KISA KANTE... MASHABIKI WAMCHANA SARRI

Bingwa - - MBELE -

MASHABIKI wa Chelsea hawamwelewi Maurizio Sarri, wakisema hawaoni sababu ya kocha huyo kutomtumia N’Golo Kante katika eneo la kiungo wa ulinzi.

Kwa madai yao yaliyoanza mara tu walipotandikwa mabao 3-1 na Tottenham, Kante ndiye anayeitendea haki nafasi hiyo na si Jorginho anayependekezwa na mkufunzi huyo wa kimataifa wa Italia.

Utetezi wa Sarri ni kwamba, Kante si mzuri anapokuwa kiungo wa ulinzi, tofauti na Jorginho au Cesc Fabregas, ambao wamekuwa wakiisaidia Chelsea wanapokuwa katika nafasi hiyo.

Kuelekea mchezo wao wa mikikimikiki ya Ligi ya Europa dhidi ya PAOK, Sarri alisema: “Kama mnavyojua, napenda kuchezesha kiungo (wa ulinzi) ambaye amekamilika kiufundi, kama Jorginho au (Cesc) Fabregas. Simtaki Kante katika eneo hili.”

Hata hivyo, kauli yake hiyo haikuwapoza baadhi ya mashabiki waliodai Sarri ameshindwa kumtendea haki Kante, wakiamini amekamilika zaidi katika eneo la kiungo wa ulinzi kuliko Jorginho.

Mmoja kati ya mashabiki hao, aliyejitambulisha kwa jina la Norman #Blxck, kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa twitter aliandika: “Madai ya Sarri kwamba Jorginho ni kiungo mzuri wa ulinzi kuliko Kante. Hiyo inaonesha ni kwa kiasi gani kocha wetu hajui soka.”

Kwa upande wake, shabiki mwingine anayeitwa Denis Emlyn, aliandika hivi: “Ni bora nimfukuze Sarri na nimrudishe Jorginho kule Napoli kuliko kumuuza Kante.”

Jorginho alikaribia kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Manchester City, wakati wa majira ya kiangazi ya mwaka huu, lakini Sarri alimdandia juu kwa juu na kumsajili kwa kitita cha pauni milioni 57.

Kante, ambaye saini yake imekuwa ikiwanyima usingizi mabosi wa PSG ya Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’, alitua Stamford Bridge mwaka juzi akitokea Leicester City, ambayo akiwa staa wao eneo la kiungo, waliutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.