosha nyimbo karibu zote za Wenge,” anasimulia Callugi.

“Wakati nimepelekwa kufanyiwa majaribio ya kuimba, palitokea msiba wa kaka yake na mdau mkubwa wa muziki, Tchatcho Mbala. Kwa vile alikuwa mtu wa karibu sana na bendi, iliamuliwa iende ikamfariji kwa kupiga shoo msibani.” Callugi anaelezea kuwa alipelekwa kufanya majaribio na mtihani wake wa kwanza ukawa kwenye msiba wa kaka yake na Mbala, mara tu baada ya shughuli ya mazishi kufanyika.

Baada ya kupanda jukwaani, Werrason akataka upigwe wimbo Kalay Boeing, ambapo kwenye baadhi ya kipande aliimba Manda Chante wakati uliporekodiwa lakini akaitosa bendi.

Kipande alichoimba yeye alitakiwa aimbe kwanza Aimelia Lias ‘De Mingongo’, alipomaliza Werrason akaamrisha Callugi na yeye aimbe.

Callugi alipoimba wanamuziki wote walibaki midomo wazi wasiamini kama ni yeye aliyekuwa anaimba, kwani aliimba kwa ufasaha mkubwa kama alivyokuwa akiimba Manda Chante.

Werrason alifurahi sana akamtaka aimbe wimbo mwingine, Callugi akaimba wimbo uitwao Douglas Ilumbe na kuzidi kuwapagawisha wanamuziki wote.

Mashabiki nao hawakubaki nyuma kwani nao walimshangilia sana wakitaka arudie tena kuziimba nyimbo ‘Once more’.

“Shoo ya msibani ilipoisha Werrason akawaambia Titina Alcapone na Patient Kusangila, wasithubutu kuniacha.”

Pengo la Manda Chante likawa kama limezibwa na Callugi pamoja na Aimelia, kwani wote walikuwa na uimbaji unaolandana naye.

Siku chache baada ya msiba huo kupita, Wenge walipiga shoo ndani ya ukumbi wa Invest Hotel jijini Kinshasa, walipopanda jukwaani Lias alitakiwa aanze kuimba na baadaye Callugi.

“Kiukweli mwenzangu Lias yeye alikuwa tayari ameshaajiriwa, ilinibidi nifanye juhudi kubwa ili na mimi niajiriwe,” anasimulia Callugi.

Callugi akaendelea kutiririka kuwa kilichokuwa kizuri kwake, sauti yake iliendana kabisa na ya Lias kwani lengo la bendi lilikuwa ni kuziba kwa usahihi pengo lililoachwa na Chante.

Alipoulizwa swali kwanini aliamua kuwa rapa badala ya kuimba, alikuwa na haya: “Baada ya kufanya shoo nyingi jijini Kinshasa, baadaye ilipopatikana safari ya Ulaya kupiga shoo wanamuziki wote walienda ila mimi tu.”

Alielezea kuwa bendi ilikuwa na wanamuziki 26 na nafasi zilizotakiwa ni wanamuziki 25 tu, hii ilimpa uchungu wa kumfanya akomae kwenye kujifua zaidi ili apate nafasi kwa siku za usoni.

“Niliona kwa kuwa Lias ameaminiwa zaidi kwenye nafasi tuliyokuwa tukiimba, nikaamua kujiongeza kwa kuanza kurapu. Nilipomweleza Werrason kuwa naweza kurapu alinipa nafasi, sikumwangusha,” anasema Callugi.

Anasimulia kuwa alipopewa nafasi ya kurapu haikuwa kazi ndogo, kwani tayari alikuwepo rapa mahiri namba moja, Roberto Wunda ‘Ekokota’.

“Kilichonifanya nikubalike zaidi kwenye rapu zangu ni kule kujitofautisha na Ekokota, kwani mimi nilikuwa nikirapu huku ninaimba kitu kilichonifanya nishangiliwe sana na mashabiki,” anasimulia.

Baadaye safari ya Ulaya ilipotokea alijumuishwa kundini akiwa kama rapa namba mbili wa bendi akisaidiana na Ekokota.

Tokea hapo aliaminiwa moja kwa moja, kwani katika ziara zote za bendi ndani ya DRC na nje alishiriki kikamilifu.

Uwezo wake wa kurapu ndani ya bendi hiyo ulionekana rasmi ilipotolewa albamu Pentagon, kwani hata wewe mwenyewe ukifuatilia vizuri utaiona shughuli yake humo akipokezana na Ekokota.

Kuna kipindi fulani katikati ya mafanikio kwenye kazi yake, Calluji alisimamishwa kufanya kazi katika bendi hiyo kwa tuhuma kwamba alimtolea lugha ya matusi mke wa Werrason ambaye alikuwa ni mmoja wa wakurugenzi na mwasisi wa bendi hiyo. Simulizi hii itaendelea tolea lijalo, nakusihi ufuatane nami ili uweze kujua nini alichokiongea Callugi kuhusu tuhuma hizo pamoja na mengine mengi.

Niliona kwa kuwa Lias ameaminiwa zaidi kwenye nafasi tuliyokuwa tukiimba, nikaamua kujiongeza kwa kuanza kurapu. Nilipomweleza Werrason kuwa naweza kurapu alinipa nafasi, sikumwangusha

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.