Fiesta, Wasafi Festival ni fursa kwa wasanii wetu kimataifa

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

IKIWA chanzo kikuu cha mapato ya wasanii ni maonyesho, basi naamini sasa ndio wakati wao wa kufanya kazi kikamilifu na kuwa karibu na mashabiki wao kupitia Fiesta, Mziki Mnene na Wasafi Festival, sasa kelele za kunyimwa shoo zitapungua.

Kupitia matamasha haya matatu makubwa naamini kilio cha njaa na kubaguliwa kitakuwa kimefika mwisho huku kazi ikibaki kwa wasanii wenyewe kuweza kufanya kazi nzuri ambazo zitawasisimua mashabiki.

Kinachotakiwa kwa sasa ni kutunga nyimbo zenye tija, kuzingatia maadili bila kusahau kuburudisha ili kuweza kuwafanya mashabiki wasichoke kuwaona kwa kuwa matamasha haya ya muziki yanapishana.

Ukiachilia mbali nyimbo zinazotakiwa kuzingatia maadili, pia umiliki wa jukwaa ili kuleta ushawishi kwani wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya, wanafanya maonyesho yao kwa kujisikia mno bila kujali watu wamekusanyika pale ili kuja kuona burudani kutoka kwao, wakiwa na msisimko wa kuona mtu anakonga nyoyo zao kikamilifu.

Tunategemea maonyesho haya wasanii hawatafanya kwa sifa ya kuitwa na fulani, bali watafanya kwa kuangalia maslahi ili kuweza kuendelea kumudu kuwepo katika tasnia kwa muda mrefu na kufika levo za kimataifa.

Kama watafanya kazi kwa mtindo huo basi naamini ile njaa na kelele za shoo ambazo walikuwa wakililia wasanii wetu kwa kipindi kirefu sasa itaisha, kwa kuwa tayari kuna hizo shoo kubwa tatu ambazo zinazunguka karibu mikoa yote ya nchi yetu.

Kupitia hili tunategemea wasanii wetu wapate fursa zaidi ya kuwika anga za kimataifa na si kutegemea wachache kama ilivyo sasa, imani yangu ni kila mwaka kwenye tuzo za kimataifa tutaweza nyakua tuzo nne hadi tano kupitia wasanii wengi na si mmoja kama ilivyo sasa. Pamoja na hayo pia, tunawaamini waandaji wa matamasha haya hasa Fiesta ambalo linamiaka zaidi ya 10, Mziki mnene nalo limepiga hatua sasa ni miaka 4 mfululizo, huku Wasafi wao wakiwa ndio wanaanza watawasaidia wasanii na kuwavusha hapa

walipo.

Mbali na wasanii pia kuna wafanyabiashara katika sehemu mbalimbali ambazo wasanii wanapita, hivyo katika mkusanyiko wa watu wengi lazima bidhaa muhimu ziwepo hii pia ni fursa nyingine.

Wasafi Festival iliyoanzishwa na msanii mwenyewe tena aliyekwishavuka anga za kimataifa ina mwaka wa kwanza tu, lakini ameweza kupeleka tamasha lake hadi kwa majirani zetu Kenya katika miji yake mikuu miwili yenye ushindani yaani Mombasa na Nairobi.

Hii ni hatua kubwa mno nina imani mwaka wa pili itaenda nchi nyingine na ndio maana nikasema hii ni fursa kwa wasanii wa Tanzania na muziki wao, kuhakikisha unakuwa tishio Afrika kitu kikubwa ni kuweza kuwateka mashabiki katika uimbaji wa nyimbo bora na utumbuizaji mzuri jukwaani utakaoweza kuwavuta mashabiki pembe zote Afrika.

Mbali na wasanii pia kuna wafanyabiashara katika sehemu mbalimbali ambazo wasanii wanapita, hivyo katika mkusanyiko wa watu wengi lazima bidhaa muhimu ziwepo hii pia ni fursa nyingine.

Hivyo wazo langu mimi ni kuomba Serikali iyaangalie matamasha haya kwa jicho la tatu ili iweze kuleta maendeleo na kunyanyua uchumi wa nchi kwa wananchi wake.

Napenda kuwapongeza waandaaji wa matamasha haya kwa kuweza kunyanyua uchumi wa nchi kwa njia ya burudani, kikubwa zaidi ni wawe na ushirikiano utakaoweza kupeleka gurudumu la maendelea mbele.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.