Straika anayetakiwa Jangwani atoweka Ndanda

Bingwa - - HABARI/TANGAZO - NA WINFRIDA MTOI

STRAIKA wa Ndanda FC, Vitalis Mayanga, hajaonekana katika kikosi hicho tangu alipomaliza mechi ya timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri chini ya miaka 23, Kilimanjaro Warriors, Novemba 20 mwaka huu.

Kuna tetesi kwamba mchezaji huyo anafukuziwa na timu nyingi za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akitajwa zaidi kutua Yanga katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.

Akizungumza na BINGWA jana kwa simu kutoka mkoani Mtwara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Khalid Adam, alikiri kumkosa straika huyo katika mechi ya juzi dhidi ya Mbao FC waliyotoka suluhu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Alisema kuwa taarifa alizopewa ni kwamba, mchezaji huyo yupo kwao mkoani Shinyanga na ana matatizo ya kifamilia.

“Nimeanza kwa sare mechi yangu ya kwanza ila nashukuru, hata hivyo kikosini alikosekana Mayanga ambaye hajarejea kambini tangu alipomaliza mechi ya kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Burundi,” alisema.

Hata hivyo, BINGWA lilimtafuta Mayanga ili kuzungumzia sababu ya kutoonekana kambini, ambapo alisema anasumbuliwa na malaria na maumivu ya enka lakini si kama ameondoka.

“Sijaondoka Ndanda mimi ninaumwa nipo nyumbani, nikipona nitarudi, kuhusu suala la kutakiwa na Yanga hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa,” alisema Mayanga.

Naye Ofisa Habari wa klabu hiyo, Idrissa Bandari, alielezea kuwa Mayanga ana ruhusa ya kutoka kwa uongozi kwa kuwa ana matatizo ya kifamilia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.